*UN waanza kutumia ndege zisizo na rubani kusaka masalia

*Zinatambua aliko mwenye bunduki, zilitumika Afghanistan

 

Baada ya Brigade Maalum ya Umoja wa Mataifa ikiongozwa na Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwasambaratisha waasi wa M23 nchini DRC, Brigade hiyo imeanza kutumia ndege zisizokuwa na marubani (drones) kufanya ulinzi katika mji wa Goma, hali inayozidi kuwafukizia moshi waasi hao.

Ndege hizo kutoka Italia zilianza kuvinjari katika anga ya mji wa Goma ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokraia ya Congo Desemba 3, mwaka huu kuiimarisha usalama katika mpaka ya nchi hiyo.

 

Kwa mara ya kwanza ndege hizo zisizokuwa na rubani zinaafanya uchunguzi na kuimarisha hali ya utulivu katika eneo la Mashariki mwa DRC. Hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa imelenga kufuatilia na kutokomeza kabisa harakati za makundi ya uasi katika maeneo ya Kivu.

 

Aina hii ya ndege Marekani imepata kuzitumia nchini Afganistani kusaka Watalibani katika milima ya Tora Bora. Ndege hizi zina uwezo mkubwa wa kupiga bila kukosea maeneo yanayokuwa yamelengwa.

Zinatumia teknolojia ya “sensor” ambapo baada ya darubini kubaini tatizo liliko, basi wataalam hutuma ndege hizo zinazokwenda moja kwa moja na kuangamiza wahusika.

 

Kwa mtu yeyote aliyeshika bunduki au chuma cha aina yoyote, anakuwa kwenye hatari ya kusambuliwa na ndege hizi kwani zenyewe zimetengenezwa kubaini silaha na kuteketeza.

 

“Njia pekee inayoweza kuwasaidia waasi wa M23 na wengine walioko kwenye misitu ya mbali ni kukaa mbali na silaha kama bunduki, mizinga au magari ya kivita, maana ndege hizi zenyewe zinaingia kila pahala misituni na kokote.

 

“Uzuri wa ndege hizi hazitumii macho ya binadamu kutafuta alipo adui, badala yake inatumia ‘sensor’ ambayo ikibaini kuna mtu ana silaha inashusha kombora. Nadhani kwa hatua hii, njia pekee ya kujiokoa kwa waasi hao ni kutupa kila silaha waliyonayo wakakaa mbali na silaha.

 

“Kitendo cha kushika silaha mkononi, ndege hizi zinakutungua. Hii ina maana kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuwa msituni kwani watakuwa hawana silaha za kutumia kupambanana na mwisho wa siku njaa itawatoa tu,” alisema mtoa habari wetu.

 

Chanzo cha habari kutoka mjini Goma kimelieleza JAMHURI kuwa sasa hali ya mji huo ni shwari kutokana na waasi wa March 23  kuukimbia mji huo.

 

“Hapa kuko shwari kabisa tunakula bata tu. Waasi hawako tena baada ya kuwavurumisha, wananchi wanaishi kwa raha na furaha. Furaha yao huzidi tu wanapotuona au kusikia ni askari wa JWTZ wako mahali fulani.

 

“Kazi tuliyotumwa tumemaliza imebaki, kazi ya kuwafundisha Kiswahili. Wacongo kila wapotuona wanataka kujua Kiswahili tunapopata nafasi tunafundisha Kiswahili,” kimesema chanzo hicho.

 

Chanzo hicho kimesema kuwa pamoja na kuifanya kazi hiyo kwa muda mfupi na ufanisi kubwa lakini haikuwa rahisi kwani waasi hao walikuwa na vifaa vingi na vya kisasa kilichowashinda ni jinsi ya kuvitumia.

 

Kimeeleza kuwa  katika mapigano hayo, Jeshi la UN likiongozwa na Brigedia Jenerali Mtanzania James Mwakibolwa wa JWTZ kupitia Brigade Maalum ya SADC waliteka vifaru vitatu vya kisasa  na bunduki nyingi za makombora mazito aina ya Katyusha.

 

“Siwezi kusema mara moja kwa sasa kuwa tumekamata silaha ngapi au vifaru vingapi, bali ninachojua, na nina uhakika navyo  kwa kuwa niliviona ni kuwa tunashikilia vifaru vitatu vya kisasa na bunduki nyingi aina ya katyusha hizi ni zinafanana kama vile MB hawa jamaa walikuwa na vifaa vingi mno, lakini tuliwazidi ujanja,” kilisema chanzo hicho.

 

Baadhi ya waasi wa M23 hivi karibuni waliliambia JAMHURI kuwa hawana hamu na askari wa JWTZ kutokana na uwezo mkubwa wa kupigana vita waliouonyesha. Walisema askari wa JWTZ walipofika katika uwanja wa mapambano hali ilibadilika kwa kiasi kikubwa na kuwafanya wachapwe haraka kuliko matarajio yao.

 

Wamekuwa wakilisifia Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa maelezo kuwa nguvu na weledi waliouonyesha katika medani za vita umewafanya waone maisha yao yapo hatarini. Waasi zaidi ya 1500 wamekimbilia nchini Uganda, huku wengine 800 wakikimbilia nchini Rwanda, nchi zinazotuhumiwa kuwa zilikuwa zinawaunga mkono.

 

Hadi mwishoni mwa wiki, ilielezwa kuwa waasi wapatao 2000 walikuwa wamejisalimisha mbele ya Serikali ya Rais Joseph Kabila wakitafuta kuingizwa jeshini na wameapa kuachana na vita baada ya kipigo walichokishuhudia kwa M23 waliofurushwa mwishoni mwa Oktoba, 2013.

 

By Jamhuri