Mchezo wa rushwa aliounusa Rais John Magufuli katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ukabila, ukanda na usiri wenye lengo la kunufaisha watu binafsi na jamaa zao, vimetajwa kumsukuma Mkurugenzi Mkuu mpya wa Takukuru, Diwani Athumani, kufumua mtandao alioukuta, JAMHURI limebaini.

“Katika harakati za kuboresha utendaji wa Takukuru, kufumua mtandao wa ukabila, kuwadhibiti wakubwa waliopenyeza ‘vijana’ wao ndani ya Takukuru na kuondoa wingu la usiri, Takukuru imeamua kuzaliwa upya,” amesema mtoa habari.

“Kwa ninavyoona, Diwani Athumani anataka kuipa heshima Takukuru. Anataka kujenga Takukuru yenye nguvu kama kitengo cha Serious Fraud Office (SFO) cha Uingereza ambacho kinashughulikia makosa makubwa ya rushwa bila kuangalia makunyanzi.

“Kwa wanaokumbuka SFO ilivyoshughulikia rushwa ya rada kwa Tanzania hadi tukarejeshewa fedha zilizoitwa ‘chenji ya rada’ karibu Sh bilioni 72, waliongozwa na uwazi na uwajibikaji. Tangu alipoingia Mlowola mambo yalipiga hatua 50 nyuma.

“Mtu kufika Takukuru kutoa taarifa ilipoteza maana. Taarifa nyingi zipo kwenye simu za mkononi. Wakati wa Mlowola mtu aliyefika mlangoni aliambiwa acha simu, na kila kitu uende na nguo zako tu, SFO Uingereza wanaruhusu hata kompyuta na mabegi yenye ushahidi kuingia nayo ofisini kwao. Hili suala naamini Diwani atalibadilisha mara moja. Utaratibu alioweka Mlowola unaishia kupata majungu na si taarifa zenye ushahidi.

“Takukuru inavyo vyumba maalumu vya kuchukulia maelezo, vyenye mitambo ya kurekodia. Kama imeharibika, basi inunuliwe mipya. Kukataa watu wasiingie na simu au vielelezo ndani ni ishara ya utovu wa uadilifu, maana watumishi wa Takukuru wanajiandaa pengine kutamka yasiyohusiana na kazi yao, hivyo wanaogopa wasirekodiwe wakiomba rushwa kwa waliofika ofisini kwao,” amesema ofisa mmoja aliyesema amefurahishwa na uamuzi wa kuhamisha watu waliokuwa wamejigeuza miungu – watu.

Fagio hilo ndani ya Takukuru limekuja miezi mitatu tangu kuteuliwa kwa Mkurugenzi Mkuu mpya, Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani, ambaye wakati anaapishwa alikabidhiwa jukumu la kufanya mabadiliko ya kimuundo ndani ya taasisi hiyo.

Mabadiliko makubwa aliyoyafanya Diwani Athumani ni pamoja na kuwaondoa wakurugenzi watatu kati ya watano.

Walioondolewa ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Alex Mfungo, ambaye kwa mujibu wa taarifa ambazo Gazeti la JAMHURI limezipata, amehamishiwa Wizara ya Kilimo na kupangiwa majukumu mengine huko.

Mwingine ni Mbengwa Kasomambuto ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi, huyo taarifa zinaonyesha kwamba atapangiwa kazi nyingine, lakini taarifa kutoka ndani ya Takukuru zinasema kigogo huyo anasubiri kupangiwa majukumu mengine ya juu katika ngazi ya mkoa.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Ekwabi Mujungu, naye ameondolewa, huku taarifa kutoka ndani ya taasisi hiyo ya Upanga, zinaonyesha kwamba naye anaangukia katika mkumbo kama wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi.

Kati ya viongozi watano waliokuwa wanaunda Menejimenti ya Takukuru, waliobaki ni Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini, Kulthum Mansour, pamoja na Mkurugenzi wa Utafiti, Sabina Seja.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, amesema ni kweli watumishi hao wamehamishwa huku akiwataja baadhi ya watumishi na nyadhifa zao.

“Baadhi ya watumishi hao ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Alex Mfungo; Mkurugenzi wa Upelelezi, Mbengwa Kasomambuto na Ekwabi Mujungu aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma,” anasema Kapwani.

Anasema uhamisho huo ni wa kawaida. Kapwani ameeleza kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa Takukuru kuhamisha watumishi wengi kwa wakati mmoja.

“Yawezekana kwa Takukuru ikawa ni mara ya kwanza kuhamishwa kwa idadi kubwa, lakini kama mnavyofahamu, sisi kama watumishi wa umma hatulazimiki kufanya kazi katika taasisi moja tu.

“Tunapenda kusisitiza kuwa uhamisho huu ni wa kawaida kama ambavyo mmekuwa mkisikia unafanyika katika wizara au idara nyingine za serikali.

“Yawezekana kwa Takukuru ikawa ni mara ya kwanza kuhamishwa kwa idadi kubwa, lakini kama mnavyofahamu, sisi kama watumishi wa umma hatulazimiki kufanya kazi katika taasisi moja tu,” anasema Kapwani.

Kapwani anasema uhamisho uliofanyika ni wa watumishi 40 ambao umehusisha ngazi ya wakurugenzi, wakaguzi wa kanda, wakuu wa Takukuru wa mikoa pamoja na wakuu wa vitengo na Makao Makuu.

Walioshika nafasi za wakurugenzi waliohamishwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Utumishi na Rasilimali Watu, Ayoub Akida na Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi, Kassium Ephrem.

JAMHURI limepata orodha ya watumishi waliohamishwa Takukuru ambao ni Ekwabi Mujungu, Mbengwa Kasomambuto, Resticks Ndowo, Ernest Barulo, Oliver Linje, J. Semiti, Geofrey Urasa, Joyce Shundi, Yohana Madadi na Alexander Budigila.

Wengine ni Peter Billa, Nakembetwa, Masiko, Eunice Mmari, Musa Misalaba, Mhyela, Steven Mbele, Makale, Sechuma, Mazome, Mogasa, Ndomba, Mkono, Mpyambale, Oscar Hosea, Danieta Tindamanyire, Emile Mwasyoge, Grace Kwangu na Beatha Peter.

Wafanyakazi wengine ni Abubakar Msangi, Mshumbusi, Grace Benjamin, Mariam Mwendamseke, R. Kitundu, Mary Kidima, Juventus Baitu, Ismail Othman, Ally Mnyani, Mwarabu na Ndibaiukao.

Rais John Magufuli alipokuwa anamwapisha Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athuman, alimtaka kuungalia upya muundo wa Takukuru ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

Jambo jingine ni kuhakikisha watendaji wa taasisi hiyo wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija na kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani.

“Nataka ukaisafishe Takukuru, kuna baadhi ya wafanyakazi wa Takukuru wanajihusisha na rushwa, kawaondoe. Nataka kuona Takukuru inashughulikia rushwa kwelikweli, hasa rushwa kubwakubwa, ukipita huko vijijini wananchi wanateseka sana, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi sana, na tatizo kubwa ni rushwa,” alisisitiza Rais Magufuli.

Pia alimtaka Kamishna Diwani kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa nchini na kuhakikisha wanaokabiliwa na tuhuma za kujihusisha na rushwa wanafikishwa mahakamani.

Septemba mwaka jana, Athuman aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera (RAS), kabla ya kuteuliwa kuwa bosi wa Takukuru, alisema anakwenda kuyafanyia kazi aliyoelekezwa na rais.

Diwani aliyechukua nafasi ya Valentino Mlowola ambaye ameteuliwa kuwa Balozi, alisema rais amempa maagizo ambayo lazima yatekelezwe.

Alisema kama alivyoambiwa na Rais Magufuli kuwa ndani ya Takukuru kuna kazi kubwa imefanyika, yeye ataangazia mifumo na utendaji wa taasisi hiyo.

“Na ukiona hivyo, unajua kuna watu wamewezesha kufanyika na hasa mtangulizi wangu (Mlowola) amefanya kazi kubwa sana sana na mimi nakwenda kuboresha,” alisema.

Diwani, ambaye kabla ya kwenda kuwa RAS Kagera alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), alisema anakwenda kutekeleza yale aliyoagizwa kwa kushirikiana na wenzake.

“Silaha yangu kubwa itakuwa ni kufanya kazi kama timu moja. Kama ni kufanikiwa tufanikiwe wote na kama ni kufeli tufeli wote.

“Hizi dhamana tunazopewa lazima tujitahidi tusije kujutia, ukaja kuulizwa ulipewa nafasi kubwa ulifanyaje?” alisema.

By Jamhuri