*Alisahau viatu vyake vya kijeshi Tanzania, akafungwa

*Mufti Simba, Askofu Kilaini, Ruwa’ichi watoa tamko

*Profesa Baregu, Wangwe, Safari, Kiwanuka wanena

 

Kifo cha Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela “Madiba”, kimefichua siri nzito kuhusu harakati zake za ukombozi wa taifa hilo kutoka katika makucha ya serikali ya kibaguzi ya Wazungu.

Watu maarufu wakiwamo viongozi wa dini na wastaafu serikalini, wametoboa siri kwamba pamoja na sifa nyingine, Mandela ndiye mtu pekee duniani aliyetumia karibu maisha yake yote huku akiwa tayari kufa kwa ajili ya kupigania haki za wanyonge katika taifa lake.

 

Baadhi wamesema Mandela ni zawadi iliyotolewa na Mwenyezi Mungu kwa Afrika Kusini kama si duniani, na wengine wanamtazama kama kiongozi ambaye hakuwa na chembe ya tamaa ya kung’ang’ania madarakani.

 

Katika mazungumzo na JAMHURI kwa nyakati tofauti, viongozi mbalimbali wamekiri kuwa Mandela alikuwa kiongozi wa aina yake, ambaye ushujaa na uadilifu wake haulinganishwi na mwingine yeyote duniani.

 

Balozi Kiwanuka atoboa siri

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Balozi Ahmed Kiwanuka, amesema pamoja na mambo mengine, anamkumbuka Mandela kutokana na tukio la kiongozi huyo wa Afrika Kusini, kusahau viatu vyake vya kijeshi hapa Tanzania.

 

“Nakumbuka mwaka 1962 Mandela alipita hapa Tanzania, alimuaga Mwalimu (Rais Mwalimu Julius Nyerere), lakini akasahau viatu vyake vya kijeshi kwa Waziri Nsilo Swai,” amesema.

 

Viatu hivi alikuwa amevipata nchini Ethiopia alikokwenda kwa mafunzo ya kijeshi, baada ya Mwalimu Nyerere awali kuwa amempatia hati ya kusafiria ya Tanzania kwenda Ethiopia, lakini alipofika nyumbani alikoitwa kwenda kuokoa jahazi akafungwa miaka mitano kwa kosa la kwenda nje ya nchi bila kibali.

 

Kwa upande mwingine, Balozi Kiwanuka amesema anamfahamu Mandela kama kiongozi wa mapambano ya kutafuta uhuru, aliyekuwa na imani thabiti, mwadilifu, aliyewezesha mabadiliko makubwa ya kidemokrasia Afrika Kusini, na aliyekuwa tayari kufa kwa ajili ya kutetea maslahi ya wengi.

 

“Viongozi wa Afrika wamuenzi Mandela, wajifunze kutokana na maisha yake. Mandela ataendelea kuheshimiwa na kukumbukwa duniani, na ushahidi wa hilo ni jinsi dunia nzima inavyomlilia kwa sasa,” amesema Balozi Kiwanuka.

 

Mufti Simba anena

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, amemuelezea Mandela kuwa ni kiongozi pekee duniani ambaye hakufaidi maisha ya ujana wake, kutokana na kutumikia kifungo cha miaka 27 gerezani wakati wa Serikali ya kimabavu ya Wazungu.

 

Amesema Mandela ni mwanaharakati na mkombozi aliyejitolea maisha yake yote kupigania uhuru na haki za Waafrika wenzake ndani na nje ya Afrika Kusini.

 

“Sisi tunamshukuru Mungu kwa kutuletea tunu hiyo [Mandela], ni kiongozi wa kupigiwa mfano duniani,” amesema Mufti Simba na kuendelea:

 

“Alipotoka jela alijenga misingi ya maelewano kati ya watu weusi [Waafrika] na watu weupe [Wazungu], ndiyo maana hata Wazungu wanamlilia sana, na ninamwomba Mungu atupatie Mandela mwingine.”

 

Askofu Kilaini: Mandela hakutaka urais

Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini, amesema nia ya Mandela hasa haikuwa kutafuta urais bali uhuru wa wazalendo wa Afrika Kusini.

 

“Mandela alipoachiwa huru baada ya kifungo cha miaka 27 jela, hakulipiza kisasi bali aliwahamasisha Waafrika wenzake kushirikiana na waliomnyanyasa [Wazungu] kulijenga taifa katika misingi ya umoja,” ameeleza Askofu Kilaini.

 

Ameongeza kuwa Mandela alikuwa kiongozi shupavu na mahiri, mwenye msimamo thabiti, asiyeyumbishwa katika harakati za kutetea haki za wanyonge.

 

“Ninamlinganisha Mandela na Nyerere [Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere] kwani ni mtu ambaye hakung’ang’ania madaraka hadi aondolewe kwa mtutu,” amesema.

 

Anaongeza, “Tunamshukuru Mungu kwa kutuletea Mandela kwani alikuwa kiongozi wa tofauti kabisa na hakuna anayefuata nyayo zake, hakuna kama Mandela.”

 

Askofu Ruwa’ichi: Mandela ni Mandela

Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Mwanza, Jude Thadeus Ruwa’ichi, amesema Nelson Mandela aliendelea kuwa mhimili kuwaunganisha Waafrika katika kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi hata baada ya kutoka jela.

 

“Mandela alikuwa kiongozi mwenye malengo makubwa na mazuri yaliyozingatia maslahi ya wengi, na aliyepigania kwa gharama yoyote ile. Aliamua mambo kwa haki, busara, huruma na msamaha,” amesema kiongozi huyo wa kiroho.

 

Amesema kitendo cha Mandela kuongoza kwa kipindi kimoja kama rais na kuachia wengine, kinamdhihirisha kuwa hakuwa mtu wa kung’ang’ania madaraka.

 

“Mandela aliongoza kipindi kimoja na kustaafu, si kwamba asingechaguliwa tena bali aliona kuna watu wengi wenye vipaji vya uongozi Afrika Kusini, akawaachia. Ni fundisho kwa viongozi wengine na zawadi kubwa kwa Afrika,” amesema.

 

Profesa Wangwe: Hakuna kama Mandela

“Ninamfahamu Mandela kama mpigania uhuru wa muda mrefu. Alipopata urais aliwasamehe waliomweka kifungoni, akahamasisha umoja nchini Afrika Kusini,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiri wa Kuondoa Umaskini (REPOA), Profesa Samwel Wangwe.

 

Profesa Wangwe ameongeza, “[Mandela] alikuwa mtu aliyejali maslahi ya watu. Kwa sasa hakuna kama Mandela.”


Profesa Safari amlilia Mandela

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallah Safari, amesema Mandela hakuwa mtawala bali kiongozi aliyefuata maadili ya uongozi.

 

“Huyo ni mjumbe wa mwisho kuondoka hapa duniani kati ya viongozi niliowahi kuwaona au kuwasikia kama akina Kwame Nkrumah wa Ghana, Mwalimu Nyerere, Ahmed Sékou Touré, (Guinea) na Sokoine. Hawa walikuwa viongozi siyo watawala,” amesema Profesa Safari.

 

Amesema Afrika imebaki kama mtoto yatima kutokana na kukosa viongozi wenye maadili mema, wanaojua kuongoza kama Mzee Madiba na wenzake waliotangulia mbele ya haki.

 

Mwanasiasa huyo amefafanua kuwa wengi wa waliobaki si viongozi bali watawala wasiojali maslahi ya wananchi, ambao wanatanguliza ubinafsi kuliko maslahi ya nchi.

 

Hata hivyo, Profesa Safari ameshangazwa na Marekani kumlilia Mandela na kumpamba kwa sifa nzuri, wakati miaka michache iliyopita ilikuwa ikimwita gaidi.


Attilio Tagalile azungumza

Mwandishi mkongwe wa habari nchini, Attilio Tagalile, amesema kama viongozi wote wangekuwa wa aina ya Mandela, machafuko na mapigano yanayogharimu maisha ya watu na mali yasingekuwa yanatokea katika mataifa mengi duniani.

 

“Mandela ni mfano mzuri wa kuigwa barani Afrika, hakung’ang’ania madaraka, alipopata urais aliongoza kwa kipindi kimoja, hiki ni kitu ambacho hakipo siku hizi.

 

“Kwa mfano, Wakenya waliuana kwa sababu ya baadhi ya viongozi kung’ang’ania madaraka,” amesema Tagalile.

 

Profesa Beregu: Mandela kama Nyerere

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, amesema Mandela alikuwa kiongozi wa kuzaliwa, si wa kuchonga.

 

Amewataja Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkrumah na Mandela kwamba walikuwa viongozi wenye upeo wa juu katika uongozi, waliojali maisha ya watu wao kuliko nafsi zao.

 

“Viongozi hawa kila walipokuwa wakilala walikuwa na mawazo ya nini watawafanyia wananchi wao ili kuwatoa katika umaskini na si kwa ajili ya familia zao,” amesema Profesa Baregu.

 

Amesema kuwa viongozi wa Afrika wana changamoto ya kuhakikisha wanaiga uadilifu na ushujaa wa Mandela katika kuutumikia umma.


Bashe: Mandela shujaa wa dunia

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe, amemwelezea Mandela kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa alikuwa shujaa wa kweli wa Afrika na dunia kwa jumla.

 

Kwamba Mandela alikuwa kiongozi ambaye kamwe hakujifikiria maslahi yake binafsi bali ya wazalendo wote wa Afrika Kusini, na kwamba alikuwa balozi wa kweli wa Bara la Afrika.

 

Kwa upande mwingine, Bashe amesema Mandela pamoja na mema mengine, atakumbukwa kutokana na kuipatia Afrika heshima ya pekee kwa kuwezesha mazingira yaliyoruhusu mashindano ya Kombe la Dunia kufanyika kwa mara ya kwanza barabi Afrika nchini Afrika Kusini.

 

Hata hivyo, Bashe alieleza wasiwasi wake kwamba huenda hatapatikana kiongozi mwingine duniani wa aina ya Nelson Mandela.

 

Mandela alifariki dunia usiku wa Desemba 5, 2013 ambapo mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kijijini kwake Qunu, kwenye mji wa Soweto.

By Jamhuri