Baadhi ya kampuni zilizoomba zabuni kwenye Awamu ya Tatu ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu II, zimeghushi nyaraka.
Mradi huo wenye thamani inayokaribia Sh trilioni moja, unalenga kufikisha umeme wa gridi kwenye vijiji 3,559 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Kubainika kwa udanganyifu huo kumekuja ikiwa ni siku chache baada ya JAMHURI kuandika taarifa inayoonesha kuwa kuna ‘mchezo usio wa kawaida’ unaofanywa na makandarasi na baadhi ya watumishi waandamizi katika Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwapo kwa kampuni zilizodanganya sifa zake zilizowasilishwa REA.


Miongoni kwa kampuni zinazotajwa ni Al-Hatimy Developers Limited ambayo imepewa barua ya kusudio la tuzo kwa zabuni ya kusambaza umeme kwa thamani ya Sh bilioni 59.816.
Kampuni hiyo ilikusudiwa kufanya kazi hiyo katika wilaya za Chato, Nyang’wale, Bukombe na Mbogwe mkoani Geita.
Imebainika kuwa kwenye rekodi za REA, Al-Hatimy imesajiliwa kwa Daraja la I, lakini rekodi zilizoko Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) zinaonesha kampuni hiyo ni ya Daraja la II kwenye masuala ya umeme. Viongozi wa kampuni hiyo wamekuwa hawapokei simu kufafanua tuhuma zinazowakabili.
Chanzo chetu cha habari kimesema: “Awali kampuni hii iliingia ubia (Joint Venture [JV]) na kampuni moja ya kizalendo. Ikafanya hivyo kuomba zabuni REA. Ilipofanikiwa, ile kampuni iliyoingia nayo JV ikatupwa kando. Hatujui kwanini (Al-Hatimy) aliamua kufanya hivyo, lakini tunadhani aliona atumie mbinu hiyo kupata zabuni yeye mwenyewe kwa kumtupa nje yule mwenzake (mzalendo).”


Kuna habari kuwa REA walipotaka taarifa za uhakiki kutoka CRB ndipo walipobaini ‘mchezo’ huo, na kwa maana hiyo Al-Hatimy ikawa imepoteza sifa za kupewa zabuni hiyo. Kwa kawaida kampuni yenye Daraja la II inatakiwa ituzwe zabuni isiyozidi Sh bilioni 1.2; lakini hii ilikuwa ipate karibu Sh bilioni 60.
Kampuni, au ubia wa kampuni zenye sifa ya kuwa Daraja la I inakuwa haina ukomo wa kiasi cha fedha kwenye zabuni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi Tanzania (CRB), Consolata Ngwimba, amezungumza na JAMHURI na kuthibitisha kutofautiana kwa taarifa za Al-Hatimy zilizoko REA na zile walizonazo CRB.
“Yeye anajitetea kwamba hakupeleka Daraja la I kule REA, lakini nyaraka zake zinaonesha hivyo. Sisi kwetu Al-Hatimy amesajiliwa Daraja la II. Namba za nyeti alivyopeleka REA na zilizoko CRB ni tofauti. Haiwezekani jambo kama hili litokee kwa bahati mbaya.
“Aliomba joint venture, kwenye pre-qualification akaonekana peke yake, hiyo naamini ikawa sababu ya kutiliwa shaka kule REA maana kama ukighushi unapoteza credibility,” anasema Ngwimba.


Mwenyekiti huyo anaupongeza uamuzi wa REA wa kuwapa zabuni makandarasi wazalendo, lakini anasema ni vizuri hao wazalendo wakawa na sifa, badala ya kufanya ujanjaujanja.
Kuhusu uhalali wa makandarasi wa nje kama kweli wana sifa, anasema wanazifanyia uchunguzi wa kina (due diligence) kabla ya kuzipatia ruhusa ya kufanya kazi nchini.
Nayo kampuni ya Power Magic Electrical Contractor and Suppliers, iliyokuwa imepewa barua ya kusudio la zabuni, imeondolewa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukosa sifa.


Iliondolewa kwa barua ya Mei 15, mwaka huu; siku ambayo JAMHURI  lilifanya mahojiano na viongozi wa ngazi ya juu wa REA jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa maswali waliyoulizwa yalihusu ‘kupewa zabuni’ kampuni hiyo licha ya kuwa usajili wake ni wa Daraja la V; na haikuwa na mbia.
Power Magic Electrical Contractor and Suppliers ilikuwa tayari imeshajihakikishia lots za mbili. Moja ikiwa ya dola milioni 2.86 za Marekani; na Sh bilioni 14.095. Kiasi hicho ni kwa mradi wa umeme katika wilaya za Chamwino, Kondoa na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Lot ya pili ilikuwa ya dola milioni 4.32 za Marekani; na Sh bilioni 24 kwa ajili ya kutekeleza zabuni katika Mkoa wa Singida.


Mkurugenzi Mkuu wa REA, Injinia Gissima Nyamo-Hanga, ameliambia JAMHURI kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kwa kampuni zote zilizopewa barua za kusudio la kutuzwa zabuni.
“Uchunguzi unaendelea kwa kina, hatuwezi kusaini na kampuni zenye kasoro. Hatujasaini mkataba, utaona tu kazi tutakayofanya – hatuwezi kusaini na mtu mbovu, kuna vyombo vinavyofanya kazi hiyo (ya uchunguzi), amesema.
Alipoulizwa idadi ya kampuni zilizokwishaonekana kuwa hazifai, Nyamo-Hanga, amesema: “Bado kazi inaendelea, tunafanya kazi hii ili kuzibaini zote. Zipo zilizokwishajulikana, naamini mtazijua tu.”
Wakati hayo yakiendelea JAMHURI, limeambiwa kuna mgongano mkubwa wa maslahi kwa baadhi ya kampuni zilizoomba zabuni na kupewa barua za kusudio la tuzo kuwa na uhusiano na baadhi ya watumishi wa REA.
Mmoja wa wamiliki wa kampuni ya EL’s ambao wana ubia na Joe’s amebainika alikuwa mshauri wa REA kwenye Mradi wa Awamu ya Pili.


“Alikuwa na mkataba REA hadi Novemba, 2016. Hizi zabuni za REA Awamu ya Tatu zilianza kujulikana Septemba, 2015 kwa hiyo alikuwa na taarifa zote, na sasa yuko kwenye kampuni zilizo kwenye orodha ya kutuzwa zabuni.
“Huyu amefanya kazi katika kampuni ya Botswana, ameamua kushirikiana nayo kupata zabuni. Huyu ana binamu yake mwajiriwa wa REA (mkurugenzi) kwa hiyo mambo yote ya ndani na nje wanayajua. Hawa ni ndugu. Ndani ya REA kuna ‘vijana wao’ ndiyo maana walishajua watapata lots ngapi hata kabla ya zabuni kutangazwa,” kimesema chanzo chetu.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa baadhi ya kampuni zina uhusiano, ama moja kwa moja, au wa kificho na baadhi ya wabunge, mawaziri na vigogo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Miongoni mwa wabunge na mawaziri hao ambao kwa sasa tunahifadhi majina yao, wanatoka mikoa ya Pwani na Dodoma.  
Utata mwingine umejitokeza kwa kampuni ya Nipo Group Limited inayopewa kazi katika Mkoa wa Arusha. Kwenye usajili CRB inaonekana kuwa ni ya Daraja la V.


Kampuni hii imepewa zabuni ya dola milioni 2.011za Marekani; na kiasi kingine cha Sh bilioni 15.545; ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya kazi za kiwango cha gridi. Haina mbia kama ilivyo kwa kampuni nyingine za Watanzania ambao hazina sifa ya Daraja la I.
Barua ya Mkurugenzi Mkuu wa REA kwenda kwa Nipo Group Ltd ya kusudio la kuipa zabuni, inahitaja kampuni hiyo ikiwa yenyewe bila mbia.


Lakini kwenye taarifa ya REA ambayo (imechapishwa kwenye gazeti hili), REA wanasema Nipo Group Limited wana ubia na Nipo Africa Limited yenye usajili wa Daraja la V.
“Iweje kampuni nyingine zote ziwe zimeonesha JV zao kwenye maombi, lakini Nipo Group Ltd wao waonekane wana ubia baada ya habari kuandikwa?” Kimehoji chanzo chetu.
Nipo Group Limited inatajwa kuwa na uhusiano wa karibu na mmoja wa mawaziri. Mara kadhaa waziri huyo amesikika akieleza ‘alivyotokwa jasho’ kuhakikisha washirika wake hao wanafanikiwa.

By Jamhuri