Tulizoea kusikia walimu wakilalamika, lakini safari hii wameamua kulia, na machozi yao yameonekana kupitia nia waliyoionyesha. Walimu sasa wametangaza mgogoro uliobeba mimba dhidi ya Serikali; ambako usipotatuliwa unatarajiwa kuzaa mgomo usio na kikomo.

Kabla hata sijausikia mgogoro huo kupitia vyombo vya habari, nilishapata taarifa za ujio wa mgomo huo. Kwenye simu yangu nilishapokea meseji nne zinazofanana kutoka kwa marafiki zangu wanaojua mimi ni mwalimu. Bila shaka wanayo kumbukumbu hiyo kwa sababu nimewahi kufundisha kama mwalimu wa muda kidato cha tano na sita; kwa masomo ya Baiolojia na Kemia pale Shule ya Sekondari Karatu wilayani Karatu.

Kimsingi madai ya walimu si mapya, lakini safari hii wamekuja na kipaumbele kipya, msisitizo mpya na sababu mpya. Wakati zamani kilio cha walimu kilikuwa ni kulipwa malimbikizo yao, safari hii kipaumbele chao kikubwa ni nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100. Zamani mgomo wa walimu wote kwa wakati mmoja ulionekana ni jambo gumu kwa sababu si walimu wote waliokuwa wakidai malimbikizo.

Lakini kwa sasa msisitizo umewekwa mpya ambao ni ule wa nyongeza ya mshahara. Kwa kipaumbele hiki, watafiti wa mambo tunaona kinaweza kuwapa hamasa walimu wote kushiriki kikamilifu katika mgomo. Ingawa kwa sasa msisitizo wa mgogoro wao unaonekana kuwa katika kuongezewa mshahara – walimu wamekuja na sababu mpya kabisa.

Zamani walikuwa wakisema inawezekana walimu kuongezewa mishahara ikiwa taifa litakusanya kodi ipasavyo, ikiwa viongozi wataacha kujipendelea, ikiwa rasilimali za nchi zitagawanywa vizuri na ikiwa Serikali itaweka kipaumbele katika elimu. Baada ya kuona gea hii imetumika pasipo mafanikio yaliyotazamiwa, sasa walimu wameibuka na sababu ya ulinganisho. Wanahoji inakuwaje wao walipwe kidogo wakati wengine wanalipwa kingi?

Kwa ufafanuzi wao kupitia vyombo vya habari pamoja na ‘stori za mitaani’ wananung’unika kuona mfanyakazi wa ngazi ya cheti katika sekta ya afya au kilimo analipwa maradufu ya mshahara wa mwalimu kwa ngazi hiyo hiyo.

Wanatoa machozi kusikia daktari wa ngazi ya shahada ambaye hadi sasa analipwa mara tatu ya mwalimu wa shahada; akidai kuongezewa mamilioni. Kwa midomo yao wamejipambanua kama wanyonge kwa sababu ya kiwango cha mishahara wanacholipwa kikilinganishwa na cha wenzao.

Jambo la kuelewa ni kwamba kiuchumi si jambo la ajabu kuona wafanyakazi wenye elimu za ngazi sawa kutoka sekta tofauti wakipishana viwango vya mishahara. Kwa kutumia kipimo kiitwacho ‘wage to production ratio’ unaweza kuamua nani umlipe nini kutokana na uzalishaji wake sambamba na vigezo vingine kifedha, kisera na kimkakati.

Ni kweli kwamba kipimo hicho nilichokitaja kinafanya kazi kirahisi katika sekta ya uzalishaji bidhaa. Lakini kinasumbua sana kinapotumika kwenye sekta ya huduma kama ambayo wapo walimu (intangible products). Ndiyo maana binafsi napata shida kujiridhisha kuhusu huu utamaduni wa kuwalipa wasomi wa ngazi zinazofanana kutoka sekta tofauti, ikiwa unazingatia vipimo vya uzalishaji kiuchumi, kisera, kimkakati na kimazingira.

Kupitia machozi yao sasa walimu wanataka kuongezewa mishahara kwa asilimia 100. Wanataka posho ya kufundishia mazingira magumu, wanataka ruzuku ya makazi pamoja na madai mengine ambayo kwa hakika kama yakitimizwa na Serikali kwa asilimia 100, basi walimu watakuwa ‘wameula’ kama tunavyosema vijana wa kizazi kipya!

Walimu wetu wamekomaa, wanataka kumwagiwa mapesa, wanataka maisha mazuri.  Mengine yote huko juu (ikiwamo kuonewa, kupuuzwa na kutothaminiwa kama wanavyosema wenyewe) naweza kuwaachia wanasiasa wajimwage nayo; lakini hili la hitaji lao la kumiminiwa fedha; walau sitaacha lipite pasipo kulitazama kwa jicho la kiuchumi.

Kinachowasukuma walimu kudai nyongeza maradufu ya pesa ni mambo makubwa mawili ambayo kiukweli ni sababu za msingi mno. Kwanza, ni mwendokasi wa kupanda kwa gharama za maisha (cost of living), mkabala na mfumuko kichaa wa bei (crazy inflation). Kwa kawaida suluhisho la matatizo haya mawili linaonekana ni mtu kuwa na pesa nyingi mfukoni. Ukurasa wa uchumi na kanuni za kifedha (kwa jamii na kwa mtu mmoja mmoja) vinatuambia nini kuhusu hili?

Kabla sijashuka kifedha na kiuchumi zaidi ninatambua kuwa mgogoro wa walimu (pamoja na wafanyakazi wengine) unakuwa na hamasa yenye kusukumwa na hisia za kisiasa kiasi ambacho tunapishana na uhalisia. Ndiyo maana utasikia walimu wakisema, “Viongozi wananunua na kutembelea mashangingi halafu sisi hawataki kutuongezea mishahara.”

Utawasikia wengine wakisema; “Kama wao wakiumwa wanakwenda kutibiwa India, basi na sisi watupe Green Card”, na utawasikia raia wakilalamika “Viongozi wanaachia madini yanakwenda kwa wageni, wanaendekeza ufisadi halafu hawajengi barabara wala kutuletea umeme.”

Orodha ya madai kama haya ambayo ni ya msingi kabisa inaendelea na kuendelea. Hata hivyo, inahitajika busara kubwa kuyatafsiri makosa, uzembe, bahati mbaya au uchelewaji wa Serikali kutekeleza matakwa ya walimu. Unaweza kupata mtaji wa kisiasa, lakini ukavuruga fikra za wananchi kiuchumi kwa miaka 50 ijayo!

Moja ya mambo yanayochangia mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha, ni kuwapo kwa ujazo wa fedha unaozidi kiwango cha uzalishaji wa huduma na bidhaa katika uchumi na mzunguko wa fedha. Ukimimina pesa kwenye mzunguko (ndani ya muda mfupi), kwa hesabu unakuwa umegusa mboni ya shetani aitwaye mfumuko wa bei ‘inflation’. Kazi kubwa ya shetani huyu ni kutafuna thamani ya fedha.

Shetani huyu ana pacha wake mwingine aitwaye ukosefu wa ajira. Mashetani hawa wawili hawaivi chungu kimoja, ukimdhibiti mmoja mwingine anainuka. Ukimimina fedha mtaani unaongeza ajira, lakini unapandisha mfumuko wa bei; ukidhibiti mfumuko wa bei unapunguza ajira mitaani.

Wachumi wa Serikali kwa sasa wana kazi ya ziada kwa sababu watu wanataka kuona ajira zikimiminika mitaani na mfumuko wa bei ukitoweka. Ni kweli kwamba inawezekana kabisa kuweka msawazo; kwa maana ajira ziendelee kuongezeka na wakati huo huo ukidhibiti mfumuko wa bei katika viwango fulani. Lakini jambo hili ni rahisi kulitamka ama kulifikiria (theoretical assumptions) ukilinganisha na utekelezaji wake.

Pengine kuna haja tujikumbushe namna dunia ilivyojikuta imeanza kutumia fedha. Watu wa kale walianza kwa biashara za kubadilishana bidhaa kwa bidhaa (barter trade). Baadaye kutokana na ugumu wa kubeba bidhaa kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili ya kubadilishana, vikaanza kutumika vito vya thamani kama vibadilishio (media for exchange).

Katika hatua hii ndipo kulitokea benki za kitamaduni (traditional banks) na hatimaye tawala (serikali) zikaja kuchukua jukumu la kusimamia mbadilishano. Serikali hizi zikaanza kuchapisha hati/vibali vinavyoonesha mkulima ‘B’ anamiliki magunia kumi ya mahindi yaliyopo eneo fulani. Kwa kutumia hati/kibali kile mkulima angeweza kwenda kwa mfugaji wa ng’ombe akampa ile hati/kibali na yeye kupewa ng’ombe wenye thamani sawa na magunia 10 ya mahindi.

Hizi hati/vibali ndizo zinazoitwa fedha kwa sasa. Ina maana kuwa serikali inatakiwa kuchapisha, kutoa na kulipa fedha zinazolingana na thamani ya bidhaa zilizopo kwenye uchumi. Ndiyo maana serikali huwa inakopa fedha kutoka nje licha ya kuwa inao uwezo na mamlaka wa kuchapisha fedha.

Kiuchumi mtu halipwi mshahara kwa kuangalia mahitaji yake, isipokuwa hulipwa mshahara kutokana na anachozalisha (direct and indirect contribution). Kwa mantiki hii ninaona niwakopeshe walimu wazo hili, ‘badala ya kulilia nyongeza ya mshahara kwa vigezo vya kupanda kwa gharama za maisha zinazowakabili, waishawishi serikali kuhusu thamani ya mchango wao kwenye uchumi (nominal value) na si (assumptive value)’.

Hili naona ni la muhimu kwa sababu hivi sasa watu tunathamini fedha kuliko bidhaa au huduma. Tunathamini fedha kuliko tija tunayozalisha. Ujinga huu ndiyo unaosababisha mtu awe na furaha anapopewa fedha asiyoifanyia kazi stahiki. Kumpa mkulima hati (fedha) inayoonyesha kuwa anamiliki magunia 10 ya mahindi wakati hakulima ni kumdanganya mfugaji ambaye atampa ng’ombe mkulima huyu hewa.

Kinadharia serikali inao uwezo wa kutekeleza matakwa ya walimu kwa kutumia mbinu mbalimbali za muda mfupi au za muda mrefu. Kwa kutumia njia za muda mfupi, serikali inaweza kukopa au kuchapisha noti nyingi zaidi (anti-heterodox programmes) na kuwalipa walimu na hata madaktari ambao wamewasha moto.  Njia ya muda mrefu ni kuboresha makusanyo ya kodi, kudhibiti mfumuko wa bei, kuboresha miundombinu ya kiuchumi na hatimaye kuongeza mishahara inayoendana na tija. (Government strategic spending with backed nominal value).

Kama serikali ikiamua kutuliza shari na kuamua kuwaridhisha walimu kwa asilimia 100, mitaa yetu itafurika pesa, tutakuwa na neema kwa muda mfupi. Lakini machozi wanayolia walimu kwa sasa, baadaye yataanza kutiririka machoni mwetu wananchi wote. Ni pale tutakapojikuta tuna fedha zisizoweza kununua, maana hata sasa shida hiyo inakua!

Natambua walimu na madaktari wana mbinu za majadiliano, ambako huanza na madai mengi na makubwa wakitarajia serikali kufika mwafaka wa wastani. Lakini tusisahau kuwa fedha zinatakiwa kuendana na tija inayozalishwa kiuhalisia na si kihisia au kisiasa!

Je, serikali itafuta machozi ya walimu kwa kumimina fedha? Tusubiri!

[email protected] 0719 127 901


By Jamhuri