wpid-Charles-KitwangaMambo mapya yameibuka kuhusiana na kuvuliwa uwaziri kwa aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, aliyevuliwa wadhifa huo Mei 20, 2016 baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.

Vyanzo vya habari vya uhakika vimeiambia JAMHURI kuwa Kitwanga alikunywa pombe akiwa na wageni wake (wakiwamo madiwani), waliotoka jimboni kwake na kuachana nao majira ya saa 10 alfajiri.

Katika hali isiyotarajiwa, majira ya saa 7 hadi 8 usiku, alimpigia simu mmoja wa wasaidizi wa Waziri Mkuu akimtaka kumwezesha kuzungumza na Waziri Mkuu muda huo, jambo lililowashtua na kulazimika kumtafuta mlinzi wake kufahamu mahali waziri huyo alipokuwa wakati huo.

Mlinzi hakupatikana kueleza kwa nini bosi wake alikuwa baa hadi usiku wa manane, suala lililowalazimu kuwasiliana na polisi Mkoa wa Dodoma wafanye kazi hiyo.

“Ililazimu kuwasiliana na mkubwa Dodoma ili kuweza kumfuatilia kiongozi wao yuko katika mazingira gani wakati ule. Vijana walikwenda na kumkuta akiendelea kupata kilevi na wageni wake. Si unajua tena ni mkubwa? Sasa jinsi ya kumwondoa pale ndipo kazi ilipoanza,” anasema mtoa taarifa.

Vyanzo hivyo vinabainisha kuwa Waziri Kitwanga alipofika katika viunga vya Bunge, alikutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Likuvi, ambaye alimuuliza kama yuko sawa kutokana na mwonekano wake, ambapo alimjibu kuwa yuko sawa naye akamtania kwa kumwambia ‘nakuona umechangamka leo’.

Pia alikutana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, alipomwona alishtuka na kumwomba kutoingia bungeni kutokana na hali yake kuwa angemsaidia kujibu maswali ya wizara yake arudi nyumbani akapumzike, lakini Kitwanga alimkatalia.

“Mwakyembe alifanya juhudi za kumzuia Kitwanga asiingie katika ukumbi wa Bunge, na alimwomba amkabidhi majibu ya maswali yake ili aweze kujibu kwa niaba yake, lakini jamaa ni king’ang’anizi akamkatalia akaingia ukumbini na moja kwa moja akaenda kukaa kwenye kiti cha kujibia maswali kabla ya kuitwa.”

Inaelezwa juhudi za Waziri wa Sheria na Katiba ziligonga mwamba, hivyo aliamua kuachana naye huku akishangazwa na hatua yake ya kulazimisha kuingia bungeni akiwa katika hali ile.

“Unajua hili jambo limemkera sana bwana mkubwa. Ilimlazimu kumuuliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama; aliyesema kuwa yeye binafsi alishindwa kumwelewa kwa siku hiyo maana Kitwanga ni mtu wa utani, hivyo alidhani anatania kama kawaida yake akamwacha aendelee, lakini kumbe hakuwa katika hali nzuri,” anasema mtoa taarifa.

Wahudumu wa Bunge inaelezwa kuwa walikwenda kumsihi Kitwanga atoke kwenye kiti cha kujibia maswali kwani muda wake wa kujibu swali ulikuwa haujawadia, lakini aliwakatalia.

“Siku hiyo alikuwa anafanya vituko tu. Alikuwa anamsukumia nyusi kila aliyeangaliana naye usoni. Hata mawaziri wawili anaokaa nao, inasemekana aliwaambia ‘leo nimezitwanga’. Kimsingi alikuwa kituko kwa kila aliyemwona,” anasema mtoa habari wetu.

Vyanzo vingine vinasema Kitwanga akiwa mkoani Arusha wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, alikutwa baa akiwa amezungukwa na jinsia inayodhaniwa ilikuwa kazini kumchomoa fedha akiwa amelewa.

“Hii siyo mara ya kwanza kwa Kitwanga kufanya mambo ya ajabu. Aliwahi kumiss behave wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mkoani Arusha. Alikutwa baa usiku amelewa akifanya mambo ya ajabu. Suala la kulewa na kufanya madudu siyo jambo jipya kwake,” anasema mtoa taarifa mwingine.

Vyanzo vya habari kutoka mkoani Mwanza vinaelezwa kuwa Kitwanga akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alikuwa anawapa wakati mgumu polisi, kwani yeye ilikuwa akiingia baa hakuwa anakumbuka kuwa baa zinafungwa saa 5 usiku.

“Wakati mwingine ilikuwa tunamwambia kuwa mheshimiwa muda umepita sana na nafasi uliyonayo haikuruhusu wewe kuendelea kuwa baa kwa muda huu, anatufokea na kusema tukisumbua atatusemea kwa Rais,” anasema mtoa habari wetu.

Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Tanzania ndiyo mawaziri pekee wanaopewa ulinzi kutokana na unyeti wa wizara wanazoziongoza na taarifa wanazopatiwa za kiusalama kila linapotokea tukio lolote.

Mawaziri wa nafasi hizo ndiyo viunganishi wa vyombo vya dola na Rais, hivyo wanapaswa kuwa watu wenye kutunza siri na kulinda heshima ya nchi wakati wote wanapokuwa kazini au nje ya kazi.

Ulevi wa Kitwanga kama ulivyotajwa na Ikulu umeibua manung’uniko na hisia zinazoacha maswali mengi, huku baadhi ya watu wakidai kuwa maji aliyopewa kunywa asubuhi yalichanganywa na ‘dawa za kulevya’ na wabaya wake aliowadhibiti alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Madiwani kutoka Misungwi, jimbo analoongoza Kitwanga, wameapa kulichukulia hatua Bunge kwa maelezo kuwa lilichezea picha zeke kiufundi kuonesha kuwa alikuwa amelewa wakati hajalewa.

Katika hatua nyingine, wapo wanaohoji kuwa lipi lilikuwa zito la kumfukuzisha kazi Kitwanga kati ya ulevi na kuhusishwa kwake na mkataba wa kupora fedha za umma.

Kitwanga anatajwa kuhusika na kashfa ya ufisadi katika Jeshi la Polisi ya Sh bilioni 34 kupitia kampuni yake ya Infosys iliyopewa zabuni na kampuni ya Lugumi Enterprises.

Jeshi la Polisi limekumbwa na kashfa kubwa ya ununuzi wa vifaa vya kuchukua alama za vidole ambapo Kamati ya PAC iligundua kuwa kampuni ya Lugumi Enterprises haikutekeleza mkataba ipasavyo.

Lugumi ililipwa Sh bilioni 34 na Jeshi la Polisi kusambaza vifaa hivyo nchi nzima katika vituo 138 vya polisi, lakini vituo 14 pekee ndivyo vilivyopata vifaa hivyo.

Kitwanga anahusishwa katika kashfa hiyo kutokana na kudaiwa kuwa mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Infosys anayoimiliki pamoja na baadhi ya maafisa waandamizi serikalini.

Kampuni hiyo ya Kitwanga inaelezwa kufanya kazi ya kuunganisha internet kati ya vituo vya polisi na mkongo wa Taifa, kazi ambayo haikufanyika kabisa.

Kitwanga amewahi kunukuliwa na vyombo vya habari (siyo gazeti hili), akisema kuwa hana uhusiano wowote na Kampuni ya Infosys kama watu wanavyodai.

Amesema halijui suala la Lugumi na kwamba anashangazwa na jinsi  anavyohusishwa nalo wakati kampuni hiyo inapewa mkataba na Serikali yeye hakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Taarifa iliyotolewa na PAC hivi karibuni inaonesha kuwa kampuni ya Lugumi iliingia mkataba na Jeshi la Polisi mwaka 2011, kwa kazi hiyo ya kufunga mitambo kwenye vituo vya polisi vya wilaya nchi nzima na kubainika kutotimiza matakwa ya mkataba huku ikiwa imelipwa asilimia 90 ya fedha zote za mkataba, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya ununuzi ya Serikali.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/2014 ndiyo iliyofichua uozo huo.

Hadi tunakwenda mitamboni, juhudi za kumpata Kitwanga kujibu hoja hizi hazikuzaa matunda, kwani kila unapoambiwa yupo ukifika unaambiwa ametoka na hata simu yake inaita bila kupokewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alipoulizwa na JAMHURI, kwa sauti ya upole amesema hajui lolote kati ya maswali aliyoulizwa na gazeti hili.

“Tulikwenda Bunge vizuri, yakatokea yaliyotokea, hivyo sijui lolote,” anasema Mambosasa.

Ofisi ya Bunge tayari imetoa taarifa kukanusha habari kwamba maafisa wake walitumia utaalamu wa hali ya juu kuchezea picha za Kitwanga na kudai kuwa ofisi hiyo inafanya kazi kwa weledi na wala haina mpango wa kumhujumu mbunge yeyote.

Bunge limekumbwa na lawama hizo baada ya kuanza kudhibiti matangazo ya televisheni yasirushwe ‘live’, na hivyo wananchi walio wengi wanaamini kwa sasa linafanya kazi ya kukata na kurusha vipande vya picha walivyo na maslahi navyo na si habari kama zinavyotokea bungeni.

By Jamhuri