Wakazi wa kata za Boko na Bunju, Dar es Salaam wamekilalamikia Kiwanda cha Saruji cha Twiga Cement (Wazo) kwa uharibifu wa mazingira ambao umeathiri makazi na uharibifu wa mali zao.

Wakazi hao wameieleza JAMHURI kwamba maporomoko ya maji kutoka katika mabwawa ya kiwanda hicho yaliyoko katika eneo linalochimbwa miamba kwa ajili ya uzalishaji wa saruji, yamezidi kuhatarisha maisha yao na wanapotoa taarifa kwa uongozi wa kiwanda hawasikilizwi na kupewa ahadi zisizotekelezwa.

“Kiwanda hiki kimetuathiri sana, na sasa tunaishi maisha magumu, nyumba zetu zimezungukwa na makorongo makubwa yaliyosababishwa na maji kutoka Kiwanda cha Wazo, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo hili,” wanasema wananchi hao.

Walioathiriwa wazungumza  

Joseph Mabwati, mkazi wa Boko, anasema kwamba Machi 2014 nyumba yake ilibomolewa na maji yaliyotoka katika mabwawa ya kiwanda hicho, yaliyokuwa yamekatika kutokana na kulemewa na wingi wa maji.

Anasema nyumba yake ilisombwa na maji pamoja na kila kitu kilichokuwamo ndani ya nyumba hiyo, na kutakiwa na uongozi wa kiwanda hicho kupeleka taarifa ya hasara iliyotokana na uharibifu huo ili alipwe fidia.

Mabwati anasema tangu alipopeleka taarifa hiyo ya hasara iliyosababishwa na maji kutoka katika kiwanda hicho kwa Meneja anayehusika na mazingira kiwandani hapo, Gerald Magoda, ameendelea kubabaishwa hadi leo hii hajalipwa kama alivyoahidiwa na uongozi wa kiwanda.

“Nilitakiwa kupeleka picha ya nyumba iliyoharibika, duka na mali zote zilizopotea na taarifa ya hasara iliyopatikana na kutakiwa kuifanya iwe siri kati yangu na uongozi wa kiwanda, ili wananchi wengine wasielewe na wao kuanza kudai fidia.

 “Nikapelekwa kwa Magoda na aliyekuwa diwani wetu aliyejulika kwa jina la ‘Maji Safi’, lakini hakuna kilichoendelea zaidi ya kuambiwa siwezi kulipwa chochote hadi upimaji wa ardhi utakapofanyika ndipo wanaweza kufikiri jinsi ya kunilipa,” anasema Mabwati.

Anasema maji ni mengi mno yanayotoka katika kiwanda hicho wakati wanapoyafungulia mabwawa, au kipindi cha mvua na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa ardhi na mashimo yanayoharibu makazi yao.

Hata hivyo, ameziomba mamlaka husika ikiwamo Wizara ya Mazingira kuwasaidia kupata haki zao zilizozuiwa kwa makusudi na uongozi wa kiwanda hicho kutokana na wananchi wengi kutokujua sheria za mazingira.

Naye Alicheraus Mwesiga, mkazi wa Boko CCM, ambaye nyumba yake iko hatarini kuanguka kutokana na kuzungukwa na shimo kubwa lililotokana na maji yanayotoka katika kiwanda hicho, anasema suala hilo alilifikisha katika Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Mazingira, na Chama Cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) bila mafanikio.

Anasema Aprili 2, 2013 walimwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT ambako walipewa msaada wa kisheria dhidi ya kiwanda hicho kwa kushindwa kusimamia sheria namba 20 ya mwaka 2004 ya mazingira.

LEAT walipeleka barua za kuwataka wahusika kusimamia sheria, vinginevyo watafungua mashtaka dhidi yao Aprili 22, 2013 ikiwa na kumbukumbu namba LEAT/BOKO/NEMC/1 lakini waliendelea kuachilia maji hayo.

NEMC kwa upande wao, walijibu barua hiyo Juni 22, 2013 yenye kumbukumbu namba NEMC/508/1/VOL.11/32 ikieleza tatizo la mfumo mbovu wa miundombinu ya kiwanda hicho, imesababisha uharibifu huo wa mazingira na kwamba hakikuwa na cheti cha tathmini ya athari za mazingira na kuamuliwa na Baraza hilo kufanya uhakiki wa mazingira yake.

Pamoja na maagizo hayo ya NEMC, kiwanda kimeshindwa kufanya marekebisho na kusababisha wakazi wa Boko CCM, Basihaya, Chasimba, Shule ya Msingi ya Mtambani, Kanisa Katoriki la Boko CCM, Zahanati na maeneo mengine kuathiriwa na mmomonyoko wa ardhi unaotokana na maji hayo.

Mwesiga na majirani zake wamekumbwa na athari ya mmomonyoko wa ardhi uliobomoa kuta za nyumba zao kutokana maji kutoka katika kiwanda hicho.

JAMHURI imetembelea maeneo yote yanayolalamikiwa na wananchi hao na kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaohatarisha maisha ya watu unaosababishwa na maporomoko hayo ya maji.

Hata hivyo, kile kinachotafsiriwa na wakazi wa maeneo hayo kwamba ni kushindwa kuzingatia sheria za utunzaji wa mazingira ama kutowajali wananchi ni uongozi wa kiwanda hicho cha saruji umechimba mfereji wa kupeleka maji Mto Nyakasangwe, lakini mfereji huo haujajengwa kabisa.

Wananchi wa maeneo hayo wanashangazwa na uchimbaji wa mfereji huo na kutelekezwa kwa muda mrefu na kiwanda, na kwamba kama jitihada za ujenzi hazitafanyika linaweza kuwa korongo litakaloleta uharibifu mkubwa sana utakaoleta athari kwa mamia ya watu.

“Mfereji umechimbwa lakini haujajengwa na hii inadaiwa kuwa ni kazi ya mhandisi wa kiwanda. Kiwanda kinahatarisha maisha ya watu na vyombo husika vinaona sawa hata kama mamia ya Watanzania watapoteza maisha,” anaeleza Jumanne Hamis, mkazi wa Mtaa wa Boko.

Naibu waziri azungumza 

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, akihojiwa na JAMHURI kuhusu malalamiko hayo ya wananchi walioathirika na uharibifu wa mazingira kutoka kiwanda cha Wazo, anasema amepata malalamiko hayo na kuwaagiza NEMC kufanya ukaguzi mara moja.

Anasema pamoja na kuwaagiza NEMC, yeye mwenyewe amefanya jitihada za kufuatilia suala hilo ambako wiki iliyopita alifika kiwandani hapo lakini hakufanikiwa kuingia ndani kutokana na madai yaliyotolewa na uongozi wa kiwanda kwamba walikuwa wamepiga dawa kwa ajili ya kuua vijidudu katika eneo lote la kiwanda.

“Haiwezekani wananchi walalamike halafu tukae kimya; niliwatuma NEMC na walitoa maelekezo lakini wamepuuzwa, kwa hiyo natarajia kufanya ziara tena maeneo yote ya kiwanda hicho na tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi,” anasema Mpina.

Mbunge wa Kawe

Naye Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee, anasema kiwanda kilitakiwa kujenga mfereji ili kuyapeleka maji katika Mto Nyakasangwe kwa ushirikiano na Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni na kinachosubiriwa ni tathmini ya ujenzi huo.

Kuhusu nyumba zilizobomoka kutokana maji yanayotoka katika kiwanda hicho na madai ya fidia za wananchi hao Mdee anasema hana taarifa zozote kuhusu suala hilo.

Mtendaji wa Mtaa wa Boko

Mtendaji wa Mtaa wa Boko, Ernest Mponda, anasema athari zinazotokana na maji yanayotoka katika Kiwanda cha Saruji cha Twiga ni kubwa sana na kipindi cha mvua maeneo mengi hayapitiki ikiwamo Shule ya Msingi ya Mtambani.

“Hawa Kiwanda cha Saruji cha Wazo ndiyo chanzo cha uharibifu wa mazingira katika maeneo haya na tumewaeleza jinsi athari zilivyo na kuna sehemu zilizojengwa miundombinu lakini tatizo bado ni kubwa,” anasema Mponda.

Akizungumzia mfereji uliochimbwa na kiwanda kwa lengo la kuyapeleka maji katika Mto Nyakasangwe ukiwa chini ya viwango, anasema wamefikisha hoja zao kwa uongozi wa kiwanda hicho na kuelezwa kwamba wanaandaa bajeti nyingine kwa ajili ya ujenzi huo.

NEMC wakwepa 

Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), limewakana wananchi hao kwamba halihusiki na malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa hadi kufikia mwaka 2012.

Akihojiwa na JAMHURI, msemaji wa Baraza hilo, Ruth Mgwaza, anasema migogoro yote ya mazingira walikwisha ikamilisha mwaka huo, hivyo hakuna migogoro inayoendelea.

“Tulimaliza migogoro yote ya mazingira hadi kufikia mwaka 2012 kwa hiyo hatuendelei na mashauri yoyote yaliyoishia kipindi hicho,” anasema.

Wakati Mgwaza akieleza kwamba migogoro yote inayohusu uharibifu wa mazingira ilipatiwa ufumbuzi, Naibu Waziri wa Mazingira, Mpina, anasema hawawezi kufumbia macho mgogoro huo wa wananchi na Kiwanda hicho cha Saruji.

Mpina anasema madai ya NEMC kwamba ilimaliza mgogoro huo na mingine inayohusu uharibifu wa mazingira tangu mwaka 2012, hayana msingi wowote kwani wananchi waliokumbwa na athari hizo bado wanalalamika.

Meneja wa kiwanda

Meneja wa Mazingira na msemaji wa kiwanda hicho, Magoda, anayedaiwa kuwalaghai waathirika wa maji yanayotoka kiwandani hapo na kuharibu nyumba na mali zao kwa kuwataka waandike taarifa za hasara walizozipata ili walipwe fidia zao na lakini akawageuka kwamba hawatalipwa, anasema suala hilo ni refu.

Magoda kwa kushindwa kujibu maswali ya mwandishi wa JAMHURI  aliyoulizwa, alituma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) yenye maelezo haya “do u think we are that much stupid??”

Alipoulizwa tena kuhusu kitendo chake cha kuwalaghai wananchi aliowataka wampe gharama za hasara zilizotokana na kubomolewa nyumba zao na maji kutoka katika kiwanda hicho, alijibu kwa ukali “tunafanya kazi kwa mujibu wa taratibu za nchi, sina msaada zaidi na kukata simu yake.”

1557 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!