Juhudi za Rais John Magufuli kudhibiti magendo katika biashara ya korosho, maarufu kama ‘kangomba’ zinaelekea kuingia doa kutokana na watendaji aliowaamini katika ngazi ya wilaya kushiriki biashara hiyo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Taarifa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi zinaonyesha kuwa baada ya watendaji wa serikali kuwadhibiti wafanyabiashara waliokuwa wananunua kangomba, wao sasa wamebaki na uwanja mpana wa kutengeneza ‘hela ndefu’.

“Labda kwa kuwa mmeingia ninyi JAMHURI mtasaidia. Hali imebadilika kutoka kuwa mbaya, sasa ni mahututi. Kwa sasa hao wanaosikika wamekamatwa kwa kangomba ni mashati tu, wahusika wenye mashati ni watumishi wa umma.

“Hivi tunavyozungumza watumishi wa umma ambao ni wakuu wa wilaya, ma-DAS, OCD, DTO ndio wamegeuka wafanyabiashara wakubwa wanaonunua kangomba. Baada ya kuona hivyo, hata watumishi wa umma wengine kama walimu na manesi nao wananunua kangomba kwa sasa.

“Mhe. Rais kazi anayo kweli kweli. Wanachofanya sasa ni kuwahiana kuandikiana ripoti chafu. Unakuta OCD kimya kimya anamtuhumu DC, naye DC anapeleka taarifa kwa waliomteua zinazowatuhumu wasaidizi wake, korosho haiiachi nchi hii salama,” amesema ofisa aliyeomba atambulishwe kama ‘Mzalendo wa Tanzania’ kwa kuepusha kufuatiliwa na wakubwa.

Mwingine amesema: “Viongozi, hasa katika ngazi ya wilaya wanamfanyia mchezo Rais Magufuli. Hivi inawezekanaje kwamba mtu anakuja anasema ana kilo za korosho tani 80? Kwa vipimo vya kawaida tani 80 anapaswa kuwa na shamba la ekari 100. Mtu huyu unakuta hana hata ekari 3.

“Pale Mtwara kuna mtu ana tani 500. Huyu ina maana anapaswa kuwa na shamba lenye ekari 600. Viongozi wa wilaya wanapambana alipwe. Unaweza kudhani analipwa yeye, kumbe ni ‘kisawe’ chao. Yule ametangulizwa tu, wenye mzigo ni wakubwa wapo wanakula ‘unyunyu’.”

Watoa taarifa wamesema magari binafsi ya viongozi akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera, yameonekana usiku katika maeneo yanayouza korosho kwa njia ya magendo huku OCD Niko na DTO wa Tunduru, Lilanga, wakituhumiwa kuwa wanawatanguliza askari wadogo kuwanunulia kangomba na kuagiza maovu mengi dhidi ya wananchi.

Kangomba ni ununuzi wa korosho kwa njia ya ulanguzi baada ya wakulima wa korosho kulaghaiwa kuuza zao hilo kabla ya soko au kumkopa mlanguzi pesa kwa lengo la kutatua tatizo kwa wakati ambapo huuza kwa bei ya chini. Mfano wakati sokoni kilo moja inauzwa Sh 3,300, walanguzi huinunua kwa Sh 1,500 au 2,000.

Wilayani Tunduru, Ruvuma, Rashid Chinyang’anyi, mkazi wa Kata ya Mindu, wilayani humo ameliambia JAMHURI kuwa tangu mwaka 2017 amekuwa akitumiwa na askari polisi kununua korosho. Mwaka jana alitumiwa tena kununua korosho kilo 350. Kilo 150 amezinunua kwa Sh 1,500 kwa kilo na kilo 200 alipaswa kuzinuna kwa Sh 2,000 kwa kilo.

Askari Polisi wa Kituo cha Nakapanya, Tunduru, PC Mtaki, alimkabidhi Chinyang’anyi Sh 625,000 mwaka jana akimtaka amnunulie korosho kwa kiwango hicho kilichotajwa hapo juu. Chinyang’anyi alinunua na kumkabidhi PC Mtaki kilo 178, ila akawa hajakabidhi kilo 172 zenye thamani ya Sh 344,000.

Chinyang’anyi amesema PC Mtaki wa Kituo cha Polisi Nakapanya amemweleza kuwa korosho hizo ni za bosi wake mjini Tunduru, ingawa hakumtaja jina na kwamba ameamua kuliweka wazi jambo hilo baada ya kutofautiana na PC Mtaki.

Chinyang’anyi alichelewa kupata korosho za kangomba na PC Mtaki akadhani ‘amemrusha’ hivyo akaenda nyumbani kwake usiku, akaingia ndani na kupekua kutafuta kitu cha thamani kufidia kiasi cha Sh 344,000 cha korosho zilizosalia.

PC Mtaki aliamua kumnyang’anya Chinyang’anyi pikipiki aina ya SanLG yenye namba za usajili T 692 CRV (hawajabadili usajili kwenda MC) na kumtaka atoe fedha zake ndipo ampatie pikipiki hiyo.

Mtendaji wa Kata ya Mindu, wilayani Tunduru, Omary Laddah, ameliambia JAMHURI kuwa baada ya gazeti hili kuanza kufuatilia suala hilo, PC Mtaki ameirejesha pikipiki kwa Chinyang’anyi ‘akilia’ Ijumaa iliyopita akiogopa kuwa sasa anafukuzwa kazi iwapo habari hizi zitachapishwa naye akakutwa na pikipiki hiyo.

Mohamed Mchanguni, mkazi wa Kijiji cha Msinji, Tunduru, amesema polisi walikwenda nyumbani kwake Novemba 13, 2018 hawakumkuta mtu, ila wakavunja mlango, wakaingia ndani na kuchukua korosho zake kilo 204 na pikipiki moja wakati yeye akiwa katika lindo la korosho shambani kwake.

“Nilipigiwa simu na polisi wakaniambia njoo uchukue pikipiki yako kituoni. Nilikwenda wakaniuliza kwa nini niliwakimbia? Nikawajibu si kweli, bali nilikuwa kwenye lindo la korosho shambani. Ndipo waliniambia sina kesi, nirudi nyumbani na kama nataka pikipiki yangu nitoe Sh 500,000.

“Nilipowaambia sina kiasi hicho wakaniambia nitoe chochote, hivyo nilitoa Sh 20,000 nikakabidhiwa pikipiki yangu,” amesema Mchanguni.

Amesema kilichomuuma zaidi ni kuambiwa na polisi hao kuwa korosho zake pamoja kwamba hazipo kwenye orodha ya kangomba, hawezi kuzipata hadi watakapomaliza kesi za wale wanaohusishwa na kangomba, lakini kama anazitaka haraka atoe Sh 500,000, kinyume cha hapo aziache. Ameziacha.

Raphael Matiku Makanya, mkazi wa Kijiji cha Msinji amesema alikamatwa Novemba 20, 2018 majira ya saa 11:00 alfajiri baada ya kugongewa mlango na polisi nyumbani kwake. Alifungua mlango, kisha mara tu wakamtuhumu kuwa anafanya biashara ya kangomba. Polisi hao waliingia ndani kupekua hawakukuta kitu chochote, lakini walimpeleka kituo cha polisi na kumweka mahabusu hadi siku ya pili.

Novemba 21, 2018 Makanya amesema aliambiwa yeye na wenzake hawapelekwi mahakamani kwa kuwa hakuna kielelezo walichowakuta nacho kuhusu biashara ya kangomba, lakini watoe Sh 50,000 ili kuachiwa. Kila mtuhumiwa kati ya saba alitoa kiasi hicho na kuachiwa.

Novemba 26, 2018 mchana, polisi wawili wakiwa na silaha walikwenda tena nyumbani kwa Makanya na kumkuta mtoto wake Makanya Matiku (12), wakamshurutisha afungue mlango na walipoingia ndani chumbani, walipekua hadi kwenye foronya kitandani na kuiba akiba yake ya Sh 400,000.

“Nilitoa taarifa kwa OCD, nikaambiwa suala langu litapelekwa mahakamani, lakini hadi leo naona kimya na hadi sasa hatima ya fedha zangu napigwa danadana. Kwa kweli wakubwa juu kama mnasikia kilio hiki kwa shughuli iliyopo Tunduru, polisi na sisi wakulima tunaishi kama Msumbiji, kwa sababu kama umekwisha kutoa maelezo kinachofuata ni mahakamani na kama hawataki kupeleka huko kinachofuata ni kudhulumika, hakuna kingine. Huu ni ujambazi,” amesema Makanya.

Naye Mwandishi Msaidizi wa Chama cha Msingi – Mndichana AMCOS, katika Kijiji cha Msinji, Hassan Makina, amesema wanunuzi wa kangomba ni wajanja wa mjini na si wa kijijini, huku akisema wengi wao ni vigogo wa serikali ambao wana watu wao wanaowatumia kuwanunulia korosho na hawakamatwi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Gaspar Balyomi, amesema hana mamlaka ya kuzungumzia ‘Operesheni Kangomba’ kwa kuwa iliundwa ‘task force’ ya wilaya chini ya mkuu wa wilaya na ndiye mwenye jukumu la kutoa taarifa hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera, amesema suala la kangomba ni gumu kwa sababu kuna vigogo wenzake wanadaiwa kushiriki katika biashara hiyo, jambo ambalo lilimlazimu kutumia njia tofauti, ikiwemo ya wakulima wenyewe kwenda kuuza korosho kwa wanunuzi wa kangomba kupata ushahidi wa tuhuma hizo.

Amesema anazifanyia kazi taarifa alizozipata na zitakapokamilika atatoa taarifa rasmi kwani imebainika kuna baadhi ya watu wana nia ya kukwamisha jitihada za ‘Operesheni Kangomba’, jambo ambalo hatakubali kwa lengo la kulinda masilahi mapana ya wakulima wa korosho na serikali.

Homera ameeleza kuwa ‘Operesheni Kangomba’ ambayo ilianza Oktoba, mwaka jana, ilikamata korosho zaidi ya tani 18 ambazo wanaendelea kuhakiki mashamba ya wahusika.

Amesema kuwa hadi sasa kuna kesi 13 mahakamani, na akaongeza: “Ni kweli gari langu limetumika katika operesheni. Wanachosahau hili ni gari dogo, kangomba inasafirishwa kwa malori. Kwa hiyo kutokana na upungufu wa vitendea kazi mara kadhaa nimetumia gari langu kuingia mtaani usiku na mchana kudhibiti wanunuzi wa kangomba.

“Sasa katika mazingira hayo, si wote wanaofurahia udhibiti wa aina hiyo. Watatafuta kila namna wachafue jina langu, wakiamini kuwa nikiondoka mambo yatawanyookea.”

Kuhusu viongozi wenzake katika ngazi ya wilaya kufanya biashara ya kangomba, amesema hawezi kuwasemea kwani hakai nao muda wote, ila akakiri kuwa naye amepata kusikia malalamiko dhidi ya baadhi ya viongozi yenye viashiria vya aina hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Gemini Mushy, amesema analifanyia kazi suala hilo kupata ukweli wa tuhuma hizo ambazo zinawataja askari wake kuhusika kwenye biashara ya kangomba kwa kuwakamata wasiohusika kwa lengo la kuficha uhalisia.

Amesema uchunguzi ukibaini ukweli wa tuhuma hizo hatakuwa na suluhu kwa yeyote aliyehusika kwani vitendo hivyo dhahiri vinalichafua Jeshi la Polisi.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, ameliambia JAMHURI kuwa uchunguzi wa tuhuma zilizotokana na ‘Operesheni Kangomba’ zikithibitika hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika kwani vitendo hivyo vinaweza kuikosanisha serikali na wananchi.

Amesema waliochukuliwa korosho zao kwa makosa endapo itabainika hivyo watarudishiwa au kulipwa kama zitakuwa zilipimwa, lakini korosho ambazo zilikamatwa na wenyewe hawakujitokeza, basi kwa mujibu wa sera, kanuni na sheria ya biashara ya korosho ikifika miezi sita serikali itazitaifisha na kuwa mali ya serikali.

“Mtu akithibitika alishiriki katika biashara ya kangomba bila kujali kama ni mkubwa au la, atakamatwa, kwani haipendezi wakubwa wameshiriki halafu unawakamata wadogo. Tutakamata tu, awe papa, awe nyangumi, tutamkamata tu,” amesema RC Mndeme.

Kaimu Kamanda wa PCCB Mkoa wa Ruvuma, Owen Jasso, amesema kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi yao, hata kama tuhuma hizo za vitendo vya rushwa Tunduru wakati wa ‘Operesheni Kangomba’ wakiwa nazo, hawatoi taarifa kila siku, bali kuna muda wa kutoa taarifa; hivyo wakati ukifika taarifa itatolewa.

Please follow and like us:
Pin Share