Wizara ya Maliasili yatajwa kuwa mtego kwa Kikwete

Pinda, Mwamunyange, Mwema watakiwa kupima uzito

Rais Jakaya Kikwete, akiwa anatarajiwa kulisuka upya Baraza la Mawaziri, kuna kila dalili kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sasa ndio imebaki kuwa kitanzi kinachotishia uhai wa Serikali yake.

 

Wakati mwaka 2011 Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa inaongoza kwa kupigiwa kelele, baada ya wizara hiyo kushikwa na Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi, sasa imetulia ila Maliasili ni tatizo.

 

Ukubwa wa tatizo la Wizara ya Maliasili unadhihirishwa na idadi kubwa ya mawaziri walioachia ngazi katika wizara hiyo, watendaji walioondolewa na jinsi wafanyabiashara wanavyoikodolea macho.

 

Kwa upande mwingine, wakati ikionekana wizara hiyo kuwa ni ngumu, Naibu Waziri mmoja amewaita wadau wake, wakiwamo wana habari kwa lengo la kuanza mpango wa ‘kumsema na kumwandika vizuri’ ili kumwezesha kuwa waziri kamili.


Naibu Waziri huyo kijana alikutana na wadau hao mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Habari zilizovuja zinasema kuanzia leo kutakuwa na habari na makala nyingi kwenye vyombo vya habari vikimpamba mwanasiasa huyo kijana kwa lengo la kumwaminisha Rais pamoja na umma kuwa anafaa kushika wadhifa mkubwa zaidi ya ule alionao sasa.


Kwa muda mrefu kumekuwapo na mvutano wa chini chini kati ya Naibu huyo na waziri wake ambaye ni miongoni mwa walioondolewa madarakani wiki iliyopita. Naibu Waziri alifikisha malalamiko hayo Ikulu akidai kwamba waziri alikuwa hampangii kazi zenye ‘tija’ za kumfanya ang’ae kiuongozi.


Wakati hayo yakiendelea, kujiuzulu kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kunatajwa kama uthibitisho mwingine wa ugumu wa wizara hiyo.

Wakati miaka yote ikitambulika kuwa wizara hiyo ni kitanzi cha mawaziri na watumishi wengine wasio kuwa na ujasiri wa kukwepa vishawishi vya fedha, safari hii imeonekana majangili ndiyo waliopata ushindi.


Mara kadhaa watu matajiri wenye maslahi binafsi ndani ya wizara hiyo wamekuwa tayari kuhakikisha wanawang’oa viongozi wasiokuwa tayari kushirikiana nao.

Katika kipindi cha miaka minane ya Serikali ya Awamu ya Nne, Wizara hiyo imeongozwa na mawaziri watano, na wa sita akiwa anasubiriwa. Alianza Anthony Diallo, Profesa Jumanne Magembe, Shamsa Mwangunga, Ezekiel Maige, na Balozi Khamis Kagasheki, aliyejiuzulu wiki iliyopita.


Tangu mwaka 2005 makatibu wakuu waliopitia wizara hiyo ni Salehe Pamba, Blandina Nyoni, Dk. Ladslaus Komba, na Maimuna Tarishi ambaye ‘amekalia kuti kavu’. Tarishi ametajwa kwenye ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, kama mmoja wa viongozi waliotia dosari kwenye Operesheni Tokomeza.


Ugumu wa Wizara hiyo unathibitika pia kwenye idadi ya Wakurugenzi wa Idara ya Wanyamapori; sehemu ambayo inatajwa kuwa ni ‘nono’ mno.

Tangu mwaka 2005 Rais Kikwete alipoingia madarakani, Idara hiyo imeongozwa na Emmanuel Severe, Erasmus Tarimo, Obeid Mbangwa, na sasa kuna Profesa Alexander Songorwa. Profesa huyu naye ametajwa kwenye ripoti ya Kamati ya Bunge, na kuendelea kwake kuwapo kwenye wadhifa huo kunatokana na majaliwa ya Rais.


Idadi kubwa ya Wakurugenzi wa Idara ya Wanyamapori imekuwa ikiondoka kwenye wadhifa huo kutokana na misukosuko mingi ya kiutendaji. Itakumbukwa kuwa Severe aliingia kwenye malumbano makubwa na Waziri Diallo; akipinga kuwa waziri hakuwa na mamlaka kisheria ya kumwondoa madarakani.


Februari 11, mwaka jana Rais Kikwete alitengua madaraka ya Mkurugenzi wa Wanyamapori, Tarimo na kumpatia likizo akisubiri kustaafu.

Kwa mujibu wa kifungu 8(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii aliteua Mbangwa kuwa Mkurugenzi wa Idara hiyo.


Hata hivyo, Mbangwa hakudumu kwenye nafasi hiyo kwa muda mrefu kwani baadaye aliachishwa kazi kutokana na kashfa ya usafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi, wakati huo akiwa mwenye dhamana na kitengo kilichohusu masuala hayo.

Pinda, viongozi wa ulinzi na usalama wang’ang’aniwa

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, bado yuko kwenye wakati mgumu baada ya jaribio la kumtaka ang’oke kwenye wadhifa huo kwa ridhaa yake kugonga mwamba wiki iliyopita.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Bunge), William Lukuvi, anatajwa kuwa kiongozi aliyeshiriki kwa kila hali kumwokoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwenye hatari ya kuondolewa madarakani.


Habari zilizopatikana kutoka Dodoma zilisema Lukuvi alihakikisha anapita kwa wabunge kadhaa na kuzungumza nao ana kwa ana akiwahimiza wafanye kila linalowezekana ili Waziri Mkuu abaki madarakani.


Badala yake akawasihi wabunge kama wanataka kuiwajibisha Serikali, basi wahakikishe wanaoondolewa ni hao mawaziri waliotuhumiwa kwenye ripoti ya Kamati ya Bunge.

Hayo yakiendelea, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliugua ghafla kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kutokana na mshituko alioupata wa kupoteza nafasi yake.


Kwa nafasi yake, Lukuvi alifanya hivyo kama sehemu ya kutimiza wajibu wake, lakini pia inaelezwa kuwa hatua hiyo ilitokana na ukweli kwamba endapo Waziri Mkuu angejiuzulu, hiyo ina maana mawaziri wote wangepoteza nafasi zao.


Pinda alinusurika baada ya kuwasilisha taarifa mbele ya wabunge waliokuwa na ‘hasira’ akisema Rais Kikwete alikuwa ameshaamua kutengua uteuzi wa mawaziri wanne-Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha; na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo.


Ingawa taarifa hiyo ilipokewa kwa shangwe na wabunge, habari zilizopatikana zinasema bado wamemkamia. Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), kama wabunge wengine, alimtaka Waziri Mkuu ajizulu; lakini yeye alienda mbali zaidi kwa kuanza kusambaza karatasi bungeni kwa lengo la kuwashawishi wabunge watie saini kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge ili hatimaye utaratibu wa kumng’oa Pinda ufanikishwe.


Uamuzi huo ulionekana kuungwa mkono na wabunge wa pande zote bila kujali tofauti zao kiitikadi. Watu walio karibu na Machali wanasema mbunge huyo bado msimamo wake ni wa kuhakikisha Pinda anang’oka hata kama ni kwenye mkutano ujao wa Bunge.


Hoja ya wabunge wengi ni kwamba Pinda amekuwa dhaifu mno kiuongozi, na kwamba kuwaadhibu mawaziri pekee hakutoshi kwa sababu yeye ndiye msimamizi wa shughuli za Serikali za kila siku-ndani na nje ya Bunge.


Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wabunge na wananchi wa kawaida wanahoji uhalali wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kushika nyadhifa zao ilhali mawaziri wakiwa wamejiuzulu.


Waliozungumza na JAMHURI wamejikita kwenye hoja ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ambaye alirejea hadi ilivyokuwa miaka zaidi ya 40 iliyopita ambako Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, na aliyekuwa Waziri mwenye dhamana na Usalama wa Taifa, Peter Siyovelwa; walijiuzulu baada ya kutokea kwa mauaji ya mahabusu mkoani Shinyanga. Pamoja nao, wengine waliojizulu ni aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Philemon Mgaya.


Kwa hoja hiyo, wanawataka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema; Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange; na Mkuu wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman; na Waziri mwenye dhamana ya Usalama wa Taifa, George Mkuchika; wajiuzulu.

Hata hivyo, kujizulu kwa viongozi hao wote huenda kukawa si jambo rahisi kutokana na kuwapo taarifa za kukang’anya zinazohusu ripoti ya Bunge iliyochunguza Operesheni Tokomeza.

Habari ambazo Serikali haijazikanusha wala kuzithibitisha zinasema baadhi ya vyombo vya dola viko mbioni kuanza kuchunguza yale yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ili kupata ukweli kuwapo mauaji na mateso kwa raia yaliyovuka mipaka ya utu.

Aidha, kujiuzulu huko kunaweza kuwa ni changamoto nyingine ngumu kwa baadhi ya viongozi hao wakuu kwa kuwa kuna taarifa kwamba Amiri Jeshi Mkuu amewaongeza muda wa kuwapo kwao madarakani licha ya kutakiwa kustaafu kisheria ili ikiwezekana waondoke wote baada ya kumalizika kwa uongozi wa Awamu ya Nne.

Mawaziri mizigo waibua changamoto

Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliwaita na kuwahoji baadhi ya mawaziri saba waliopewa jina la ‘mawaziri mizigo’. Uamuzi wa kuwaondoa mawaziri hao uliachwa mikononi mwa Rais Kikwete.


Miongoni mwa mawaziri waliohojiwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya; na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.


Kwa upande wake, Bunge lilipitisha azimio la kumtaka Ghasia na naibu wake wawili -Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa- kupima na kutafakari kama wanatosha kusimamia wizara hiyo.

Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Bunge ya Hesabu za Serikali kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani ya Tamisemi, kwenye halmashauri na Hazina.

Kikwete hajatatua tatizo

Wasomi na wananchi mbalimbali mbalimbali wamekosoa uamuzi wa kuwang’oa madarakani mawaziri wanne wakisema hatua hiyo haitatatua tatizo lililopo ikiwa ataendelea kumkumbatia Waziri Mkuu Pinda.


Waziri Mkuu alitangaza bungeni uamuzi huo wa Rais Kikwete aliyekwenda nchini Marekani kuangaliwa afya yake, baada ya wabunge kupigilia msumari taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyobainisha vitendo vya unyanyasaji na dhuluma dhidi ya wananchi vilivyojitokeza wakati wa Operesheni Tokomeza.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wasomi kadhaa wamesema Rais Kikwete anapaswa kufanya uamuzi mgumu wa kumng’oa Pinda ili afuate nyayo za mawaziri hao kwa kuwa ameshindwa kuwasimamia mawaziri.

Profesa Humphrey Moshi

Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, amesema wizara zote zinafanya kazi bila ya kuwa na mawasiliano ya kiutendaji, kinachotakiwa ni kuhakikisha kila wizara inakuwa na kamati ndogo itakayoshughulikia mawasiliano kati ya wizara moja na nyingine kuliko ilivyo sasa.


“Mimi sioni sababu ya wafugaji na wakulima kupigana na kuuana wakati kuna wizara na zina mawaziri, kuna Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kuna Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, sasa kinashindikana nini kuwasiliana ili kutatua tatizo hilo,” amehoji Profesa Moshi.

Amesema iwapo mawaziri hao watakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara watajua nini cha kufanya kati yao na kupunguza au kumaliza kabisa matatizo hayo kwani Tanzania bado ina nafasi kubwa kwa malisho ya mifugo.


Amesema wizara nyingi zinafanya kazi kwa usiri bila kuwashirikisha wizara nyingine, hivyo kushindwa kujua suala linaloshughulikiwa linaweza kuathiri wizara nyingine kiutendaji kama ilivyotokea katika Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Mazingira na Maliasili.


Akizungumzia mgongano wa majukumu kati ya waziri na makatibu wakuu wa wizara, Profesa Moshi amesema jambo hilo limekuwa likisumbua kila idara ya Serikali kutokana na mfumo wa ajira ilivyo hapa Tanzania .


“Kwa bahati nzuri mie nilikuwa mjumbe katika kamati ya kutengeneza Dira ya Maendeleo ya Taifa, jambo hili nililiona tukalizumgumzia tukapendekeza nafasi zote za kuteuliwa zifutwe na watu waombe kwa kuandika maombi na kufanyiwa usaili na wakipita katika usaili wapate kazi, lakini wajue wanawajibika kwa waziri huska kuliko ilivyo sasa, kila mtu ni mteule wa Rais, hii ni hatari katika uwajibikaji,” amesema.


Amesema haiwezekani kuanzia Mkurugenzi wa Wilaya hadi Katibu Mkuu wa Wizara awe mteule wa Rais, hatua hiyo inaleta matatizo katika utendaji wa mwaziri kwani wanashindwa kuwawajibisha watendaji hao kwa kuwa siyo waliowapa kazi bali ni Rais.


Kuhusu cheo cha uwaziri, amesema utamaduni wa Rias kuchangua mwaziri kutoka katika Bunge nao ni tatizo kwani si wabunge wote wana uwezo wa kuongoza wizara.

Profesa Moshi amesema kuna watu wengi nje ya Bunge wenye uwezo wa kuongoza wizara hizo na kumsaidia Rais kuleta maendeleo tofauti na watu walio ndani ya Bunge.


Ametoa wito kwa Rais kutumia nafasi kumi alizopewa kikatiba kuteua wabunge wengine wenye uwezo mkubwa ili kushika nafasi za uwaziri katika uteuzi ujao wa Baraza la Mwaziri.

Amesema hata hivyo, Serikali inatakiwa kuangalia upya sheria ya mazingira kwani kutofanya hivyo kutazidisha migogoro ya ardhi kila kukicha.


Profesa Moshi amesema sheria hiyo isiishie kutungwa na kukaa kabatini bali elimu kuhusu sheria hiyo itolewe kwa wakulima na wafugaji kuhusu mipaka ya hifadhi na vijiji.

Amesema wafugaji wanatakiwa kuelimishwa kuwa kufuga mifugo inayoendana na ukubwa waeneo la malisho na kuwa ufugaji wa mifugo mingi isiyoendana na eneo analofugia hakuna tija kwake na kwa taifa.

Profesa Mwesiga Baregu

Kwa upande wake, Profesa Mwesiga Baregu amesema tatizo lililopo ni mfumo wa ajira ndani ya Serikali. Kwamba mfumo uliyopo umeshidwa kufanya kazi kwa kuwa hauko wazi.

Amesema watendaji wengi katika wizara wanashindwa kuelewa mipaka ya kazi yao , wanashindwa kuafikiana katika uamuzi na baadaye wanaanza kurushina vijembe.


“Mfumo unawapa kiburi kwa kuwa wote ni wateule wa Rais, hakuna mtu wa kumfukuza kazi mwenzie kwa kuwa mwenye uwezo ni Rais pekee, hapa tunatakiwa kurekebisha mfumo ili kila mtu ajue anawajibika kwa nani, bila kufanya hivyo hata wakiteuliwa wengine hakuna mtu atakayepona,” amesema Profesa Baregu.


Amesema pamoja na ubabe wa makatibu wakuu, hata waziri wengi hawajui majukumu yao ya kazi.

 

Ametoa mfano kuwa mawaziri wengi wanaingilia kazi za wakurugenzi au mameneja wa taasisi na kwamba utakuta waziri anaeleza mikakati ya taasisi wakati yeye anatakiwa kutoa maagizo na kusubiri utekelezaji.


Amesema kuwa iwapo utekelezaji utakuwa sifuri anachotakiwa kufanya ni kuchukua hatua zinazostahili na kama hazitatekelezwa anatakiwa kutoa taarifa kwa Wazari Mkuu na kupendekeza hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya mameneja au wakurugenzi, lakini hilo halifanyiki.


Akizungumzia ugumu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,  Profesa Baregu amesema wizara hiyo imekuwa na matatizo tangu zamani.

Amesema taarifa iliyosomwa na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira haijaeleza ni kwa kiasi gani matatizo yako katika wizara hiyo.


“Sehemu ya taarifa ya Kamati ya Lembeli inatuambia sehemu tu ya matatizo, lakini yako mengi mno, haikuangalia ni kiasi gani wanyama wamepotea, na hata Serikali imekuwa makini kwa kiasi gani katika operesheni hiyo ili kutafuta suluhisho la kumaliza tatizo la kumaliza wanyama wetu,” amesema Profesa Baregu.


Amesema wizara hiyo imekuwa na matatizo kwa muda mrefu, hususan katika taasisi zake kwani bado kuna matatizo makubwa ya kiutendaji.

Deo Filikunjombe anena

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amesema tatizo siyo mfumo wa utawala bali ni utendaji mbovu unaotokana na viongozi kulewa madaraka baada ya kuteuliwa na kujikuta wakisubiri kila kitu kuletewa mezani badala ya kufika katika maeneo ya kazi ilihali mengine wanadanganywa.


“Unajua ni aibu kubwa kufukuzwa kazi katika screen [runinga] watu wote wanaona, wakwe zako, mkeo, watoto, kama mimi sikubali kwa hili jambo ni kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo,” amesema Filikunjombe.


Amesema mawaziri wengi wamekuwa wakilalamika kuwa utendaji wao wakazi unaharibiwa na makatibu wao jambo hilo sio kweli kwani wapo mawaziri wanowakataa makatibu mizigo na wanabadilishiwa.


“Nimeona mfano kwa Magufuli akisema huyu katibu simtaki ni mzigo kweli anabadilishiwa yuko tayari kuachia uwaziri kuliko kufanya kazi na katibu mzigo au mkorofi, niliwahi kushuhudia akikataa kufanya kazi katika moja ya barabara hapa nchini kutokana na bajeti ndogo, lakini baadaye aliongezewa, tatizo la wengine wana nidhamu ya woga, wanalalamikia chini chini, ” amesema.


Amesema kama sheria hiyo ni mbovu wanayo nafasi ya kukaa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuona jinsi gani wanaweza kuibadilisha na kuleta bungeni.

Amesema sakata lilowapata mawaziri Kagasheki na Dk. Mathayo; limetokana na kuponzwa na Dk. Nchimbi na Nahodha.


“Hapa tatizo siyo Kagasheki, najua kuwa ni mchapakazi sana , tatizo ni Emmanuel Nchimbi na Nahodha ambao hawakujua vijana wao wanafanya nini katika operesheni hiyo na sisi kazi yetu si wanyama, watu kwanza wanyama baadaye, najua kuwa tunawapenda wanyama, lakini watu zaidi,” amesisitiza.

Machali amng’ang’ania Pinda

Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), amesisitiza kwamba Pinda hana ‘ubavu’ wa kuhimili wadhifa huo, ndiyo sababu baadhi ya mawaziri wamebweteka na kuacha mambo yanayohusu maendeleo ya wananchi kuyumba.


“Mpaka leo sina imani na Waziri Mkuu kwa sababu hajali matatizo ya wananchi. Kushindwa kwa mawaziri ni matokeo ya Waziri Mkuu kushindwa kusimamia mawaziri watekeleze majukumu yao vizuri.


“Kuwawajibisha mawaziri hawa wanne hakutoshi, hapa Rais kikwete hajatatua tatizo. Tatizo ni Pinda, katika hili Serikali imepoteza uhalali,” amesema Machali. Mbunge huyo ameendelea kumtuhumu Waziri Mkuu huyo akisema amefumbia macho tatizo la kunyanyaswa kwa wakazi wa eneo la Kageramkanda, Kasulu Mjini wanaodaiwa na Serikali kuwa wamevamia hifadhi ya msitu licha ya kuishi hapo kwa zaidi ya miaka 30 sasa.

 

Hata hivyo, kwa upande mwingine, Machali amesema kuna mazingira ya uonevu kwa baadhi ya mawaziri waliotenguliwa.


“Yapo mazingira ya kuonewa kwa baadhi ya mawaziri hawa [waliong’olewa]. Mfano, kuna taarifa kwamba Katibu Mkuu na watendaji wengine wakuu katika Wizara ya Maliasili na Utalii wamekuwa wakimpuuza Kagasheki kwa sababu hana mamlaka ya kuwafukuza kazi,” amesema.


Kuhusu azma yake aliyoitangaza bungeni ya kukusanya sahihi za wabunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Machali amesema shughuli hiyo inakwenda kwa kuzorota kwani hadi mwishoni mwa wiki alikuwa amepata sahihi 26 za wabunge kutoka vyama vya siasa vya upinzani pekee.

 

“Ninaendelea kuwashawishi wabunge wakubali tumng’oe Pinda. Ninajua mchakato huu ni mgumu, wabunge wa CCM wataukwamisha, lakini lazima tuendelee kupiga kelele. Mabadiliko hayawezi kuja mara moja [haraka], lazima tupige kelele,” amesema.

Shibuda azungumza

Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), amewatuhumu makatibu wakuu wa wizara kwamba wengi wao ni kikwazo cha maendeleo ya Watanzania.

“Makatibu wakuu wa wizara ni tatizo, ni miungu-watu, wengi wao na baadhi ya mawaziri wamekuwa makuadi, wazandiki na mawakala wa utandawazi,” amesema Shibuda bila kufafanua zaidi.

Amesema kitendo cha kuwang’oa mawaziri na kuwaacha makatibu wakuu wa wizara hizo ni sawa na kutibu ugonjwa wa malaria huku ukiendelea kulea mazalia ya mbu.

Itutu wa ADC anena

Kamishna wa Alliance for Democratic Change (ADC) Kanda ya Ziwa, Shaban Itutu, amepongeza uamuzi wa Rais Kikwete wa kuwavua madaraka mawaziri hao, lakini amesema kuna haja ya kuendeleza ufagio huo wa chuma kwa viongozi watendaji wengine wa Serikali wanaotumia vibaya madaraka yao .

“Rais asiishie kwenye wizara hizi nne pakee kwa sababu karibu wizara zote kuna ‘majanga’. Watendaji wabovu wote wawajibishwe, na tume maalum iundwe kuchunguza utendaji wa watumishi katika wizara zote,” amesema Itutu.

Itutu ameitupia lawama pia Idara ya Usalama wa Taifa akisema imedhihirisha udhaifu wake kwa kushindwa kufichua na kuzuia vitendo viovu vilivyotekelezwa wakati wa Operesheni Tokomeza kabla ya Kamati ya Lembeli kuvibaini.

James Bwire wa CCM

Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Mahina jijini Mwanza, James Bwire, amesema kutenguliwa kwa mawaziri hao ni fundisho na onyo kwa mawaziri wengine wanaojisahau kusimamia vizuri dhamana za kuwatumikia wananchi.

“ Hilo ni fundisho kwa mawaziri waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi lakini wakajisahau na kutoa mwanya wa matatizo katika wizara zao,’ amesema Bwire.

Akizungumzia hoja ya kumwajibisha Waziri Mkuu, Bwire amesema hoja hiyo haipaswi kushikiwa ‘bango’ kwa kuwa licha ya ukweli kwamba ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali, kiongozi huyo hana mamlaka ya kuamua chochote pasipo baraka za Rais na Makamu wa Rais.

“Waziri Mkuu amebanwa jamani, huyu ni tofauti na Lowassa [Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani] ambaye alikuwa jasiri wa kufanya uamuzi mgumu,” amesema.

Augustino Sasi

Diwani wa zamani wa Kata ya Kemambo, Tarime mkoani Mara, Augustino Sasi (CHADEMA), yeye ametafsiri utenguaji huo wa mawaziri kama kitendo cha CCM kujiandalia mazingira mazuri kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

 

1272 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!