KIJANA WA MAARIFA (9)

Jifunze zaidi uongeze uzalishaji

Katika chuo kimoja cha kujifunza karate lilitolewa tangazo la vijana waliopenda kujiunga na kozi ya karate wafanye usajili na kuanza kozi hiyo katika mwaka mpya wa masomo.

Wolfgang akiwa kijana aliyehitimu masomo ya uzamili alikuwa ni mmojawapo wa vijana walioguswa na tangazo hilo. Hivyo alikwenda kujisajili.

Mafunzo yakaanza huku jumla ya wanafunzi wakiwa watano na Wolfgang akiwemo. Vijana wale wengine wanne walikuwa hawajawahi kuona hata chembe ya masomo ya sekondari inafananaje. Kimsingi kiwango chao cha elimu kilikuwa darasa la saba.

Wolfgang baada ya kugundua wale wenzake wote wameishia darasa la saba, alianza kuwadharau na kuona kwamba kozi hiyo kwake itakuwa rahisi sana.

Walianza na kujifunza vitu vidogo, kimojawapo kikiwa kufanya usafi wa mazingira. Wolfgang hakuona kama hiyo ni kazi ya kiwango chake, hivyo yeye hakuhusika katika mambo yanayohusu usafi. Wale wenzake wakaendelea kama kawaida.

Hakujali kuhusu kuwahi darasani, daima yeye alikuwa mtu wa mwisho kuingia darasani. Mwaka wa kwanza wa masomo yao ukaisha. Masta (Mkuu wa mafunzo) akataja wanafunzi wanaopaswa kupanda darasa. Orodha iliyotajwa ilikuwa na wanafunzi wanne. Jambo la kushangaza kijana Wolfgang hakuwa katika orodha hiyo.

Jambo hilo lilimuuzunisha sana, kwani alijiona yeye ni wa viwango vya juu, inakuwaje sasa anakosa kupanda darasa? Hakuishia hapo, ikabidi amfuate masta  ili kuuliza kulikoni.

Alipofika katika chumba cha masta na kuuliza kwa nini hakupanda darasa. Masta alichukua kikombe cha chai na kumkabidhi. Wolfgang alipokea kikombe kile, kisha masta akaanza kumimina chai katika kikombe alichoshikilia Wolfgang.

Masta akamimina chai mpaka chai ikaanza kumwagika, huku Wolfgang akiwa anashangaa tukio lile. Masta aliendelea kumimina chai. Mara ghafla akahamaki akisema: “Masta! Huoni kikombe kimejaa na chai inamwagika?”

Masta akaacha kumimina chai. Kisha akasema: “Sasa umepata funzo, wewe na kikombe kilichojaa hamkuwa na tofauti, haukutaka kamwe kumimina kikombe chako, muda wote tulipokufundisha tayari kikombe chako kilikutwa kimejaa, hivyo haukujifunza lolote.”

Mpendwa msomaji, maisha ya Wolfgang yanatisha sana, ni mtu anayejiona amejua kila kitu hataki kujifunza kitu kipya. Hiyo ni hatari sana. Ukitaka kuboresha zaidi maisha yako lazima ukubali kujifunza, lazima kikombe chako kiwe kitupu ili uingize chai mpya, ukiacha kikombe kijae bila kukimimina utaishia kuwa na maisha kama ya Wolfgang.

Wahenga walisema: “Elimu ni bahari.” Elimu haina mwisho. “Shule ni kitu kimoja, elimu ni kitu kingine,” alisema Austin Kleon.

Ukitaka kuongeza uzalishaji katika nyanja au sekta yoyote sharti uongeze elimu yako.

Elimu si lazima uende shuleni ukajifunze kukariri na kujibu mitihani (kama mifumo mingi ya shule ilivyo). Elimu inapatikana kila mahali siku hizi. “Haijalishi upo shuleni au haupo, ni kazi yako muda wote kupata elimu,” ni maneno ya mwandishi Austin Kleon.

Akitambua umuhimu wa elimu, naye RZA anasema: “Sikujali nilikwenda shuleni au sikwenda, muda wote nilisoma.”

Kuna faida nyingi za kujifunza mara kwa mara. Ukijifunza unaongeza ufahamu, unaongeza maarifa. Unajua lipi linafanya kazi na lipi halifanyi kazi. Mambo yaliyoonekana magumu sasa yanakuwa mepesi.

Siku hizi unaweza kujifunza kwa urahisi kuliko ilivyokuwa zamani. Unaweza kujifunza kupitia intaneti, hapa ndipo dunia imefunguka.

Siku hizi kuna vyuo vikubwa duniani vinatoa kozi mbalimbali bure kwa njia ya mtandao, kozi hizo ukiwa tayari kujifunza zinaweza kukufikisha mbali.

Mtandao kama www.Udemy.com unafundisha mambo mengi mazuri yanayoendana na dunia ya sasa kwa gharama ndogo tu. Ama kweli elimu sasa ni rahisi kuipata lakini ni wachache wanatumia fursa hiyo.

Tume ya Sensa ya Marekani pamoja na Taasisi ya Elimu ya Marekani waliwahi kufanya uchunguzi kuhusiana na kuongezeka kwa elimu sambamba na kiwango cha uzalishaji, majibu yafuatayo yalipatikana:

Kwanza, ukiongeza elimu ya mtu kwa asilimia 10 unaongeza uzalishaji wake kwa asilimia 8.7; pili, ukiongeza muda wa kufanya kazi wa mtu kwa asilimia 10 unaongeza uzalishaji wa mtu huyo kwa asilimia 6; na tatu, ukiwekeza katika mtaji watu kwa asilimia 10 uzalishaji unaongezeka kwa asilimia 3.2.

Ukitaka kuongeza uzalishaji, jifunze, jifunze, jifunze.

Kuna aliyewahi kusema: “Usiache kujifunza, kwa sababu maisha hayajawahi kuacha kufundisha.”