King Enock (wa pili kushoto) akiwa jukwaani na Dar es Salaam Jazz mwaka

TABORA

Na Moshy Kiyungi

Mzaliwa wa Zambia, Michael Enock, aliyekuja kutambulika baadaye kama ‘King’ au ‘Teacher’, aliingia nchini mwaka 1960 na kuwa nguzo ya muziki wa dansi.

Pamoja na sifa kubwa alizokuwa nazo miongoni mwa mashabiki wa muziki na hata watu wa kawaida, King Enock, kwa takriban miaka 44 nchini, aliishi katika mazingira duni maeneo ya Mwenge, jijini Dar es Salaam.

“Sikutegemea kuwa maskini kiasi hiki. Jasho langu limepotea kwa kuwa miaka ya nyuma hakukuwapo chombo cha kulinda haki za wanamuziki,” amewahi kusema nguli huyo katika mahojiano na mwandishi wa makala hii akiwa kitandani akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi.

Kitu pekee kilichomfariji ni kuona wanamuziki wengi wamepita mikononi mwake, akiwafundisha muziki kuanzia miaka ya 1960 kukiwa na upinzani kati ya Dar es Salaam Jazz na Western Jazz.

Jina lake kamili ni Michael Enoch Chinkumba aliyezaliwa Oktoba 1942, Luansha nchini Zambia.

Alianza kuonyesha kipaji cha muziki tangu akiwa mdogo, akitengeneza gitaa lake la kwanza kwa kopo na nyuzi nyembamba, kisha akaanza kujifunzia kupiga.

Baadaye akatumia magitaa yaliyonunuliwa na kaka yake na wakiwa shuleni, tayari walishaanza kufanya maonyesho ya muziki nyakati za usiku, wikiendi; wakiwa na kundi lililojulikana kama ‘Music Brothers Concert Group’.

“Kundi letu lilikuwa na akina dada watatu; Adesi, Rhoda na Pani, lakini hawakudumu kwani mwaka mmoja tu baadaye (mwaka 1958) wakapata wachumba na kuolewa,” anasema Teacher.

Wakati tayari ameshahitimu masomo ya masuala ya muziki katika chuo rasmi nchini Zambia,

aliyemleta nchini ni mwanasiasa mkongwe na mdhamini wa TANU enzi hizo, John Mwakangale, aliyekitambua kipaji chake alipotembelea Zambia mwaka 1960.

Mwakangale na ndugu zake wakaanzisha bendi mjini Mbeya yenye wanamuziki kutoka Malawi, Zambia na Tanzania ikijulikana kwa jina la ‘Three Brothers’; bendi ya kwanza nchini kutumikiwa na Michael Enock.

Bendi hiyo ilitoa upinzani mkali kwa Mbeya Jazz iliyokuwapo mjini humo.

Baada ya maonyesho Mbeya, Chunya, Tabora na Mwanza, bendi hiyo ikasambaratikia Mwanza mwaka huo huo baada ya vyombo vyao vyote vya muziki kuibwa.

“Viliibwa Mwanza wakati tukijiandaa kwenda kupiga muziki Musoma. Baada ya kuvipakia kwenye lori, dereva akasema anakwenda kujaza mafuta, kumbe ni mwizi! Akatokomea na hatukumuona tena,” anasema kwa masikitiko.

Maisha ya deiwaka kwa Enock yakaanza. Akatoka Mwanza na kwenda kujiunga na bendi moja huko Nzega akitumia vyombo vya kuazima.

Akiwa Nzega, mwanadada (mmoja wa viongozi) kutoka Dar es Salaam Jazz, Bilimi Ally, alimuona ukumbini akipiga solo vizuri sana; akazungumza naye, wakakubaliana, kisha wakapanda treni kwa safari ya Dar es Salaam!

Akajiunga na Dar es Salaam Jazz, Majini wa Bahari, na kukutana na magwiji wa muziki wa dansi wa wakati huo, wakipiga muziki katika mtindo wa ‘Mundo’.

Bendi hiyo ilirekodi nyimbo kadhaa maarufu katika studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) siku hizi TBC Taifa na studio za Chandarana nchini Kenya.

Uchakavu wa vyombo ukaikumba bendi hiyo na mwaka 1978 ikashindwa kuendelea na kazi.

Michael Enoch akaenda kuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Dar es Salaam International iliyokuwa ikimilikiwa na Zakaria Ndabamei, na kuungana na akina Marijani Rajab, Cosmas Tobias Chidumule, Ally Rajabu, Kakere Belesa, Joseph Mulenga ‘King Spoiler’ na Abel Balthazar.

Wengine ni akina Abdallah Gama, Haruna Lwari, Machaku Salum, Ibrahim Mwinchande na Betto Julius.

Miongoni mwa vibao vya bendi hiyo vinavyokumbukwa ni ‘Rufaa ya Kifo’ (Chidumule), ‘Nyerere Baba Mlezi’, ‘Mwana Rudi Wee’ (Mulenga), ‘Margret Msikilize Shangazi’ (Kakere) na ‘Sikitiko’ uliotungwa na Marijani.

Hata hivyo, bendi hiyo ilidumu kwa miezi miwili tu, ikafa baada ya kutoelewana kati ya mmiliki na wanamuziki.

Takriban wanamuziki wote, isipokuwa Marijani, wakaondoka na kwenda kuanzisha bendi ya Mlimani Park Orchestra chini ya umiliki wa Tanzania Transport & Taxis Services (TTTS).

Wanamuziki wengine waliojiunga na Mlimani Park ni Muhidini Maalim Gurumo, Hassan Bitchuka, Hassan Juma ‘Town’, Suleiman Mwanyiro ‘Computer’ na Abdallah Omar ‘Dullah’ wakitokea Juwata Jazz Band.

Pamoja na maisha magumu, hasa mazingira mabaya aliyoishi mwishoni mwa maisha yake, kabla ya kifo chake, King Enock, alitoa shukrani kwa Watanzania akisema:

“Kwa kuwa niliondoka Zambia zaidi ya miaka 42 iliyopita na sijarudi tena. Wazazi wangu walifariki dunia nikiwa shule ya msingi na ndugu zangu kila mmoja yuko kivyake.

“Ninawashukuru nyote, aidha ninaishukuru sana bendi yangu ya Sikinde kwa kunithamini mpaka hii leo.

“Sasa wenzetu wanaoinukia ndio watanufaika na matunda ya jasho lao; wao wanarekodi na kuuza kanda, lakini sisi tulitunga nyimbo na kuzipeleka RTD ambako hazikurekodiwa na kusambazwa kibiashara, bali zilikitumika kuburudisha katika vipindi mbalimbali.”

King Enock amewafundisha muziki vijana wengi ambao hivi sasa ni wanamuziki wa kutegemewa katika bendi mbalimbali nchini.

Maisha aliyoishi King Enock hayakulingana na mema aliyoyafanya katika maendeleo ya tasnia hiyo. Alidumu Sikinde tangu mwaka 1978 hadi alipofariki dunia mwaka 2004.

King Enock alipatwa na kiharusi mwaka 1989 na kuendelea kuhudumiwa na Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC) kwa matibabu na mshahara.

Mwandishi anapatikana kwa namba: 0784331200, 0736331200, 0767331200 na 0713331200.

By Jamhuri