*Gesi ya 25,000/- itatosha kupikia hadi maharage miezi mitatu

*Dar es Salaam, Mtwara wanufaika, magari 50 yatumia gesi

 

Ugunduzi wa gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo trilioni 46.5 ni ukombozi wa wazi kwa uchumi wa Tanzania. Thamani halisi inayokisiwa kwa gesi hii ni karibu dola bilioni 500 za Marekani, kiwango ambacho ni mara 50 ya uchumi wa sasa. Kati ya gesi hii iliyogunduliwa Kijiji cha Msimbati, mkoani Mtwara, na maeneo mengine ya nchi, futi za ujazo trilioni 38.5 zipo katika kina kirefu cha maji na futi za ujazo trilioni 8 zipo nchi kavu. Kuna dalili za mafuta, ila hayajagunduliwa. Katika makala haya, JAMHURI imehojiana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Yona Killagane, ambaye anaeleza mambo mengi ya msingi yenye kutia matumaini kuwa sasa neema iliyokuwa ikisubiriwa hatimaye imewasili Tanzania. Endelea…

 

Killagane anasema gesi inatumika kuzalisha bidhaa nyingi kuliko inavyofikiriwa. Inatumika kuzalisha umeme, kama nishati kwenye viwanda, nishati majumbani kwa kuendesha mfumo joto (heating system), kuendesha magari na ni malighafi ya kutengenezea mbolea, plastiki, nguo kama silki, na kioo chepesi cha kuzuia mikwaruzo na michubuko kwenye kompyuta, simu na saa.

Mkurugenzi huyo anasema hata chupa za maji, ndoo na bidhaa kama vikombe na vyote vinavyotengenezwa kwa plastiki asilimia kubwa inatokana na gesi.

Anaangalia kigezo cha kuzalisha mbolea, kuwa gesi itasaidia mno kuendeleza kilimo nchini. Mashamba ya mpunga, miwa, majani ya chai, malisho ya kisasa ya mifugo, ngano, viazi, mihogo na mazao mengine yanaweza kustawi kwa kasi kubwa ikiwa tu, mbolea inayotumiwa na gesi itatumika. Uzuri wa bidhaa zinazotokana na gesi, matumizi yake ni kidogo lakini yanakuwa na matokeo makubwa.

Ukiacha uzalishaji wa bidhaa, kwa wenyeji wa Mtwara,  wanaweza kuitumia gesi kwa kupikia, kukaushia korosho, samaki, kuendesha magari na hata kuwasha mwanga kutokana na umeme utakaozalishwa.

Killagane anasema kwa Mtwara na Lindi miji hiyo imepangiliwa vyema hivyo kuna mradi wa kusambaza gesi kwa wakazi wa miji hiyo kuwafikishia majumbani. Urahisi wa eneo hili kusambaziwa gesi hadi majumbani unatokana na mikoa hii kuwa na mitaa inayoeleweka.

Kwa mujibu wa Killagane, wakazi wa Mtwara wanaweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwa kutumia gesi. Mbali na kuondokana na adha ya kukausha samaki kwa kutumia kuni, hata wakulima wa mhogo wanaweza kutumia gesi kutengeneza wanga badala ya kutumia mkaa na mafuta mazito, hali inayopunguza gharama za uendeshaji.

“Ni wazi Mtwara kutakuwapo mafuriko ya viwanda baada ya gesi hii kuanza kuzalishwa rasmi. Wageni mbalimbali watakwenda Mtwara, hivyo wajiandae kuwa na hoteli zenye viwango. Mradi wa kusambaza gesi, tunalenga kuwapatia gesi asilia kwenye hoteli. Tunajenga mtandao wa mabomba hadi kwenye nyumba zao na uzuri wa Mtwara mitaa imepangiliwa vizuri na hivyo upitishaji wa bomba utakuwa rahisi mno. Hata Lindi mitaa iko safi,” anasema Killagane.

Kuhusu unafuu wa gesi, anasema: “Kwa shilingi 25,000 unaweza ukatumia kwa miezi miwili hadi mitatu pamoja na kupikia maharage. Uzuri wa gesi, hakuna energy (nishati) yoyote inayopotea. Maji yakiishachemka, ule mkaa huwezi kuuhifadhi. Mkaa unatoka moshi, hivyo energy content ni kidogo ya mkaa. Gesi haina athari, mkaa hadi uanze kupuliza moshi unakuja machoni unaharibu macho, unaambiwa mtu ni mchawi [kwa kuwa na macho mekundu] wakati si kweli.

“Kama unatumia sufuria, huwezi kuona sufuria inakuwa na tone la moshi au kupata masinzi. Muda mkaa ukiwasha inabidi usubiri ukolee. Ila gesi ni mara moja,” anasema Killagane wakati akitaja faida za gesi.

Kwa Jiji la Dar es Salaam anasema kuna nyumba 70 za Mikocheni mali ya TPDC zimeunganishwa na mtandao wa gesi.

“Watu wengi walikuwa na hofu na gesi kuwa inalipuka. Gesi asilia, gesi hii hailipuki kama inayotokana na mafuta ghafi. Gesi asilia ni nyepesi kuliko hewa, ukiifungulia inatoka nje. Gesi ya kutoka kwenye mafuta ni nzito kuliko hewa, hivyo inasambaa kwenda chini. Ni salama kutumia gesi asilia,” anasema.

TPDC kwa sasa wanajenga mtandao wa kuzunguka Jiji la Dar es Salaam. Mtandao utatoka Ubungo, unakwenda Mikocheni, na barabara za Bagamoyo, Ubungo-Morogoro, Ubungo-Mandela. Kipande cha Ubungo hadi Mikocheni, kitasambaza pia gesi maeneo ya Sinza, Makongo na Mwenge kwa ajili ya jeshini Lugalo na Mbezi. Viwanda vya Mikocheni pia vitaunganishwa.

Hadi sasa kuna kituo kimoja cha mgari kujazia gesi eneo la Ubungo Maziwa. Hadi sasa magari 50 yamebadilishwa kutoka petroli na kutumia gesi jijini Dar es Salaam.

Gharama ya kubadilisha ni dola 1,000 (Sh 1,640,000) kwa gari dogo lakini unapotumia gesi, gari linatembea umbali mrefu mara moja na nusu ukilinganisha na petroli.

Killagane anasema gesi inakwenda umbali mara moja na nusu, ikilinganishwa na mafuta kwani kuna mengine hayaungui wakati gari linatembea.

Anasema gesi, hata asubuhi ukiwasha gari inatoka maji kwenye bomba badala ya moshi. “Injini inadumu muda mrefu sana, kwa maana haina carbon. Kwa utafiti tulioufanya, bei ya gesi ni chini kwa asilimia 45 ya bei ya petroli. Hii utaona kuwa gesi ni bei rahisi zaidi,” anasema Killagane. Hadi sasa viwanda 37 vimeunganishwa na gesi tayari.

Kuhusu hatari ya gesi kuvuja, Killagane anasema mabomba yanayotumiwa yana mgandamizo mkubwa kwa kiwango ambacho hayawezi kuvujisha gesi, hivyo kuna usalama wa kutosha. Hata hivyo, anasema mfumo ulivyojengwa ikitokea gesi inavuja, basi itafahamika mara moja. Pia gesi itawekwa dawa maalum, yenye harufu ya yai viza, kama kuna sehemu inavuja mtu aweze kugundua haraka kutokana na harufu hiyo.

Changamoto kubwa wanayokumbana nayo wakati wa kusambaza gesi ni utitiri wa miundombinu. “Kuna miundombinu mingi sana ipo chini na hakuna alama. Kuna fiber optic, mabomba ya maji, cable za TTCL, na sisi tunachimba mita moja na nusu, hivyo lazima tukutane na miundombinu hii.  Kwa upande wetu tunaweka tape maalum kuashiria kuwa kuna gesi. Ingependeza wote wanaoweka miundombinu wakaweka alama maalum.

Jiji la Dar es Salaam kwa siku yanatumika magunia 40,000 hadi 50,000 ya mkaa, hali inayohatarisha uwepo wa misitu. Mradi huu unalenga kuanza na maeneo kama shule, jeshi na hospitali ambao wengi bado wanatumia kuni au mkaa. Gereza la Keko tayari limeunganishwa na gesi.

Killagane anasema fedha yote ya Serikali inayotokana na mapato ya gesi itakuwa inakwenda kwenye mfuko maalum wa Serikali. Mfuko utakuwa na sheria yake na jinsi utakavyokuwa unaendeshwa. Nia ni kama sera ya gesi inavyosema, kwamba ile ni rasilimali ina kikomo. Kizazi cha leo na vizazi vijavyo, lazima vifaidi, usipokuwa na mfuko kuwekeza kwenye miradi ya muda mrefu kama miundombinu, afya na elimu, fedha zinaweza kuishia kwenye semina na makongamano.

“Sheria pia itasema zitatolewa kwa misingi gani, na zitatumikaje. Gesi isije ikaleta ugonjwa wa kushindwa kukusanya kodi katika maeneo mengine,” anasema.

Manufaa ya gesi hata sasa hivi tayari yamekuwapo. Uzalishaji wa umeme tangu mwaka 2004 nchi imeokoa takribani dola milioni 240 za Marekani kati ya Julai 2004 hadi Desemba 2013, uchumi umeokoa dola milioni 4.22 za Marekani, kwenye umeme.

Kiasi cha umeme wa megawati 320 kama gesi isingekuwapo mitambo hii ingetumia mafuta na ina maana fedha hizo zingetumika kununua mafuta. Viwanda vimeokoa dola milioni 537.59 za Marekani. Majumba na taasisi, dola 830,000, Hoteli ya Movenpick Dar es Salaam kwa sasa inatumia gesi. Hewa chafu, katika kipindi hicho tani 3.3 bilioni haikuzalishwa.

Killagane anasema baada ya Sera ya Gesi kukamilika mwishoni mwa mwaka jana, sasa inaandaliwa Sheria ya Gesi. Anasema sheria hizi zitakuwa katika makundi matatu ambayo ni Up Stream – inayohusu utafutaji na uzalishaji wa mafuta au gesi, Mid Stream – Uzalishaji na kutengeneza miundombinu ya kuchakata mafuta au gesi na Down Stream – Matumizi ya gesi ujenzi wa mabomba ya kusambaza, viwandani na kuzalisha kwa kutumia umeme.

Kwa upande wa miundombinu, anasema ni muhimu Serikali kumiliki hiyo miundombinu kuepusha mtu binafsi kuhodhi miundombinu hiyo na kuweka bei kubwa. Hata anapojenga mtu binafsi, miundombinu hii inawekewa masharti kuruhusu kila mtu anayetaka kuitumia kuruhusiwa kufanya hivyo sawa na ilivyo kwenye barabara.

“Gesi inabeba uchumi wa Taifa, miundombinu mikubwa lazima iwe ya Serikali na ndivyo ilivyo dunia nzima. Unaweza kumwachia mtu binafsi akafunga, hata umeme, transmission line ni za Serikali, ukimwachia mtu kesho anang’oa anasema haimpatii faida,” anasema Killagane.

Kwa nia ya kumfaidisha zaidi Mtanzania, sheria inamtaka mwekezaji kutumia bidhaa na huduma zinazopatikana Tanzania. Ikiwa bidhaa na huduma zinazohitajika hazipatikani kwa ubora unaotakiwa hapa nchini, kampuni zinapaswa kusaidia kujenga uwezo wa Watanzania.

“Kwa mfano, kama unasema unataka nyanya, kama pale Mtwara huwezi kuzipata uwasaidie wale watu waweza kuzalisha nyanya kwa kiwango unachokitaka. Hata hivyo, hatutaki udalali katika kufanya hivyo kwani unaongeza gharama kwa mtumiaji,” anasema Killagane.

Vijana 189 wamepelekwa nchini China kusomea masuala mbalimbali ya gesi. Utaalamu wa kwenda kwenye visima, vijana wanaopelekwa Dubai wanajifunza kwa miezi mitatu ndipo wanaruhusiwa kwenda kwenye mitambo ya kuzalisha gesi. Hii ni fursa nyingine kwa Watanzania kupata ajira ya uhakika.

Killagane amekuwa TPDC tangu mwaka 1975 akianzia upande wa uhasibu, baadaye akaenda utawala na mwaka 1991 akawa Mkurugenzi Mtendaji.

Anahitimisha mahojiano kwa kusema suala la ulinzi wa bomba la gesi linapewa kipaumbele mno. “Hili bomba litakuwa uhai wa Taifa lazima lilindwe sana. Utakuwapo ulinzi shirikishi kwa wananchi katika vijiji vyote linakopita bomba hilo,” anasema Killagane.

1655 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!