Na Angalieni Mpendu

Historia inatueleza kuwa Kiswahili ni lugha
kongwe miongoni mwa lugha mama nyingi
zilizopo hapa nchini. Ni lugha adhimu,
nadhifu na ni titi lisilokwisha hamu. Lakini
baadhi ya Watanzania wanakibananga
katika utumizi wake. Iwe katika msingi wa
ujeuri, ujinga au dharau.
Lugha ya Kiswahili imetusaidia Watanzania
kuelewana, kushikamana na kuwa wamoja
kutoka taifa la kunyanyaswa, kuonewa na
kutawaliwa hadi kuwa taifa huru lenye
heshima, amani na usalama. Hii ndiyo faida
moja wapo ya Kiswahili.
Kiswahili kimetuwezesha kupanga mipango
mkakati ya ukombozi wa fikira na mawazo
yetu, ukombozi wa utu wetu na ukombozi
wa nchi yetu hadi kuwa taifa huru na tulivu.
Leo Watanzania tunatembea kifua mbele,

macho mita mia moja kuona maadui
kutokana na uelewano wetu katika kutumia
Kiswahili.
Nathubutu kusema Kiswahili ni pambo
mithili ya pete ya madini yenye thamani
kubwa iliyovaliwa kidoleni. Tanzania na
Kiswahili ni chanda na pete. Ni pete ya
thamani, haipatikani dukani, sokoni wala
kichochoroni. Nahau hii itathibitika katika
maelezo yafuatayo.
Nanukuu: “Katika kuufikiria utumizi wa
Kiswahili hatuna budi kupata fasili ya
maneno; taifa, utamaduni, mawasiliano na
lugha, kwa kuwa hatuwezi kueleza utumizi
wa lugha yoyote ile bila ya kuhusisha na
mambo haya. Katika kufanya hivi inabidi
tufanye tahadhari katika kuzitazama fasili
hizo, kwani zinakusudiwa kusaidia
kuendeleza mjadala.” Mwisho wa kunukuu.
Nimenukuu maelezo haya ya hayati Profesa
Zacharia S. Mochiwa wa iliyokuwa Taasisi
ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), sasa ni
Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI)
ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa nia
ya kuweka zaidi msingi wa maelezo yangu
kuhusu utumizi na matamshi potevu ya

maneno ya Kiswahili.
Lugha yoyote hutokana na mchanganyiko
wa maneno ya lugha mbalimbali ambazo
hulelewa na hutunzwa na jamii inayotumia
lugha hiyo. Jamii inapoacha kulea, kutunza
na kukuza, lugha inapotea au inakufa.
Aidha, utumizi fyongo wa maneno na fasili,
huibabaisha jamii husika kupata lugha
fasihi, na hapa mawasiliano huenda
shaghalabaghala.
Tukumbuke Kiswahili chenye asili ya
Kibantu kimetumiwa na wenyeji kabla ya
wageni (yaani Waajemi, Waarabu, Wareno,
Wajerumani, Waingereza n.k.) kuingia
nchini kufanya biashara na utawala katika
maeneo ya Zanzibar, Bara na mwambao wa
pwani ya Afrika ya Mashariki.
Wageni hawa wa kutoka nchi za Arabuni,
Asia na Ulaya waliwasiliana na wenyeji wao
wakitumia Kiswahili. Msamiati wa Kiswahili
ukapata maneno kutoka lugha ya Kiajemi,
Kiarabu, Kireno, Kihindi, Kijerumani na
Kiingereza. Baadhi ya maneno hayo
tunayatumia katika mazungumzo yetu.
Kwa mfano neno ‘shule’ ni kutoka
Kijerumani; neno ‘meza’
,
‘nanasi’

na ‘muhogo’ ni kutoka Kireno. Neno ‘chai’
na ‘dobi’ ni kutoka Kihindi. Neno
‘mahakama’
,
‘ardhi’ na ‘rais’ ni kutoka

Kiarabu. Neno ‘tochi’ na ‘motokaa’ ni kutoka
Kiingereza n.k.
Kiswahili kiliwavutia sana wageni, kwa vile
lahaja ya Unguja mjini ilipendelewa na
wamisionari na watawala wa kikoloni katika
matumizi ya kila siku. Ikumbukwe pia
Zanzibar ndiyo ilikuwa makao makuu ya
biashara kwa Afrika ya Mashariki mwishoni
mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne
ya 20.
Umaarufu wa Kiswahili ulivuma, ulisambaa
na uliwika hata katika nchi za nje kutokana
na mvuto wa lahaja mbalimbali za Kiunguja,
Kipemba, Kimakunduchi, Kimrima, Kimvita,
Kiamu, Kingwana, Kingazija na nyinginezo.
Utamu wa Kiswahili ulipata radha zaidi pale
Waswahili walipobembea na nahau, fasili,
tenzi, mashairi na tungo mbalimbali
zilizoelezea thamani ya Kiswahili, ukarimu
wa wenyeji, utu wao na uchapa kazi wao.
Mswahili mwenzangu, unasemaje kwa
maelezo haya machache? Usikose
kufuatilia makala hii wiki ijayo.

Mwisho

By Jamhuri