Nilikuwa naelekea kukata tamaa kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitakuwa na viongozi wanaokerwa na umaskini unaoendelea kuwanyima Watanzania wengi maendeleo ya kweli.

Lakini nikiri kwamba hatimaye wiki iliyopita, wewe Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, umeusitisha moyo wangu kukata tamaa hiyo kwa jinsi ulivyoanza vizuri.

 

Ikiwa ni wiki moja tu tangu uteuliwe na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kushika wadhifa huo nyeti katika chama tawala, umeanza vizuri, umenitia matumaini.

 

Kinana, kitendo chako cha kutangaza vita dhidi ya vigogo walioshindwa kuendeleza viwanda vya kubangua korosho baada ya kuvinunua serikalini, ni hatua nzuri, umeanza vizuri lakini una changamoto ya kuhakikisha unaendelea na kumaliza vizuri.

 

Umetaka viwanda hivyo vipatavyo 12 huko mkoani Mtwara, ama vianze kufanya kazi ama virudishwe serikali kwani imebainika kwa sasa havifanyi kazi ya kubangua korosho, badala yake vimegeuzwa maghala ya kuhifadhi korosho ambazo hazijachambuliwa zikisubiri kusafirishwa kwenda nchi za China na India.

 

“Wamenunua viwanda vyetu lakini wameshindwa kuviendeleza, ajira zimepotea, wananchi wa Mtwara wanaendelea kuwa maskini.” Hii ni sehemu ya kauli yako Mheshimiwa Kinana, uliyoitoa wakati ukihutubia mkutano wa wananchi katika Kijiji cha Mkunwa, Mtwara, wiki iliyopita.

 

Tena nisichelewe kukupongeza Mheshimiwa Kinana kwa kubaini kuwa uhai wa viwanda hivyo uliwezesha ajira kwa wananchi wengi, lakini baada ya kufungwa wengi wakiwamo vijana sasa wanakosa ajira.

 

Ni ukweli usiopingika kwamba vigogo walionunua viwanda hivyo wamechangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha uchumi wa mikoa iliyopo Kusini mwa Tanzania. Lakini pia wamekuwa wakivitumia kujiombea mikopo kwenye benki kwa ajili ya kujinufaisha na familia zao.

 

“Tumechoka, sasa ni lazima tukatae unyonyaji huu. Wabunge wa Mtwara ni lazima tusaidiane kusimamia hili hata kama kwa kutunga sheria itakayolinda viwanda vyetu. Kama wao wamenunua viwanda wakakiuka masharti yanayowataka kuviendeleza, sisi tutashindwa vipi kutunga sheria itakayolinda wakulima na viwanda vyetu?” Hii ni kauli yako nyingine Mheshimiwa Kinana, yenye sura ya kutetea rasilimali za nchi zitumike kunufaisha umma.

 

Kinana, ukumbuke viongozi wengi wa CCM na serikali waliopita na hata waliopo sasa wamekuwa na kauli za aina hiyo, tamu mithili ya asali, lakini wameishia kuwa nguvu ya soda ambayo daima huanza kwa kasi kubwa ya ajabu na kuisha kinyonge mno.

 

Bila shaka wewe Kinana umejipanga vizuri kuhakikisha kasi uliyoanza nayo huko Mtwara haiishii kuwa nguvu ya soda. Umeanza vizuri na bila shaka utaendelea na kumaliza vizuri. Tena bila shaka utasimama kwenye maneno yako.

 

Ninaposema utaendelea na kumaliza vizuri ninamaanisha kuwa hautaishia kutaka viwanda vya korosho vilivyofungwa huko Mtwara virejeshwe serikalini ikiwa vigogo waliovinunua wameshindwa kuviendeleza. Kwamba utaendelea kushughulikia hadi kuwezesha ufumbuzi wa matatizo mengine lukuki yanayowakabili wananchi.

 

Watanzania wengi watafurahi kuona na kusikia unashughulikia kupata ufumbuzi wa dhuluma zinazofanywa na wawekezaji wa kigeni dhidi ya wananchi, ambao baadhi yao wananyang’anywa ardhi zao na kulipwa fidia duni kupisha miradi mbalimbali ikiwamo ya uchimbaji madini. Kinana ukumbuke wachimbaji wadogo wa madini wamekuwa wakiahidiwa kutengewa maeneo ya uchimbaji kwa miaka mingi sasa bila mafanikio.

 

Mheshimiwa Kinana, juhudi zako zilenge pia kumulika tatizo la mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali linaloendea kuwatafuna wananchi mithili ya mchwa utafunavyo nguzo na paa za nyumba. Siku hizi kila mfanyabiashara anajipangia na kupandisha bei ya bidhaa wakati wowote atakavyo. Wanaoumizwa zaidi na mfumo huu wa kidhalimu ni Watanzania wengi wasiyo na uwezo wa kiuchumi katika nchi hii.

 

Gharama kubwa za elimu kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo ni mzigo mwingine mkubwa unaoendelea kuwaelemea wananchi wengi. Kinana usisahau kukemea na kutaka serikali idhibiti michango holela katika shule isiyozingatia kipato duni cha Mtanzania. Watoto wengi kutoka familia maskini wameendelea kukosa elimu nchini na bado serikali haijawaona kwa jicho la huruma!

 

Lipo pia tatizo la viongozi wachache wanaofanya ubadhirifu wa mali za umma na kuhujumu uchumi wa nchi yetu. Hawa nao usiwaonee haya katika juhudi zako za kushughulikia matatizo yanayowanyima Watanzania maendeleo ya kweli.

 

Tafiti zinazofanywa na taasisi na watu mbalimbali zinaonesha kuwa tabaka kati ya matajiri na maskini linaendelea kupanuka kila siku. Watu wachache wanazidi kunufaika na rasilimali za nchi hii na kupata utajiri mkubwa kupindukia huku walio wengi wakizidi kuwa maskini kupindukia!

 

Kuna watu katika nchi hii wanaishi kwa kipato cha chini ya Sh 1,000 na kula mlo mmoja kwa siku, huku wajanja wachache wakipata zaidi ya Sh 500,000 na kula milo zaidi ya mitatu kwa siku! Hii ni taswira mbaya hata mbele za Mwenyezi Mungu.

 

Rushwa nayo ni miongoni mwa kero kubwa inayoendelea kuvuruga maisha ya Watanzania wengi. Inasababisha wengi kukosa haki mbalimbali katika ofisi za umma. Baadhi ya wagonjwa na wajawazito wanakufa baada ya kunyimwa huduma, kisa wamekoswa fedha za kununua huduma za kitabibu kwa wauguzi na madaktari wanaolipwa mishahara kutokana na kodi za wananchi!

 

Basi itoshe tu kusema kwamba Mheshimiwa Kinana umesikika, umeonesha makali yako huko Mtwara, umeanza vizuri. Lakini kikubwa sasa ujue kwamba una changamoto kubwa ya kuhakikisha unayosema yatatekelezwa kwa vitendo. Kwa kufanya hivyo utakuwa umeendelea na kumaliza vizuri katika juhudi zao za kutetea maslahi ya umma. Mwenyezi Mungu akutangulie.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

By Jamhuri