Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali hiyo imekusudia kuendelea kutoa matibabu bure kwa wakazi wote wa Unguja na Pemba.

Amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha uchumi na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato.

“Serikali inaendelea na uamuzi wake iliotoa Machi 3, 1965 wa kuwapa wananchi matibabu bure, ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Unguja na Pemba wanapata huduma za kinga na tiba kwa ajili ya kuendeleza afya na kusisitiza kuwa serikali itafanya kila iwezalo ili huduma za afya ziendelee kuwa bure,” amesema.

Dk. Shein ametoa msimamo huo mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Gombani, Pemba, Mkoa wa Kusini Pemba katika kilele cha sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Amesema Sh bilioni 688.7 zilikusanywa mwaka 2017/2018   na  taasisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB); ikilinganishwa na Sh bilioni 521.8 zilizokusanywa na taasisi hizo mwaka 2016/2017.

Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la Sh bilioni 166.9; sawa na asilimia 32. Amesema mafanikio hayo yameiwezesha serikali  kutekeleza mipango ya kuinua uchumi na kuwasogezea wananchi huduma za kijamii kwa wepesi na kwa ufanisi.

Rais Shein amesema kuwa kasi ya ukuaji uchumi huo ilikuwa  asilimia 7.7 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2016. Pato la mtu binafsi limeongezeka na kufikia Sh milioni 2.1 sawa na dola 944 za Marekani kwa mwaka 2017; ikilinganishwa na Sh milioni 1.89 (dola 868) mwaka 2016.

Amesema mfumko wa bei umeendelea kudhibitiwa katika tarakimu moja katika mwaka 2018, ambapo kasi ya mfumko huo ilifikia asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 5.6 kwa mwaka 2017.

Amesema mafanikio hayo yaamechangiwa na juhudi mbalimbali za serikali ikiwemo kuwashajiisha wazalishaji wa ndani na kuweka mazingira mazuri ya biashara katika uagizaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.

Amesema katika kipindi cha miaka 55 ya Mapinduzi, yamepatikana mafanikio makubwa mno na kuimarika kwa huduma za elimu ambapo kabla ya Mapinduzi mwaka 1964 huduma hizo zilikuwa chache na za ubaguzi.

Katika utekelezaji wa mradi wa maji wa Mkoa wa Mjini Magharibi, kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Rais Shein amesema kuwa kazi kubwa tayari imekwisha kufanyika na visima tisa vipya tayari vimekwisha kuchimbwa na 23 vya zamani vimefanyiwa matengenezo.

Amesema pampu mpya zitafungwa kwenye visima hivyo, mabomba mapya yamelazwa na ujenzi wa matanki makubwa ya maji unaendelea Saateni na Migombani Mnara wa Mbao.

Kwa upande wa huduma za umeme amesema hadi Desemba, mwaka jana serikali imezifikisha huduma za umeme katika vijiji 2,694 kati ya vijiji 3,259 vya Unguja na Pemba, ikiwa ni sawa na asilimia 83. Vijiji 55 kati ya hivyo vilipatiwa umeme mwaka jana.

Amesema kuanzia Novemba, mwaka jana utafiti mwingine wa mafuta na gesi asilia ulianza katika maeneo yenye maji madogo   Pemba na baadaye utaendelea kwa upande wa Unguja.

Kwa mujibu wa mkataba, Kampuni ya RAKGAS imeidhinishwa rasmi kufanya kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Pemba – Zanzibar.

Katika hatua za kuliimarisha Shirika la Meli la Zanzibar, amesema kuwa serikali inajenga meli mpya ya mafuta (MT Ukombozi II) ambayo ujenzi wake unafanywa na Kampuni ya Damen Shipyard ya Uholanzi. Inatarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni.

Kwa upande wa utalii, amesema sekta hiyo imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na idadi ya watalii ikiongezeka. Mwaka 2018 watalii 520,809 waliwasili Zanzibar, ikilinganishwa na watalii 433,116 mwaka juzi.

Rais Shein amewahakikishia wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza  na kuimarisha Muungano uliopo.

“Mimi na Dk. John Pombe Joseph Magufuli tutahakikisha kuwa Muungano wetu unadumu na unaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wetu wa awamu zilizotangulia ili nchi yetu iendeleea kupiga hatua kubwa zaidi na ibaki kuwa ya amani na utulivu,” amesema.

Sherehe hizo zilipambwa kwa shamrashamra mbalimbali zilizoongozwa na vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama pamoja na vikundi vya ngoma za asili.

Please follow and like us:
Pin Share