Kilichomponza tajiri Zakaria

Mfanyabiashara Peter Zakaria (58), amerejesha mali zote alizonunua kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU), akiamini kwa kufanya hivyo ataondoa ‘nuksi’ ya kuandamwa na Serikali. Tajiri huyo mkazi wa Tarime mkoani Mara, anayemiliki vitegauchumi mbalimbali yakiwamo mabasi ya Zakaria, amekabidhi nyaraka za umiliki wa mali hizo serikalini, wiki iliyopita. Zakaria anashikiliwa rumande akituhumiwa kuwajeruhi kwa risasi maofisa usalama wawili waliomfuata kwenye ofisi zake usiku, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni ‘kumteka’ na kumpeleka kusikojulikana. Kwa miezi saba sasa, mkewe yuko mahabusu akishitakiwa kwa uhujumu uchumi kutokana na kuwa kwenye nyaraka za ununuzi wa mali za Chama cha Ushirika Nyanza. Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Adam Malima, amethibitisha kuwa waliojeruhiwa kwenye tukio hilo la Juni 29, mwaka huu ni maofisa wa Usalama wa Taifa. Chanzo cha habari kutoka ndani ya familia ya Zakaria kimesema wanaamini misukosuko mingi inayoiandama familia hiyo, inasababishwa na mambo kadhaa,
moja likiwa hilo la ununuzi wa mali za NCU. Mke wa Zakaria, Anthonio Zakaria, amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi akihusishwa na ununuzi wa mali za chama hicho cha ushirika. Tangu alipokamatwa mwaka jana, ameendelea kuwa rumande. Msemaji wa ukoo wa Zakaria, Samuel Chomete (65), amethibitisha urejeshaji wa nyaraka na mali zote za NCU ambazo zinamilikiwa na familia ya Zakaria. Chomete ameliambia JAMHURI mjini Tarime kwamba mali hizo zimerejeshwa rasmi serikalini kuanzia Julai 3, mwaka huu. Hata hivyo, hakueleza makabidhiano hayo yamewahusisha viongozi gani wa Serikali au NCU. Mali zinazotajwa ni nyumba ya NCU ambayo kwa sasa kuna Benki ya CBA (Commercial Bank of Africa), na kituo cha mafuta cha Zakaria kinachotazamana na Jengo la Kitegauchumi la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Barabara ya Kenyatta jijini Mwanza. Familia ya Zakaria inasema ilinunua mali hizo kihalali mwaka 2002. Kurejeshwa kwake kunatokana na msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuhakikisha wale wote walioshiriki ‘kufilisi’ ushirika maeneo mbalimbali nchini wanashitakiwa. Chomete amekataa kutaja kiasi cha fedha kilichotumika kununua mali za ushirika huo. Uamuzi wa familia na
ukoo wa Zakaria unalenga kulinda usalama wa mfanyabiashara huyo na familia yake. “Tumeonana na yeye Zakaria, ameshauri mali hizo zirudishwe, asije akafa bure. Na mama mkurugenzi (Anthonio) amesaini nyaraka za makabidhiano Jumanne (iliyopita). “Vyote tumerudisha serikalini ili vikabidhiwe Nyanza Co-operative Union,” Chomete ameliambia JAMHURI. Anthonio Zakaria, ambaye ndiye anayeonekana kwenye nyaraka za ununuzi tangu Januari, mwaka huu, amezuiwa katika Gereza la Butimba jijini Mwanza, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. Meneja wa NCU, Juma Mokili, ameulizwa kama ameshapokea mali za chama hicho kutoka kwa familia ya Zakaria, na amesema hawajakabidhiwa. Licha ya kukiri kuwa familia hiyo inamiliki mali zinazotajwa, amesema asingependa kuingia kwenye undani wa suala hilo kwa kuwa lipo mahakamani. Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, mahali ambako kuna mali hizo, Marry Tesha, ameulizwa na kujibu kuwa kazi ya urejeshaji mali hizo inasimamiwa na mkoa. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amezungumza na JAMHURI na kuomba apewe muda ili apate ukweli juu ya kurejeshwa kwa mali hizo.
“Hiyo taarifa ndiyo naisikia kwako… Ngoja nifuatilie Jumatatu au Jumanne (jana au leo) nitakuwa na jibu,” amesema Mongella.
UPEKUZI NYUMBANI KWA ZAKARIA Julai 5, 2018 Polisi walimchukua Zakaria kutoka Musoma na kwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake Tarime. Magari kadhaa, yakiwamo mawili yaliyojaa polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wenye silaha, yalifika kwenye makazi ya mfanyabiashara huyo na kufanya upekuzi. Mamia ya wananchi walikaribia eneo la tukio. Katika upekuzi huo unaodaiwa kuwa na baraka za Mahakama, inaarifiwa kuwa bunduki mbili aina ya shotgun na rifle pamoja na vibali vya umiliki vilichukuliwa na polisi. Baadaye walirejea Musoma. Wananchi kadhaa mjini Tarime bado wanajadili tukio la kuvamiwa Zakaria. Mwananchi mmoja, Heche Chacha, amehoji, “Kama kweli hawa watu walikuwa na nia njema ilikuwaje wabandike namba kwenye gari lao (T 245 CTW) wakati siyo yao? “Yawezekana pengine hawa watu walitaka kumchonganisha Zakaria na Ndesi Mbusiro, anayemiliki gari lenye namba hiyo T 245 CTW,” amesema Heche ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara.

Zakaria mahakamani Julai 5, mwaka huu Zakaria alifikishwa mahakamani mjini Musoma akikabiliwa na mashitaka ya kujaribu kuua. Alikanusha tuhuma hizo. Katika kesi hiyo Na. 3/2018 iliyopo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara, mfanyabiashara huyo anatetewa na mawakili wawili – Onyango Otieno na Kassim Gilla. Upande wa mashitaka yupo Wakili Lukelo Samuel. Wakili Samuel amedai kuwa mshitakiwa anakabiliwa na makosa mawili ya kujaribu kuua. “Mshitakiwa alitenda kosa hilo Juni 29, 2018 katika Mtaa wa Anglikana wilayani Tarime. Ametenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha Sheria cha Kanuni ya Adhabu, Sura Na 16 Kifungu cha 211 (a) kilichofanyiwa marejeo mwaka 2006,” amedai Wakili huyo wa Serikali. Inadaiwa kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo kwa watu wawili waliotajwa kwa majina ya Ahmad Segure na Isack Bwire. Wakili huyo wa Serikali hakutaja kazi zao wala mahali wanapoishi. Alisema majeruhi hao wanatibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam. Akaiomba Mahakama kutompa dhamana mtuhumiwa huyo, akidai hiyo ni kwa ajili ya usalama wa mshitakiwa na pia hali za kiafya za majeruhi si nzuri. Wakili Gilla akaiomba Mahakama impatie mteja wake dhamana kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika kisheria. “Vifungu vya Sheria Na 148 Kifungu kidogo cha 5 (a) Na ( i-v) pamoja na Kifungu cha Sheria Na 148 Kifungu cha 6-7, vinaainisha juu ya uwepo wa
dhamana. “Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 13 (6) inazungumzia suala zima la upatikanaji wa dhamana kwa mtuhumiwa,” alisema Wakili Gilla. Akadai kwamba upande wa Serikali umeshindwa kutoa nyaraka zinaoonesha kuwa majeruhi wapo hospitalini wakitibiwa. Pia hakuna kiapo cha daktari kinachothibitisha
yote hayo. “Mwanasheria wa Serikali ameshindwa kutoa pia ushahidi unaothibitisha moja kwa moja kuwa kuna viashiria vya kuhatarisha maisha ya Zakaria, iwapo atapatiwa dhamana.” Akijibu hoja hizo, Mwanasheria wa Serikali, Samuel, alidai kuwa wanajua kuwa mshitakiwa ana haki ya kupewa dhamana, lakini Jamhuri imeona kuna
haja ya kuzuia dhamana, kwani kesi hiyo haijaanza kusikilizwa. Kutokana na majibizano hayo ya kisheria, Hakimu Mfawidhi wa Mkoa, Hashim Mushi, akasema: “Nimesikiliza hoja za pande zote mbili na nimeona nikae nizipitie kwanza, ili kujiridhisha. Hivyo, naahirisha kesi hii hadi tarehe 10/7/2018, Mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu dhamana kwa mshitakiwa.”