Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, kati ya mambo anayohusishwa nayo ni msemo maarufu kwamba: “…kila zama na kitabu chake.”

Bila shaka msemo huu kutoka kwa mzee Mwinyi unalenga kutufanya tuwe makini ili tusichanganye mambo yanayofanyika kwa sasa na yaliyofanyika wakati mwingine hapa nchini, ni msemo unaotufanya tuondoe shaka na hali ya kujiuliza ni kwa nini hili linafanyika wakati huu na si wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu au Awamu ya Nne?

Ni kwamba, inawezekana yanayofanyika leo yako sahihi kulingana na wakati uliopo, hali kadhalika yaliyofanyika wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza yalikuwa sahihi kulingana na wakati huo, sidhani kama yanapingana, maana kila zama na kitabu chake.

Nakumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuulizwa na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jinsi alivyokuwa akiiona na kuichukulia Katiba ya Tanzania. Sijui kama muulizaji alikuwa amemtega kwa swali hilo, Mwalimu Nyerere alimjibu mtangazaji huyo kwamba kwa namna katiba ya nchi yetu ilivyokuwa ni kama ilikuwa ikimshawishi kuwa dikteta.

Alisema kwamba ilikuwa ikimrundikia mamlaka makubwa mno, kiasi kwamba viongozi wengine wengi wakuu wa aina yake enzi hizo madaraka hayo yaliwaelemea na kujikuta wanaangukia kwenye udikteta. Mwalimu alitoa maelezo kwa uzito uliostahili juu ya Katiba na kueleweka vizuri.

Mfano, alisema kwamba nchi changa ambazo kwanza ndiyo zilikuwa zinajitawala zina wasomi wachache sana, hivyo zilihitaji katiba za aina hiyo (katiba inayompa nguvu zaidi kiongozi mkuu), vinginevyo mambo yangekwama na kuziendesha nchi hizo lingekuwa jambo tata.

Yapo mambo mengi yanayoweza kutazamwa kwa muktadha huo na kuonekana kweli kwamba kila zama na kitabu chake.

Mfano, mwaka 1973 Kamati Kuu ya TANU, chama tawala wakati huo, ilitoa tamko kwamba makao makuu ya nchi yahamie Dodoma. Lakini mpaka mwaka 1999, wakati anafariki dunia Baba wa Taifa, miaka takriban 26 baada ya tamko hilo, hazikuwepo dalili zozote za kufanikisha jambo hilo.

Tulipoingia tu Awamu ya Tano, moja ya mambo ya kwanza ni pamoja na hilo, kuhamisha makao makuu ya nchi kutoka Dar es Salaam  hadi Dodoma. Tena ikumbukwe kwamba, Rais Dk. John Magufuli anapotamka jambo mara nyingi hupendelea kulishadidia kwa nukuu za Baba wa Taifa katika kuonyesha jinsi lilivyo na umuhimu wa pekee.

Lakini sijamuona Rais Magufuli akihoji kwa nini Baba wa Taifa alishindwa kuyahamishia makao makuu ya Serikali mjini Dodoma? Bila shaka, kwa mtazamo wangu, ni kwa sababu kila zama na kitabu chake.

Yapo mambo mengi yanayofanyika kwa wakati huu na kubaki yakishangaza ni kwa nini hayakuwezekana muda wote wa awamu zilizopita? Kwa mfano, tumeona ndege zikinunuliwa kwa muda mfupi na nyingine kubwa katika mazingira ambayo hayakuwahi kufikiriwa kwamba kama zingeweza kununuliwa. Tumeona barabara za ghorofa zikiendelea kujengwa jijini Dar es Salaam, yote hayo yamewezekana wakati huu wa Awamu ya Tano.

Tunaweza kujiuliza, kwa nini haya hayakufanikiwa wakati mwingine na yamefanikiwa wakati huu? Na jinsi tunavyomuelewa alivyokuwa mzee wa Kizanaki (Mwalimu Nyerere), ni kwa sababu kila zama na kitabu chake.

Tutakuwa hatuitendei haki historia ya nchi yetu kwa kujivunia tu yanayofanyika kwa wakati huu, hivyo kujipa ushawishi wa kuyabeza yaliyofanyika nyuma tukiona kwamba hakuna cha maana kilichofanyika wakati huo.

Iwapo tunao uzalendo wa kweli kwa nchi yetu, tunapaswa kuelewa kuwa lengo letu hasa ni kuiboresha zaidi nchi yetu, kila wakati tufikirie kuiboresha, si kwa ajili yetu tuliopo wakati huu, bali hata kwa ajili ya vizazi vijavyo. Na katika kufanya hivyo litakuwa si jambo jema kuboresha jambo moja halafu tukae na kuanza kujilaumu ni kwa nini hatukuliboresha jana.

Kwa namna hiyo tutakuwa tumezidiwa na wanyama ambao sijaelewa kwa lugha ya Kiswahili wanaitwaje lakini kwa lugha ya Kihaya wanaitwa ‘endimi’ na ‘emparangwa’.

‘Endimi’ ni wanyama ambao usiku kucha huwa wanachimba mashimo makubwa ambayo hutumiwa baadaye na ‘emparangwa’ kama makazi yao. ‘Endimi’ wanachimba mashimo tu lakini hawalali, wanaofaidi mashimo hayo ni ‘emparangwa’.

Ndiyo maana Wahaya wakasema kwamba “endimi elima emperangwa etaha,” wakiwa na maana kwamba huyo mnyama aitwaye ‘endimi’ kazi yake ni kuchimba tu mashimo ambayo anayenufaika ni ‘emparangwa’.

Kwa hiyo wanyama hao wangeanza kazi ya kujiuliza ni kwa nini jana haikuwa kama leo, wakiwa na maana ya kwa nini mashimo hayo hayakuchimbwa jana, sijui ni kwa wakati gani hayo mashimo yangechimbwa na hao wanaoyafaidi wangeyatumia wakati gani kupata njozi.

Tukirudi kwenye hekima za mzee Mwinyi, ni kweli kwamba kila zama na kitabu chake. Hii yote ni katika kutafuta kuboresha, na kuboresha hakuna mipaka. Kwa hiyo tujiepushe na swali la “kwa nini leo na si jana?”

Yanayofanyika leo wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ni uboreshaji wa nchi yetu ambao ulipaswa ufanywe na vizazi vilivyopita, vilivyopo na hata vijavyo kwa manufaa ya nchi yetu, kama kweli upo uzalendo unaohitajika. Ndiyo maana ukajitokeza usemi wa wahenga kwamba: “Roma haikujengwa kwa siku moja” – (Rome was not built in a day).

[email protected]

0654 031 701 / 0784 989 512

By Jamhuri