Vyama vya upinzani ni vichanga? -4

Katika sehemu ya tatu ya makala haya wiki iliyopita, nilizungumza uchanga wa vyama vya siasa na malengo yao. Pia niligusia kauli iliyotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa Uchaguzi Mkuu 1995 kuhusu uwezo wa vyama vya upinzani kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2015. Leo tunaendelea…

Hivi tunavyozungumza CCM na vyama vya upinzani kila kimoja kimo katika harakati ya kupanga mipango ya kushinda uchaguzi huo. CCM itafikisha miaka 38 na baadhi ya vyama vya upinzani vitafikisha miaka 23. Hapatakuwa tena na suala la uchanga wala watoto. Labda suala la utoto!

Hali au tabia ya kufanya mambo kama mtoto ni utoto, daima watoto hawadumu katika michezo yao. Aghalabu wanapokuwa katika shughuli zao hupenda kulizana, kulalamikiana, kushtakiana na kupigana ngumi. Ugomvi ndiyo kilele cha shughuli zao za kila siku. Ndiyo maana wahenga wamesema ngoma ya watoto haikeshi.

 

Dhana ya kuwa na vyama vingi vya siasa ni katika utekelezaji wa demokrasia ya kweli inayohitaji kuwako kwa ushiriki wa wananchi katika uamuzi wa mustakabali wa maisha yao.

Kuwa na uchaguzi huru na haki, utawala wa kisheria, utekelezaji wa haki za binadamu, usawa na uwajibikaji. Pamoja na hayo upo udhibiti wa matumizi mabaya ya madaraka, stahamala kisiasa na uhuru wa kiuchumi chini ya Katiba iliyoundwa na wananchi wenyewe.

Kutokana na maelezo kama hayo nilitarajia kuona ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa, ungeleta uhusiano mzuri baina ya chama na chama na kulenga kuboresha uchumi wa wananchi.


Kasi ya kuleta maendeleo ya watu ingekuwa kubwa kutokana na vyama kushirikiana katika kuhamasisha na kufafanua sera zao, katika kukomesha maovu na kujenga uchumi imara wa Taifa.


Lakini leo, hali halisi haikuwa hivyo, imekuwa kinyume chake, kwani vyama vinavyobeba bango la upinzani, vinakandia sera na juhudi za chama kilicho madarakani.


Lengo ni kuking’oa madarakani tu, hata kama uamuzi wa chama hicho ni mzuri na wenye tija au sera zake zinawiana na sera zao. Haviko tayari kusifu kazi nzuri iliyofanywa kwa wananchi, isipokuwa kutoa dharau na kukashifu kazi nzuri hizo.


Kwa mfano, hivi majuzi, tumeshuhudia vyama vya upinzani vilivyojizatiti kupinga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, asitie saini muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba kwa madai kuwa mchakato wa sheria haukuzingatia taratibu zilizopo na si kamilifu. Hivyo, muswada urudishwe bungeni kwa majadiliano zaidi na baadaye ndiyo rais atie saini yake.


Ukweli uliopo, tena mchana kweupe, lengo ni kuvuruga na kuchelewesha taratibu za kupata Katiba mpya, ambayo wao ndiyo waliokuwa vinara wa mageuzi ya kuwa na Katiba inayoshirikisha wananchi.


Cha ajabu, baada ya kuona kumbe mambo yanakwenda shwari na sifa zitakwenda kwa chama tawala, waliona heri kutia angalau dosari ndogo ili mambo yakwame na hapo wapate kunena, si mnaona! Hawawezi hawa! Kama hivyo ndivyo, nathubutu kusema hiyo si dhamira ya kuwa na vyama vingi vya siasa. Tujiweke sawa.


Ombi lao halikupata mafanikio kama mahitaji yalivyotaka. Kwanza sheria ilibidi kufuatwa na kumtaka Rais Kikwete kuweka saini yake. Pili, malalamiko, marekebisho na mapendekezo yapelekwe bungeni, ambako muswada huo wenye saini ya rais, utafanyiwa hayo mahitaji adhimu.


Uamuzi huo ulikubaliwa na vyama vya upinzani. Je, huoni suala la ushirikiano lilihitajika baina ya vyama vya upinzani, chama tawala na Serikali yake? Kukutana na kujadiliana juu ya suala hilo na hatimaye kuafikiana bila kutoleana maneno ya kashfa na vidole machoni.


Hapa, napenda kutanabaisha kwamba Watanzania kura tunazo mikononi. Je, tuendelee kuichagua CCM kwa sababu inatawala, inatulea, inafanya mambo mengi mazuri kwa wananchi na tunatoka nayo mbali tangu enzi za wazazi wake TANU na ASP, lakini ina sifa za tuhuma dhahiri shahiri za baadhi ya viongozi na wanachama wake ni watoa na wapokea rushwa, wezi na mafisadi?

 

 

By Jamhuri