Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaingia katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu kikiwa tayari kimekwisha kujihakikishia ushindi kwa asilimia 70 katika ngazi zote zitakazogombewa.

“Kutokana na jinsi tulivyojipanga, hadi hivi sasa tuna uhakika wa asilimia 70 ya kura za urais na asilimia 70 ya viti bungeni,” anasema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.

Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalumu, Polepole anasema kwa jinsi chama hicho kilivyojipanga kina uhakika wa kuendelea kushinda chaguzi zote zitakazofuata katika miaka 90 ijayo hadi mwaka 2100.

Akifafanua, Polepole anasema ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana ni ishara ya kile kitakachotokea baadaye mwaka huu kwenye Uchaguzi Mkuu.

Katika uchaguzi huo CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 90 baada ya vyama vingine vya siasa kujiondoa kwa madai ya kutofuatwa kwa taratibu, jambo lililosababisha zaidi ya asilimia 90 ya wagombea kutoka vyama vya upinzani kukatwa majina yao, hivyo kushindwa kugombea.

“Lakini ushindi wetu utatokana na mambo makubwa mawili. Kwanza, ni kazi ambayo tayari CCM imeshazifanya kuwaletea wananchi maendeleo. Kuwaletea wananchi huduma za kijamii karibu kama vile maji, elimu, afya na miundombinu,” anasema Polepole.

Anaitaja sababu ya pili ya chama hicho kushinda Uchaguzi Mkuu ujao kuwa ni oganaizesheni nzuri ya chama ambayo inakifanya chama hicho kifanye kazi si tu kama taasisi, bali taasisi iliyo karibu zaidi na wananchi.

Polepole anajigamba kuwa ushindi wa CCM kwa sasa wanautazama kwa kizazi, hivyo mpaka sasa CCM imekwisha kushinda, na zaidi wanajipanga kuongoza kwa vizazi vitatu, yaani  kuanzia 2025 hadi 2050, 2050 hadi 2075 na kizazi cha tatu 2075 hadi 2100.

“Watu wanaweza kuhoji kama Polepole atakuwapo? Sijui kama nitakuwapo au nitakuwa mbinguni lakini itakuwapo mipango tunayaoipanga sasa hivi,” anasema.

Anasema mipango inaendelea ya kuifanya CCM kuwa chama cha kidijitali na hadi hivi sasa kutokana na utafiti wa kisayansi uliofanyika ndani ya chama, wamejihakikishia kuwa wana wanachama kama milioni 15 nchi nzima.

Anasema idadi ya wapiga kura nchi nzima inatarajiwa kuwa kama milioni 22, na iwapo Wana CCM hao milioni 15 watajitokeza kupiga kura, basi chama hicho tayari kina mtaji wa asilimia 70.

Maendeleo ya watu

Anawabeza wanaosema Serikali ya Awamu ya Tano inafanya maendeleo ya vitu badala ya kuendeleza watu, kwa kusema kwamba hawaelewi wanachokiongea.

 “Fikiria mgonjwa anatolewa Sengerema anapelekwa Bugando, kwa kutumia kivuko cha Kamanga kuja mjini Mwanza unatumia saa mbili. Lakini serikali ya John Magufuli na Chama Cha Mapinduzi wameelekeza lijengwe daraja lenye kilometa tatu kati ya Kigongo – Busisi na kuvuka Ziwa Victoria zitakuwa dakika nne, hapo unajua ni maisha ya watu wangapi yatakuwa yameokolewa?” anahoji Polepole.

Anasema malengo makuu ya CCM ni kushinda uchaguzi na kushika dola, na lengo muhimu zaidi ni kuwatumikia Watanzania kwa uaminifu na kuwaletea maendeleo.

Anasisitiza kuwa CCM itawafikisha Watanzania katika dira ya taifa inayotakiwa ambapo kutakuwepo na maendeleo kwa watu wote.

Anasema Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusogeza fursa wezeshi kwa wananchi kunaipa CCM nafasi ya kushinda kwa urahisi katika uchaguzi huo.

Anasema serikali inayoongozwa na CCM imewezesha kusogezwa karibu miundombinu kama barabara, umeme, uchumi shirikishi na jumuishi, maji na afya.

“Haya mambo yote yanamhakikishia fursa wezeshi Mtanzania kwamba kufanikiwa kwake kutakuwa ndani ya uwezo wake,” anasema.

Anasema dhamira ya CCM ni kuwezesha kutoa uongozi kwa Watanzania, hivyo kwa mwaka 2020 kikatiba ni mwaka wa uchaguzi, hivyo CCM imejiandaa kikamilifu kushiriki uchaguzi huo.

Halikadhalika, anasema wanaendelea kufuatilia ratiba ya serikali itakayotolewa na Tume ya Uchaguzi na wamejipanga vizuri kushiriki.

Anasema mtaji wa ushindi wa kwanza walionao ni kazi zote zilizofanywa na Rais John Magufuli ndani ya miaka minne zitakazowafanya Watanzania kutopata taabu kuielewa CCM.

“Watanzania wanapenda twende nao na sisi tumejipanga kama chama kutowaangusha. Sifa lukuki tunazopata kwa Watanzania tutazitumia kama chachu ya kufanya mambo mazuri zaidi tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, tutakapochagua rais, wabunge na madiwani,” anasema.

Anasema jambo jingine litakaloisaidia CCM kushinda uchaguzi ujao ni mageuzi makubwa yanayofanyika ndani ya chama kila baada ya miaka kumi.

Anasema mageuzi hayo yenye lengo la kukifanya chama kujitazama, kujitathmini na kuweka uongozi mwingine imara, utakifanya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao.

Anaongeza kuwa mwaka 2017 walifanya mabadiliko ya kimuundo ndani ya chama ambayo yamekipa nguvu na uimara na kukifanya kuwa karibu na wananchi huku akisema kuwa kimekuwa chama kilicho karibu na watu.

Polepole anasema mabadiliko hayo makubwa waliyoyafanya yameongeza nidhamu ndani ya chama na kukifanya kuwa imara.

“Katika hili la mageuzi ya chama kwa kweli kupitia uongozi wa chama na Ndugu John Joseph Magufuli na Katibu Mkuu wetu, Ndugu Bashiru Ally, tumehakikisha kwamba nidhamu ya chama wakati wote inakuwa imara, hasa nidhamu ya chama kwa viongozi,” anasema Polepole na kuongeza kuwa viongozi mara nyingi walikuwa wakileta vurugu kinapofika kipindi cha uchaguzi lakini anaahidi kuwa katika kipindi hiki hakutakuwa na msamaha kwa mtu yeyote atakayevunja misingi ya nidhamu ya chama hicho.

Kutokana na mabadiliko ya kimuundo, anasema CCM kwa sasa ina wanachama zaidi ya milioni 15, idadi anayosema ni mtaji mkubwa utakaoiwezesha kushinda kwa urahisi.

Anasema CCM sasa hivi haihesabu nyumba ili kubaini wanachama wake kama ilivyokuwa zamani, bali kwa sasa baada ya kufanya mabadiliko inahesabu mtu mmoja mmoja.

Anaongeza kuwa mtaji mwingine utakaoifanya CCM kushinda ni kuwa chama taasisi, tofauti na vyama vingine.

Anasema muundo wake unaifanya CCM kujiendesha kwa mujibu wa katiba na kuzingatia matakwa ya sheria ya vyama vya siasa.

“Sisi tuna vikao ngazi ya taifa, tuna oganaizesheni ya chama na utendaji ngazi ya taifa, ngazi ya mkoa, wilaya, kata, kule Zanzibar tuna ngazi ya jimbo, wadi halafu ngazi ya tawi.

“Pale kwenye tawi ndiyo karibu kabisa na wananchi, pale tuna taasisi kamili, kuna katibu pale anayefanya shughuli za utendaji za chama, tuna mtu anafanya shughuli za uenezi wa chama. Tuna mwenyekiti, tuna kamati ya uongozi na siasa, tuna kikao kikuu cha uongozi, tuna halmashauri kuu ya tawi, huo wote ni mtaji wa kutufanya tushinde,” anasema.

Aidha, anasema muundo huo umeenea nchi nzima, na kwamba wanayo matawi yanayofikia 30,000 nchi nzima, ambapo kuna matawi yenye zaidi ya wanachama 1,000.

Anaongeza pia kwamba chama kimeingizwa kwenye mfumo wa kidijitali ambavyo kadi za chama hicho zinaweza kusomeka katika mifumo yoyote kielektroniki.

Anasema wametengeneza ‘Smart card’ zinazoweza kusomeka hata kwenye mfumo wa mashime za ATM, lengo la kufanya hivyo akisema kuwa ni kuwaleta karibu wanachama wao ili waweze kusomana.

“Hivi sasa mifumo yetu inatuwezesha kuwaona wanachama wote nchi nzima,” anajigamba.

Anasema kwa kuwa CCM inathamini utafiti wa kisayansi, ushindi huo ni bayana kutoka na mambo makubwa ambayo serikali imefanya mijini hadi vijijini.

“Ukiwauliza wananchi wanataka nini, watakwambia tunataka amani na mshikamano, hapa tumetoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kwamba suala la amani si jambo la kulifanyia mzaha.

“Watu wanataka kuona huduma za kijamii zinawafikia kwa urahisi, hapa imefanyika kazi kubwa, tumeleta maji, tunatoa elimu bure.

“Katika eneo la afya, kazi kubwa imefanyika, tangu Uhuru mpaka mwaka 2015 tulikuwa na vituo vya afya 115 tu.  Tangu ameingia Rais Magufuli mpaka mwaka 2017 ameweza kujenga vituo vya afya 500 nchi nzima, hizi ni hospitali ndogo za wilaya, kwa sababu huduma zote za afya zinapatikana hapo,” anasema.

Akizungumzia malalamiko ya vyama pinzani kufanyiwa hujuma kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, anasema nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na desturi nzuri, hivyo malalamiko yao yanakosa msingi.

Anasema nchi haiongozwi kwa matamko ya barabarani, uchaguzi wa serikali za mitaa ni uchaguzi uliosimamiwa na sheria ya uchaguzi na kanuni zake, huku akibainisha kwamba wapinzani hawakuzingatia taratibu hizo.

Anasema kabla ya uchaguzi kufanyika vyama vyote vilikubaliana juu ya miongozo hiyo na kuweka sahihi za kukubaliana na miongozo hiyo.

Hata hivyo, anavitaka vyama vya upinzani kuelewa kuwa uchaguzi una sehemu tatu; yaani kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Anasema vyama vya upinzani vilijipanga wakati wa uchaguzi pasipokujua kuna mipango kabla, wakati na baada ya uchaguzi, hali iliyosababisha baadhi kususia uchaguzi huo.

“Wapinzani waliingia wakati wa uchaguzi, lakini hawakujua kwamba ushindi wa uchaguzi ni mikakati inayofanyika kabla ya uchaguzi.

“Sisi tuliwekeza elimu kubwa kwa wanachama waliopitishwa kugombea kwa tiketi ya CCM, tulipeleka mawakili 1,200 kwenda kutoa elimu ya namna ya kujaza fomu, fomu zilijazwa vizuri bila ya kosa hata moja,” anasema.

Anaongeza kuwa uchaguzi ni mchakato, huku akikituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupanga njama za kuvuruga uchaguzi huo kwa kuondoa wagombea wake siku mbili kabla ya uchaguzi badala ya kukata rufaa.

By Jamhuri