Maisha ya wananchi wanaoishi jirani na Kiwanda cha Bakhresa cha kuchakata matunda kilichopo katika Kijiji cha Mwandege, Mkoa wa Pwani, yapo hatarini kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kiwanda hicho.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wananchi hao wanasema maisha yao yapo hatarini kutokana na mfumo wa majitaka unaotiririsha maji kutoka ndani ya kiwanda hicho na kutiririshwa kwenye makazi yao.

Wanasema kijiji chao kimekuwa katika mvutano wa muda mrefu na uongozi wa kiwanda hicho, kutokana na hali hiyo bila mafanikio yoyote huku wakiendelea kuathirika.

“Ni kweli nchi yetu inahitaji uwekezaji kama huu, lakini wamiliki hawana budi kuweka mazingira mazuri ya kiafya kwa wakazi wanaozunguka eneo husika,” anasema mwananchi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Anasema katika siku za hivi karibuni kiwanda hicho kilitembelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Pombe Magufuli, lakini hawajui kama walimweleza ukweli kuhusu uchafuzi huo wa mazingira unaohatarisha afya zao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwandege, Athmani Ubuguyu, anasema mpaka sasa yeye kama kiongozi wa kijiji, suala hilo lipo nje ya uwezo wake kwani alikwishafanya kila jitihada lakini imeshindikana.

Ubuguyu anasema mamlaka zote zinazoshughulikia mazingira zilishafika katika Kijiji cha Mwandege na kufika katika ngazi ya wilaya hadi Taifa, hata hivyo hakuna kilichofanyika hadi leo.

Anasema mamlaka husika zinapaswa kufanya kazi kwa kutanguliza maslahi mapana ya wananchi kuliko kuangalia maslahi ya hawa wanaoitwa wawekezaji.

“Kilichobaki kwangu mimi ni kutoa ushirikiano kwa kila taasisi inayokuja kuulizia suala hili, ila kwa upande wangu kama kiongozi wa kijiji nilishamaliza majukumu yangu,” anasema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwandege, Hassan Abdallah, anakiri uwepo wa tatizo hilo na kudai limekwamishwa na mamlaka husika kwa kushindwa kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo.

Abdallah anasema kuwa miezi mitatu iliyopita, maafisa wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) walifika kijijini hapo kukagua na kujiridhisha uwepo wa tatizo hilo la kiwanda hicho lakini wameshindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hili.

Anasema wakazi wa eneo hususani watoto wanakabiliwa na tatizo la upumuaji hasa nyakati za usiku ambako kiwanda kinapokuwa kimewasha mitambo yake yote. 

“Kiwanda kina mifumo mibovu ya utunzaji wa majitaka; kuna wakati maji yalivunja ukuta uliowekwa na kutiririka hadi nje ya kiwanda na kuharibu nyumba zilizoko jirani, haijulikani hadi leo madhara ya kiafya waliyopata wananchi hao hadi leo.

“Kiwanda kina mfumo wa kuhifadhi majitaka yaliyokwishatumika kiwandani, lakini maji haya yanapigwa na upepo yanatoa mvuke ambao ukiwafikia wakazi wa eneo hilo miili yao huwasha na kuanza kujikuna pamoja na kukohoa,” anasema Abdallah.

Haya ni maji yenye kemikali kutoka kiwandani, yanaposhindwa kudhibitiwa kwa kujengewa miundombinu salama ni hatari hata kwa wafanyakazi wa kiwandani wenyewe,” anasema Abdalah.

Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Dk Bonaventura Obaya, anasema ofisi yake inazo taarifa za uchafuzi huo wa kimazingira unaofanywa na kiwanda hicho na kukiri kuwa maofisa wake wamewahi kwenda huko.

“Ni kweli kuna maofisa wangu walishakwenda huko Mwandege, hebu nipe muda kidogo nijaribu kutafuta majibu yaliyo sahihi kutoka kwa maofisa wangu wanaolishughulikia suala hilo,” anasema Obaya. 

Anasema mamlaka yake kwa kawaida inafanya kazi kwa mujibu wa sheria kwa maana hiyo kama kuna tatizo ambalo ni kubwa mamlaka yake haiwezi kulifumbia macho. 

“Ndugu mwandishi, mimi kama Mkurugenzi siwezi kujua kila kitu kinachoendelea ndiyo maana kuna mgawanyo wa kazi katika taasisi yoyote ile, kama kuna uozo wowote uliofichwa na maofisa wangu watawajibika,” anasema Obaya.

Anasema Baraza hilo linayo mamlaka ya kusimamia shughuli za utunzaji wa mazingira nchini, chini ya sheria namba 20 ya Utunzaji na Usimamizi wa Mazingira (EMA) ya mwaka 2004.

Anasema Sheria hiyo ya mazingira ilianza kutumika rasmi Julai mosi, 2005. Katika kutekeleza majukumu yake NEMC ina mamlaka ya kukuza, kuchochea, kusimamia na kuunganisha masuala yote yanayohusiana na mazingira.

Anasema ofisi yake inayo malalamiko mengi nchi nzima yanayotokana na uchafuzi wa mazingira na mengi yamefanyiwa kazi na mengine yanaendelea kufanyiwa kazi. 

“Suala la uchafuzi wa mazingira ni mtambuka linalohitaji kupigwa vita na kila mmoja miongoni mwetu kwa manufaa ya Taifa letu na kizazi kijacho,” anasema Obaya.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,  Luhaga Mpina, alipoulizwa juu ya uchafuzi huo wa mazingira amesema kuwa ofisi yake bado haijapokea malalamiko ya wananchi hao na hakuna mwananchi aliyewahi kufika ofisini kwake kuhusiana na hilo.

“Malalamiko ya wananchi hao hayajawahi kufikishwa ofisini kwangu lakini maadamu umenipa taarifa hizi nitahakikisha nawasiliana na NEMC wanipe faili nielewe walikofikia. Jumatatu litakuwa jambo la kwanza kufuatilia, na kama kuna ukiukwaji wa sheria kwa makusudi sheria husika zitachukua mkondo wake,” anasema Mpina.

Kwa upande wa msemaji wa Kampuni hiyo, Sufiani Husein, anasema kampuni yake imekuwa ikijitahidi kuangalia mfumo mzima wa mazingira kama sheria zinavyo agiza. Kampuni imejizatiti kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kiafya kwa wananchi wanaolizunguka eneo la kiwanda.

“Kiwanda kinajishugulisha na usindikaji wa matunda kwa hivyo suala la harufu linaweza kuwa la kawaida kwa wakamuaji wa matunda hasa nyakati za mvua, hata hivyo, uwekezaji tulioufanya ni mkubwa sana kukabiliana na tatizo,” anasema Husein.

Anasema wao kama wawekezaji wa ndani wanajitahidi kuhakikisha wanafuata kama sheria zinavyotaka katika kuhakikisha kiwanda kina kuwa na rafiki wa wananchi.

By Jamhuri