Mchezaji wa zamani wa Mbeya City, Eliud Ambokile (pichani), wiki iliyopita alisafiri kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kujiunga na timu ya Black Leopards inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo kwa mkopo wa miezi mitatu.

Katika maisha ya soka Ambokile amepiga hatua kubwa, amefanikiwa kupata nafasi ya kucheza kwenye ligi bora licha ya kuwa na umri mdogo.

 

Usajili wa Ambokile umewaduwaza wadau wengi wa soka nchini, kwani kuna wakati kuna tetesi zilienea zilizodai kuwa  mchezaji huyo amekosa wakala wa kumsimamia katika usajili wake, vilevile tetesi za awali zilidai amepata timu katika Ligi Kuu ya Misri.

Imekuwa nadra kwa wachezaji wa Kitanzania kutoka kwenye klabu ndogo kama Mbeya City au Ruvu Shooting kusajiliwa na timu zinazocheza ligi kubwa barani Afrika. Wachezaji wengi husajiliwa kutoka klabu za Yanga, Simba au Azam.

Baadhi ya wachezaji waliopata bahati ya kucheza katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini ni Mrisho Ngasa, aliyetokea Yanga, Uhuru Seleman aliyetokea Simba, ambaye hivi sasa anachezea timu ya Biashara United na Abdi Banda ambaye hadi sasa anachezea timu ya Baroka. Ambokile amepata ‘zari’ ukimlinganisha na wachezaji wengine.

 

Ambokile ameiacha timu yake ikiwa inashika nafasi ya 12 katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL), huku akiifungia jumla ya magoli tisa  – timu nzima ikiwa imefunga jumla ya magoli 24. Ambokile ndiye alikuwa injini ya timu kutokana na kuhusika  kwa zaidi ya asilimia 44 ya ushindi katika timu yake. Hivyo, nafasi nzuri ambayo Mbeya City waliopo hivi sasa katika msimamo wa ligi imechagizwa na Ambokile kwa kiasi kikubwa.

 Ligi Kuu ya Afrika Kusini ni miongoni mwa ligi kuu tano bora barani Afrika, hivyo kama atajituma itamsaidia kusajiliwa moja kwa moja na timu hiyo.

Katika msimamo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini, timu yake mpya ya Black Leopards inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi hiyo inayojumuisha timu 16 katika ligi hiyo, baada ya kujikusanyia jumla ya alama 20, huku Bidvest Wits ikishika usukani wa ligi hiyo baada ya kujikusanyia alama 34.

 

Hali hiyo inaifanya  Black Leopards kuwa moja ya timu ambazo ziko katika hatari ya kushuka daraja, hivyo Ambukile ana kazi kubwa kuhakikisha timu yake hiyo mpya inabaki katika ligi kuu.

Bila kumng’unya maneno, Ambokile atakabiliwa na ushindani mkali wa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kwani mshambuliaji mwenzake katika timu ya Leopards, Mzambia, Mwape Musonda, ndiye kinara wa kufunga magoli katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, hadi sasa ametikisa nyavu mara nane.

 

Vilevile akionyesha makali yake kama yale aliyoonyesha kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, anaweza kupata nafasi ya kusajiliwa na klabu kubwa za Afrika Kusini kama Mamelodi Sundowns, Kaizer Chiefs, Orlando Pirates na hata kupata nafasi ya kwenda kucheza Ulaya kama ilivyo kwa Mbwana Samata.

Ambokile hatakuwa mgeni katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, kwani ataungana na beki kisiki, Abdi Banda, anayeichezea timu ya Baroka.

Wakati huohuo, timu ya Mbeya City ina kazi kubwa ya kuhakikisha inapata matokeo mazuri, hivyo Kocha Nswazirimo Ramadhan na benchi lake la ufundi hawana budi kuhakikisha wanaziba pengo la Ambokile baada ya kumruhusu akacheze katika timu ya Black Leopards, kwani nafasi waliyonayo katika ligi ilitokana na mchango mkubwa wa Ambokile.

Please follow and like us:
Pin Share