Chama cha Jahazi Asilia kimesema mtindo unaotumiwa na vyama vya CCM na CUF kubeba wanachama kwenda na kurudi kwenye mikutano ya hadhara hauvikisaidii vyama hivyo kujitambua na kupima kisiasa kama vinakubalika au la.

Hayo yamewekwa bayana na Mwenyekiti wa Jahazi Asilia, Amour Bamba katika mahojiano na JAMHURI yaliofanyika hivi karibuni mjini Unguja.

 

Bamba amesema inashangaza kuona vyama hivyo vikitumia nguvu nyingi kubeba wanachama wake kwa kutumia magari na kwenda nao mikoa ya Mjini, Kusini na Kaskazini Pemba na Unguja  vikiamini kuwa huko ni kukubalika kwao kisiasa. Alisema kitendo hicho hakionyeshi kipimo halisi cha kukubalika kwao kwa wananchi  na badala yake vyama vyote viwili vinajidanyanya kisiasa na kuhatarisha maisha ya wanachama wao kutokana na uwezekano wa kutokea ajali wanapokwenda au kurejea kutoka katika mikutano hiyo.

 

“Wanajihadaa na siasa za fahari ya macho, hawapati vipimo halisi vya kukubalika. Wanajivunia nguvu za fedha kwa kukodi magari, kubeba wafuasi ili wakajaze mikutano yao kinadharia na si kuhalisia,” amesema Bamba.

 

Alisema kisingi vyama vya CCM na CUF kila kimoja kinakubalika upande mmoja wa visiwa vya Unguja na Pemba hivyo ni vigumu vyama hivyo kujitambua kama vina ongezeko la idadi ya wanachama wake au vinapungukiwa kwa utaratibu wanaoutumia.

 

“Kura za CCM na CUF ni zile zile. CUF wanatanga na njia Unguja zikipigiwa kura na watu kutoka Pemba wanaoishi Unguja na CCM huko Pemba kikipata kura za watu wenye asili ya Unguja waliohamia Pemba,” anafafanua Bamba kwa tathmini ya kihistoria na uchambuzi wa  kisiasa.

 

Anaeleza kuwa mgombea yeyote atakaesimamishwa na CCM akiwa na asili ya Pemba hatapigiwa kura nyingi na watu wa Unguja wakati mgombea wa CUF ataendelea kupata kura nyingi za Pemba na watu kidogo wa Pemba wanaoshi Unguja.

 

Akizungumzia sababu za chama chake kutopata kiti tangu kisajiliwe kisheria, Bamba alisema Jahazi Asilia ni chama cha tatu bora cha kisiasa Zanzibar ambacho kinapingana na  siasa za ukabila, asili na historia na kusema siasa za asili wenye nazo ni CCM na CUF.

 

“CCM na CUF wanaendekeza ukabila na asili za visiwa, Jahazi haitaki kujiegemeza  huko, kuyakaribisha hayo kunaweza kuijengea tena nchi  matabaka, ubaguzi na machafuko ya kijamii,” alisema.

 

Alipotakiwa kutoa maoni kuhusu matamshi ya  hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kuwania tena ukatibu mkuu wa chama chake na kuwania urais mara ya nne mwaka  2015, Bamba alisema hakutegemea kusikia matamshi hayo hata kama ni ya kidemokrasia na kikatiba.

 

“Malim Seif ni mwanasiasa mahiri katika kuanzisha jambo, tatizo lake ni dhaifu katika umaliziaji. Anasumbuliwa na msukumo wa asili ya Unguja na Pemba, ataendelea kupata kura nyingi Pemba na haba Unguja, hilo limemkwamisha ashindwe kufikia ndoto na matlaba yake,” anabainisha Mwenyekiti huyo wa Jahazi Asilia.

1174 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!