Watu wengi huwa wananiuliza swali hili mara kwa mara, “Je, kila mtu ni lazima awe mjasiriamali?”

Nimekuwa nikiwajibu na leo ninataka kulijibu kwa namna nyingine na kwa upana. Ili kulijibu swali hili ninaomba nitumie Biblia kupata baadhi za rejea.

Ingawa hapa nitatumia Biblia, ninatambua kuwa vitabu vyote vitakatifu vimeeleza kuwa Mungu alimuumba kila mwanadamu ili aishi kwa mafanikio duniani.

Katika Biblia tunaambiwa kuwa Mungu alipowaumba wanadamu aliwapa agizo hili, “…….zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale….”. [Mwanzo 1: 27-30]. Baada ya hapo akawapa mbegu za mimea mbalimbali ili wafanye kazi ya kupanda na kupata mazao, matunda na mboga kwa ajili ya chakula. Pia akawapa ruhusa ya kutumia wanyama kwa ajili ya kupata nyama kama chakula.

Watu wengi wanaposoma agizo hilo la Mungu kwa wanadamu huwa wanadhani Mungu alimaanisha kwenda kuzaliana watoto pekee. Lakini ukisoma sura yote ya agizo hilo utabaini kuwa agizo lilikuwa ni zaidi ya kuzaliana watoto na lilikuwa ni agizo la ujasiriamali.

Tuliopita kwenye madarasa ya uchumi na biashara tunafahamu kuwa unaposema biashara ama ujasiriamali wa kibiashara unakuwa ukiongelea maeneo yafuatayo; ubunifu na uzalishaji, kuongeza unachozalisha, kusambaza unachozalisha (masoko), kusimamia haki ya ubunifu wako (kutiisha) na utawala wa rasilimali zote zinazokuwezesha kuzalisha na unazozalisha.(kutawala)

Hii ina maana kama ni kuzaa watoto, Adamu na mkewe walitakiwa kuzaa watoto, watoto nao wakaongezeke, wanaoongezeka wakajae duniani pote. Lakini hawa wanaojaa duniani pote ni lazima wasimamiwe vema na waongozwe kikamilifu.

Kama ni kupanda na kuvuna mazao mbalimbali, walitakiwa kupanda mbegu hizo na baadaye wazisambaze mahali pengi na kule zinakosambaa waweze kuzifuatilia na kuzisimamia (kutawala).

Kwa picha nyingine ni kuwa Mungu alikusudia mwanadamu kutumia kidogo alichompa kwa ajili ya kuzalisha vingi, kuvisambaza na kuvisimamia. Ndiyo maana Mungu hakumpa mwanadamu mahindi bali alimpa mbegu za mahindi. Ndiyo maana hakumpa miti bali alimpa mbegu za miti. Ndiyo maana hakumpa watoto bali alimpa uwezo wa kuzaa watoto.

Yaani ni kwamba Mungu alimtaka mwanadamu kutumia rasilimali na mazingira aliyoyaumba kwa ajili ya kutengeneza na kuzalisha mambo ambayo yatamsaidia katika kupata chakula na kupata maendeleo. Kutumia vichache na kuzalisha vingi huo ndiyo ujasiriamali. Kuikuta hali katika uduni na kuiboresha huo ndiyo ujasiriamali.

Kwa hiyo, utagundua kuwa alichokiumba Mungu na kumkabidhi mwanadamu ulikuwa ni ujasiriamali. Kwa lugha nyepesi tunasema Mungu alimuumba kila mwanadamu (nasisitiza kila mwanadamu) kuwa mjasiriamali.

Mungu alitambua kabisa kuwa ujasiriamali unafanikishwa na vitu vifuatavyo; mtazamo, fikra na uamuzi vilivyomo ndani ya kasha liitwalo utashi. Ndiyo maana katika pumzi aliyompulizia mwanadamu iliambatana na utashi. Kwa kutumia utashi Mungu alijua kwamba kwa kumpa Adamu mbegu ya maharage, angejua kuwa mbegu hiyo inatakiwa kupandwa ardhini na kabla ya kupandwa ardhi ni lazima ilimwe.

Kwa kutumia utashi, Mungu alitambua kuwa mwanadamu angejua ni nini cha kufanya ili watoto watokee na wazidi kuongezeka. Utashi waliopewa binadamu wa kwanza ndiyo tulionao leo — utashi wa ujasiriamali.

Kinachotusumbua watu wengi ni kuwa hatujaamua kufungua utashi wetu ili kutumia mtazamo, fikra na uamuzi, utakaotufanya tuishi kwa makusudi kamili ya kuumbwa kwetu — yaani kuwa wajasiriamali.

Kwa mujibu wa agizo la Mungu utabaini kuwa ujasiriamali ni kitu kinachopaswa kumsaidia kila mtu kupata chakula na kuwa na maendeleo. Kwa sura pana ni kwamba popote anapokuwapo mwanadamu ni lazima atumie ujasiriamali kwa ajili ya kuboresha maisha yake.

Ipo shida moja kubwa ya kwamba kila unapotajwa ujasiriamali wengi huwa wanapeleka mawazo katika suala la kujiajiri ama la kujiongezea kipato. Ni kweli kuwa hayo ni sehemu ya ujasiriamali, lakini siyo maana pekee ya ujasiriamali. Ndiyo maana wachambuzi wa ujasiriamali huwa tunatenganisha dhana hii katika makundi mawili — wajasiriamali wa kibiashara (wajasiri-wa-mali) na wajasiriamali wa kikazi (wajasiri-wa-kazi).

Makundi yote haya pamoja na wale ambao hawana kazi yoyote waliumbwa kutumia ujasiriamali kwa ajili ya kupata chakula na maendeleo.

Kumbuka kuwa ujasiriamali (kwa mtazamo wa Mungu) ni kutumia aina yoyote ya rasilimali, mazingira na utashi wako kwa ajili ya kupata chakula na maendeleo (ya kwako na ya wanaokuzunguka). Mathalani; mfanyakazi aliyeajiriwa anaweza kufanya ujasiriamali kwa namna mbili: Mosi, ni ule wa kujiongezea kipato nje ya ajira yake na pili ni kuboresha na kuongeza maendeleo zaidi ya yale anayochangia kwa taasisi ama kampuni yake.

Mfanyakazi anapokuwa mbunifu na kuibuka na mapendekezo mapya kuhusu uboreshaji wa bidhaa ama huduma za kampuni ama taasisi anayofanyia kazi, huo ni ujasiriamali (ujasiriakazi). Mfanyakazi anapojitolea zaidi katika kazi za kampuni yake pasipo kutanguliza malipo, huo ni ujasiriamali (ujasiriakazi). Pia mfanyakazi anapoanza kuweka kidogo kidogo sehemu ya mshahara wake na hatimaye kuanzisha biashara ama mradi wa kumuongezea kipato, huo ni ujasiriamali.

Tunachoona hapa ni kuwa kila mtu ni mjasiriamali na anatakiwa kuishi kiujasiriamali.

Hadi hapa bila shaka unapata picha! Picha yenyewe ni hii: “Kwa kuweka utashi wa kijasiriamali kwa mwanadamu, Mungu alikusudia mwanadamu asife kwa kukosa chakula, na asiishi duniani pasipo maendeleo kwa namna na katika mazingira yoyote yale”.

Kwa kulijua hili, tuna makundi mawili ya kuyatazama —  walioajiriwa lakini wanalia kwa mishahara isiyotosha na wale ambao wanalia kwa ukosefu wa ajira. Ukiwasikiliza watu wote wa makundi haya mawili utasikia kilio chao wakilia hivi; “Tunakufa kwa maisha magumu!”

Tatizo kubwa si ukosefu wa ajira kama ambavyo waliokosa ajira wanavyoweza kulia na kulalamika. Tatizo kubwa si udogo wa mishahara kama ambavyo wenye mishahara kidogo wanaweza kulalamika. Tatizo lipo katika kushindwa kufungua utashi wa kijasiriamali tuliopewa na Mungu.

Lazima tuelewe kuwa Mungu alipomuumba mwanadamu hakukuwapo na kitu kiitwacho “waajiri” na wala hakukuwapo na kitu kiitwacho “mishahara”. Kila mtu alitakiwa kutumia rasilimali zinazomzunguka kwa ajili ya kupata chakula na maendeleo.

Ni kweli kwamba dunia ilibadilika na mambo mengi yakatokea na hivyo kuzalisha waajiri na waajiriwa, lakini ukweli ni kwamba tangu kuumbwa kwa dunia, licha ya kupitia vipindi na mikasa mingi, mwanadamu hajawahi kunyang’anywa utashi wake.

Ndani ya utashi kuna mtazamo, kuna fikra na kuna uamuzi. Uamuzi sahihi huja kwa fikra sahihi na fikra sahihi zinaletwa na mtazamo sahihi. Mtazamo unaanza kwa kuamini. Ni lazima uamini kuwa upo duniani kufanikiwa, ni lazima uamini kuwa mafanikio yako hayashikwi na mwajiri wako, hayashikwi na serikali yako.

Mungu alipomuumba mwanadamu hakukuwapo na serikali, hivyo ni lazima uwe na mtazamo kuwa hata bila serikali unaweza kufanikiwa! Mungu anapomuumba mwanadamu hakukuwapo na waajiri, hivyo ni lazima uamini kuwa hata pasipo mwajiri ama hata kwa huo mshahara mdogo bado unaweza kufanikiwa!

Kwa nini uamini hivyo? Ni kwa sababu wewe ni mjasiriamali! Wewe ni mjasiriamali kwa namna gani? Ni mjasiriamali kwa sababu una utashi uliobeba mtazamo, fikra na uamuzi unaoweza kukusaidia kutumia vichache kuzalisha vingi, kutumia mazingira duni kupata mazingira bora, kugeuza changamoto kuwa fursa na kuchukua visivyodhaniwa na kuvifanya vya kutumainiwa!

Umekosa ajira? Unadhani kuwa kwa kukosa ajira utakufa? Huwezi kufa hata kidogo. Nakwambia huwezi kufa kwa sababu wewe ni mjasiriamali. Unaweza kuniambia, “Sanga mimi sina hobby na ujasiriamali na wala sifikirii kuwa mjasiriamali.” Ni sawa! Lakini ninakuuliza swali; “Upo tayari kufa kwa sababu ya kukosa ajira? Je, upo tayari kuishi maisha duni na ya kimaskini kwa sababu eti unalipwa mshahara kidogo?”

Ninachokueleza ni hiki, badilisha mtazamo wako kuhusu ajira kwa sababu maisha yako hayapo katika ajira pekee. Hebu kichwani kwako anza kuingiza fikra mpya kwa sababu fikra za kudhani kuwa mshahara utakufanyia kila kitu zinakupotezea muda na zitakuongezea ufukara tu. Kwa wakati huu hebu fanya uamuzi na ujisemee ‘sitakufa kwa sababu ya kukosa ajira, sitakuwa maskini kwa sababu ya mshahara wangu kuwa kiduchu.’ Unaweza na inawezekana kwa sababu wewe ni mjasiriamali haswa!

Mpaka hapa tumeshaona kuwa kila mtu anatakiwa kuwa mjasiriamali. Kila binadamu anazo zana (mawazo, fikra, uamuzi) zinazoweza kumsaidia kutumia fursa na mazingira yanayomzunguka kwa ajili ya kupata chakula na maendeleo yake. Hapa hakuna kusubiri kinachoitwa kuwezeshwa kwa sababu mbegu tunazo na tunatakiwa kuingia kazini.

Kama Mungu hajakusudia ufe eti kwa sababu umekosa ajira, unasubiri nini kuanza kujishughulisha ili uendelee kuishi. Kama Mungu hajakusudia ufe kwa sababu eti unapata mshahara kidogo, kwa nini usianze leo kutumia hicho kidogo katika kuzalisha vingi? Inawezekana!

Sanga ninasema, “Wanadamu wote tunastahili ushindi wa kijasiriamali”,

stepwiseexpert@gmail.com +255 719 127 901

1867 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!