Nini kifanyike kuhusu timu za hapa nchini? Pengine ndilo linaweza kuwa swali kwa wadau wa soka. Mashindano ya SportPesa yalimalizika juzi huku tukishuhudia klabu kutoka nchi jirani zikichuana kwenye fainali.

Katika mashindano hayo ambayo Yanga ilitolewa mapema tu na Kariobangi Sharks ya Kenya, hali hiyo imedhihirisha kwamba klabu za Tanzania hazijajipanga vizuri.

Mashindano hayo yalihusisha timu zinazodhaminiwa na SportPesa. Wadhamini hawa wameanzisha kombe linaloitwa ‘SportPesa Cup’, ambalo huzikutanisha timu zote zinazodhaminiwa na SportPesa kutoka Kenya na Tanzania.

Katika michuano hiyo timu za Tanzania za Simba, Singida United, Yanga na Mbao zimeshindwa kufanya vizuri mwaka huu dhidi ya timu za Kenya. Miaka miwili iliyopita timu ya Gor Mahia ilitwaa kombe hilo mara mbili mfululizo na kupata nafasi ya kucheza na timu ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Uingereza.

Mwaka juzi fainali ya jumla ya michuano hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Watanzania wakibaki kuwa watazamaji wa mechi baina ya Gor Mahia dhidi ya Everton.

Mwaka jana michuano ya SportPesa ilifanyika nchini Kenya na timu ya Gor Mahia ilifanikiwa kutwaa tena kombe hilo la Sport Pesa na kupata tena fursa ya kucheza na timu ya Everton nchini Uingereza ili kumpata bingwa wa jumla wa michuano hiyo.

Kikubwa zaidi, katika michuano ya mwaka huu 2019, Watanzania walikuwa na matarajio makubwa kwamba  klabu za Yanga na Simba zingeweza kutwaaa taji hilo, lakini haikuwa hivyo. Singida United ndiyo ilikuwa timu ya kwanza ya Tanzania kuyaaga mashindano hayo baada ya kutolewa na timu ya Bandari FC kwa kufungwa 1-0.

Yanga nayo ikatolewa na Kariobangi Sharks kwa jumla ya magoli 2-3, lakini matumaini ya Watanzania yakahamia kwa timu ya Simba, baada ya timu hiyo kushinda mechi dhidi ya AFC Leopards ya Kenya kwa jumla ya magoli 2-1.

Timu ya Mbao ilirejesha matumaini makubwa kwa Watanzania baada ya kumtoa bingwa mtetezi, Gor Mahia kwa njia ya matuta, hivyo kufanikiwa kutinga nusu fainali.

Mechi iliyofuata ya Simba dhidi ya Bandari FC kutoka Mombasa, Simba ikafungwa magoli 2-1, kadhalika Mbao nao wakayaaga mashindano kwa kutolewa kwa mikwaju ya penalti na Kariobangi Sharks.

Kauli ya Rais mstaafu, mzee Ali Hassan Mwinyi, kwamba kwenye michezo Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu bado inaendelea kusimama, kwani licha ya michuano hii kufanyika katika ardhi ya Tanzania, bado wageni wameondoka na kombe.

Mwaka 1998, timu ya Yanga SC ilifanikiwa kuingia katika hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika, hata hivyo haikufuzu kucheza hatua iliyofuata. Lakini bado unaweza kujiuliza, kwanini mzee Mwinyi alisema Tanzania kwenye michezo ni kichwa cha mwenda wazimu?

Mbali na Yanga, Simba SC mwaka 2003 pia ilifanikiwa kuingia hatua ya makundi kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika baada ya kuitoa timu ya Zamalek ya nchini Misri na kuishia hatua ya makundi. Swali ni bado Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu?

Hata kwa upande wa klabu za Yanga na Simba wakitoa historia yao ya mafanikio ndani ya nchi, utakesha kuwasikiliza, unahitaji hata siku tatu kufahamu zaidi kuhusu mafanikio yao, lakini kwenye ngazi ya kimataifa hawana historia yoyote ya mafanikio, labda katika michuano ya Kombe la Kagame.

By Jamhuri