Wakati naandaa makala niliyosema “Kinachonifanya nimpende Lowassa ni hiki” na kuichapisha katika gazeti hili la JAMHURI wiki iliyopita, hayakuwa mategemeo yangu kama makala hiyo ingeigusa jamii kwa kiasi nilichokishuhudia. Nimepigiwa simu nyingi mno, nimetumiwa ujumbe mfupi wa maandishi mwingi,  na bado mpaka sasa naendelea kupokea simu na ujumbe!

Kwa walionipigia simu nilizungumza nao, lakini sikuweza kuwajibu wote walionitumia ujumbe mfupi wa maandishi. Kwa vile sasa nahitimisha mjadala huo, naomba wote ambao sikuwajibu wapate majibu yangu kwenye makala hii. Kwa walioniunga mkono moja kwa moja sina majibu yao, isipokuwa nawashukuru sana na kusema kwamba tuko pamoja.

 

Kuna swali nililokutana nalo mara nyingi la kwamba Lowassa kakutuma? Nataka nijibu kwamba Lowassa hajanituma kitu, na kusema ukweli hanijui kabisa. Msukumo wangu wa kuandika makala ile umetokana na vitendo vyake kama kiongozi.


Naomba tuelewane kidogo, sikutaja sifa za Lowassa kimaumbile, kusema kwamba pengine nimevutiwa na sura yake, urefu wake au mvi alizo nazo. Kilichonisukuma ni umahiri wake alio nao katika kazi, uthubutu wake, ujasiri wake, ubunifu wake, kujitegemea kifikra nakadhalika. Hayo ndiyo yaliyonifanya nimuone Lowassa kuwa anafaa kutuongoza.

 

Jambo lingine ambalo naendelea kukutana nalo hadi sasa ni la tuhuma za rushwa katika mkataba wa Richmond. Ninachotaka niseme juu ya hilo ni kwamba kwa bahati nzuri nchi yetu, tangu ilipopata uhuru mwaka 1961, inaendeshwa kwa mjibu wa Katiba na sheria zilitungwa na wananchi wenyewe kupitia kwa wawakilishi wao, wabunge. Na nchi yetu imesimama kwenye mihimili mitatu, Serikali, Bunge na Mahakama.


Chombo cha juu kabisa kinachothibitisha kosa la mtu ni Mahakama. Kwahiyo kama Mahakama zipo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, polisi tunao na bado sijasikia Lowassa yupo mahakamani, hata kujibu tuhuma tu, inatia shaka sana kiasi cha kunifanya niamini kwamba yanayosemwa juu yake kuhusu Richmond ni mbinu chafu dhidi yake.


Kwa maana hiyo tuhuma hizo naziona si tuhuma tena bali porojo. Porojo hazikunifanya nikose kumuona mtu anayefaa kuwa kiongozi wangu mkuu. Halikadhalika porojo hizo hazimnyimi yeye, kama mwananchi mzalendo, uhuru wa kugombea nafasi ya urais kama ana nia hiyo.


Nimeamua kuziita tuhuma hizo porojo sababu naelewa, kwa mazoea miongoni mwetu, kila litokalo kinywani mwa mtu au watu, kuna wanaotokea kulichukulia kiuhalisia kama vile ni kauli ya Mungu!


Mfano kuna wakati fulani watu waliwahi kutamka kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati akiwa hai, ni tajiri namba moja hapa Tanzania na wa pili ni marehemu Oscar Kambona. Kwamba Kambona kuishi kwake uhamishoni  London ni mbinu tu za kuyalinda mabilion yao.

 

Wakati mwingine zikatoka porojo kwamba Waziri Mkuu wa zamani na aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Cleopa David Msuya, ni tajiri namba moja katika Afrika Mashariki. Kwamba anamiliki kiwanda cha kutengeneza magari kule India, na kwamba magari hayo ni aina ya DCM. Tukaambiwa kuwa kirefu cha DCM ni David Cleopa Msuya. Wengi wakaiamini porojo hiyo.


Haikuishia hapo, pale kwenye barabara ya Shekilango, Jijini Dar es salaam,  palikuwepo na kampuni kubwa iliyokuwa ikimiliki malori mengi. Kampuni hiyo ilihusishwa na aliyewahi kuwa waziri wetu mkuu, Salim  Ahmed Salim.


Hizo ni baadhi ya porojo ambazo lakini ziliwafanya baadhi ya wananchi wawaangalie kwa jicho baya wale waliokuwa wakitajwa.


Lila na fila havitangamani. Baada ya muda tukagundua kuwa Baba wa Taifa, Mungu amlaze mahali pema, kumbe hata masurufu alikuwa akiyarejesha. Hakuwahi kujirundikia mali wala fedha. Oscar Kambona tulimuona alivyorejea nchini akiwa hajiwezi kiafya na kifedha. Mzee Msuya sidhani kama ana mahali pengine zaidi ya pale alipo. Salim Ahmed Salim sijui hata kama akipewa mtaji biashara ni fani yake. Kweli lila na fila havitangamani.


Kuendelea kuwatuhumu tu viongozi wetu bila mahakama kuhusishwa ni jambo ambalo wanaolitenda inawabidi wajifikirie mara kadhaa. Sababu hili ni gonjwa hatari ambalo naamini kwamba dawa yake tunayo sisi. Dawa yake ni kuwalazimisha wote wanaowatuhumu wawapeleke mahakamani, vinginevyo wanaotuhumu ndio wapelekwe mahakamani.


Ni mahakama pekee inayoweza kutupatia ukweli. Nje ya mahakama ni kuoneana,  wakati mwingine kwa chuki tu. Fikiria una mtu unayemchukia na unakutana naye katikati ya watu wengi, ukitaka kumkomesha wewe piga kelele za mwizi. Akikamatwa dadika mbili tu zinatosha kumfanya aharibiwe vya kutosha na pengine kubaki maiti. Hakuna anayeuliza kaiba nini, wapi na lini. Maana yake nini, ni kwamba tumejizoesha kuamini litokalo vinywani mwa watu, hatujipi muda wa kuuliza. Hii ni hatari.


Swali lingine nililokutana nalo ni kwamba, anayotuhumiwa nayo Lowassa kama si ya kweli kwa nini akae kimya kiasi hiki? Kwa hilo nadhani binadamu tumejaliwa mengi, lakini wapo ambao hawakujaliwa kuwa na tani za meno vinywani mwao. Na mara nyingi watu wa vitendo hupungukiwa na maneno, Lowassa ni mtu wa vitendo,  au pengine muda wake ukifika atalizungumzia.


Namalizia kwa upande huo kwa kusema kwamba tuhuma bila kupelekana mahakamani ni porojo, hakuna tena muda wa kuamini porojo.


Nasema bila kuota wala kuuma maneno kwamba kutuhumiana bila ushahidi ni mbinu chafu zinazolenga kuwamaliza kisiasa wale wanaoonekana kukubalika katika jamii. Jamii nayo inapaswa kuliona hilo na kusema hapana. Lazima likemewe kwa nguvu zote.


Wapo waliosema Lowassa ni mbabe, kwamba hana taratibu za kazi. Lakini katika tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba mbabe ni mtu anayetumia nguvu zake, ziwe za mwili au madaraka, kumnyima mtu haki yake kiuonevu. Ni lini Lowassa alimuonea mtu kwa mtindo huo?


Hivi mhandisi aliyekwenda shule anaposimamia ujenzi wa ghorofa nne akakubali zitumike nondo mm. 12 ghorofa likaanguka, akisemwa mtadai kaonewa? Mwingine anasimamia ujenzi wa daraja lakini hata kabla ujenzi haujaisha daraja linaanza kupata nyufa, akisemwa mtadai anaonewa? Nesi yuko zamu, analetwa mgonjwa mahututi anaendelea kuchezea simu yake ya kiganjani, akisemwa mtadai anaonewa?


Watu wa aina hiyo wakitimuliwa kazi papo kwa hapo watadai ndio ubabe? Je, hao nao wanahitaji waundiwe Tume ya maadili kuwachunguza? Hao inabidi watambue kwamba hawatendi haki, kwahiyo kuwafukuza kazi papo kwa hapo ndio kuwatendea wao haki. Lowassa analitambua sana hilo.


Kwa Watanzania wengi bado wanaamini kwamba uhuru ni kufanya utakavyo hata kama ni kinyume cha sheria na utaratibu, kwenda kazini kwa muda utakao, kutega kazi, kuwa na visingizio, kutotimiza wajibu nakadhalika. Wale wote wenye tabia za aina hiyo ni lazima wamuogope sana Lowassa maana yeye si sitahili yao.


Lowassa si kiongozi anayekuwa kwenye shughuli za kukagua maendeleo ya taifa aishie kudanganywa kwa kuchezewa ngoma na kwaya za kumsifia zikiambatana na vitafunwa pamoja na vinywaji, kwa wahusika kudhani mawazo yake yatahamia huko na kukosa kukiangalia alichokikusudia. Akikuta umetimiza wajibu atakupongeza, lakini kama umeshindwa atakupa haki yako unayoisitahili. Kamwe huo si ubabe, ni umahiri na ujasiri wake kama nilivyovielezea hapo juu.


Pia wapo walioongelea michango yake katika misikiti na makanisa. Hivi tunatarajia nini kwa mtu aliyepata kuwa kiongozi wetu wa juu? Kweli tunaweza kuona fahari kumuona Lowassa akiwa kwenye tamasha la mashindano ya mbio za mbuzi ambayo kwa mtu timamu ni kioja na vichekesho? Lini mbuzi akatamani mashindano ya mbio?


Makanisani na misikitini yapo mengi ya kuchangia, shule, watoto yatima, walemavu na kadhalika. Kwa yule anayeona Lowassa anakosea kwenda maeneo hayo nadhani atakuwa na utambuzi kidogo sana kwa nini yupo duniani, ila amebarikiwa kwa wingi wa ubinafs, husuda na fitina.


Sababu kuhusika kwa Lowassa kwenye mambo hayo yanayopigwa vita na baadhi ya watu, ndivyo inavyopaswa kuwa kwa kiongozi. Inaonyesha na kudhihirisha kwamba anaweza kufanya kazi za kitaifa, hata kama hana madaraka ya kitaifa kwa sasa, na hapo ndipo picha yake inapoonekana.


Kiongozi bora lazima awe na kitu moyoni mwake hata kama hayupo madarakani, kile kilichomo rohoni mwake kitaendelea kutokeza na kudhihirika.


Mfano Baba wa Taifa alipostaafu hakuanza shughuli za kutalii, bali aliendelea na juhudi zake za kuhubiri amani, kupatanisha penye migogoro, sababu hilo ndilo lililokuwa rohoni mwake. Rais Mwinyi anaendelea na juhudi za kuhakikisha Kiswahili kinakuwa lugha kubwa, si katika Afrika tu, bali duniani kote bila kusahau matembezi ya mshikamano, hayo naye yamo rohoni mwake.


Kwahiyo wanaomwalika Lowassa kwenye matukio ya makanisa na misikiti hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya wala kwa kubahatisha tu, au kwa vile wanaona alivyo na pesa, hapana, wanaangalia rohoni mwake pana nini. Pia, hata Lowassa mwenyewe amekwishasema kuwa fedha hizo anachangiwa na marafiki zake wapenda maendeleo.


Wapo wanaouliza kwamba Lowassa pesa anapata au anatoa wapi. Kwa nini kwanza tusishangae michango mikubwa inayotolewa na kutumika katika sherehe moja tu ya harusi? Hivi sasa sherehe ya kawaida inagharimu shilingi milioni 15 – 35, hicho kimeishakuwa kipimo kwa mtu wa kawaida. Pesa hiyo kwa kiasi kikubwa inatumika kwa kula, kunywa na kusaza!


Kama hivyo ndivyo, kuna ubaya gani kama Lowassa na rafiki zake watachanga na kutoa milioni 10 – 20 kwa maendeleo ya jamii? Sioni ubaya wake katika hilo, sana sana nitazidi kumpongeza tu. Kwa kufanya hivyo anatuonyesha njia sahihi, nini wajibu wake kwa jamii.


Wakati naelekea mwisho sitaki kuwasahau wasomaji watatu waliomwita Lowassa ifuatavyo; mmoja alimwita jembe, mwingine akamuita shoka na wa mwisho akamuita sululu! Mimi nadhani kwa kuwatendea sawa wote hao watatu nawapatia mpini imara wa shaba usiovunjika wala kuungua.


Ikifika wakati unataka kulima unaweka mpini wako unalima, ukifika wakati wa kupasua miamba unachukua mpini unaweka kwenye sululu, kazi inaendelea. Hali kadhalika ifikapo kazi ya shoka unaweka mpini kazi inasonga mbele. Hongera sana Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0717 599 579


1436 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!