JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

Baadhi ya wataalamu wa uchumi walitabiri kuwa huenda thamani ya sarafu ya Afrika Kusini ikaathirika kwa kiasi kikubwa baada ya kiongozi wake wa zamani, Jacob Zuma, kujisalimisha polisi na kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 gerezani.

Mara nyingi uchumi wa nchi hufungamanishwa na viongozi wake wakuu, wanasiasa wenye nguvu, wafanyabiashara wakubwa na kampuni kubwa. 

Kwa Jacob Zuma na uchumi wa Afrika Kusini alikuwa anafananishwa na aliyewahi kuwa rais wa Marekani, Donald Trump na uchumi wa n chi hiyo.

Aghalabu, mambo aliyoyafanya au kuyasema Trump yaliakisi kwenye uchumi wa nchi lakini hali haikuwa hivyo Afrika Kusini baada ya Zuma kuingia jela.

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita thamani ya sarafu ya nchi hiyo, Rand, haikuonekana kuathirika sana kwenye masoko kutokana na kufungwa kwa Zuma kama ilivyokuwa imedhaniwa.

Hali ya sasa ni tofauti na Desemba 2015 wakati Zuma alipokuwa madarakani na kumfukuza kazi aliyekuwa Waziri wa Fedha, Nhlanhla Nene, usiku wa manane.

Hatua hiyo ilisababisha thamani ya Rand kushuka na kufikia kiwango cha chini kuwahi kutokea cha Rand 16 kwa dola moja ya Marekani.

Kwa ujumla wake, hatua hiyo ya rais Zuma wakati huo ilisababisha hasara ya Rand bilioni 5 kwa nchi kwa mujibu wa makadirio yaliyokuwa yametolewa na hazina ya nchi hiyo.

Hali hiyo ilidhibitiwa baada ya Zuma kulazimishwa kumteua Pravin Gordhan kama Waziri wa Fedha. 

Miaka miwili baadaye mwaka 2017, wakati Zuma alipopoteza uongozi ndani ya Chama cha ANC kwa Cyril Ramaphosa, Rand ikaanza kupanda tena na kufikia kiwango cha juu katika kipindi cha miaka minne.

Utafiti uliofanywa na IMF unaonyesha kuwa tangu kutokea kwa tukio la askari kuwaua wachimbaji madini huko Marikana (2012), Rand imekuwa ikiathiriwa sana na matukio yanayotokea ndani ya nchi hiyo.

Hivyo, ilidhaniwa kuwa kufungwa kwa Zuma kunaweza kusababisha sarafu hiyo kushuka thamani lakini hali haijawa hivyo.

Usiku wa Jumatano iliyopita dakika 15 baada ya saa sita usiku wakati Wakfu wa Zuma ulipotangaza hadharani kuwa kiongozi huyo ameamua kujisalimisha na kuanza kutumikia kifungo chake, sarafu ya Rand haikuonekana kuathirika.

Sarafu hiyo ilianza siku ikiwa na thamani ya Rand 14.36 kwa dola ya Marekani. 

Siku ilipomalizika thamani ya Rand ilikuwa ni 14.32 kwa dola.

By Jamhuri