Kiwanda cha Sukari chafutwa uwekezaji

Wimbi la uingizwaji wa sukari nchini kwa njia ya magendo limeleta athari kubwa kwa viwanda vya ndani na baadhi yao sasa vimeanza kupunguza wafanyakazi pamoja kufuta baadhi ya mipango yake ya uwekezaji ya muda mrefu.

Hali hiyo pia inadaiwa kuinyima Serikali mapato yatokanayo na kodi mbalimbali kutoka katika viwanda hivyo huku nyongeza ya mishahara na marupurupu kwa wafanyakazi ikipungua kwa kasi ya kutisha.

Kiwanda cha Sukari cha TPC kilichopo nje kidogo ya mji wa Moshi, ni moja ya viwanda ambavyo vimeathiriwa na sukari hiyo ya magendo na hivyo kusababisha kushuka kwa uzalishaji kutoka tani 420,000 mwaka jana hadi kufikia tani 320,000 ikiwa ni hasara ya tani 100,000.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni kwa wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro (RCC), uongozi wa kiwanda hicho umedai kuwa umefuta mpango wake wa uwekezaji wa miaka mitano wenye thamani ya Sh. bilioni 100 kutokana na wimbi hilo la sukari kutoka nje ya nchi.

Akiwasilisha taarifa ya kiwanda hicho, Mtendaji Mkuu anayeshughulikia masuala ya utawala, Jaffari Ally, anasema kuwa kiwanda chake kimeahirisha mpango huo kutokana na kushuka kwa shughuli za uzalishaji huku gharama za uendeshaji zikipanda.

Anasema kuwa madhara ambayo kiwanda hicho kimeyapata kutokana na wimbi hilo ni mrundikano mkubwa wa sukari katika maghala na gharama za ziada za kuhifadhi sukari hiyo huku akionya hatari ya kuporomoka kwa ustawi wa sekta ya sukari nchini.

Alitaja madhara mengine kuwa ni wazalishaji  wa sukari nchini kushindwa kulipa wadau wao sambamba na kushindwa kurejesha mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha yakiwamo mabenki.

Kwa mujibu wa Jaffari, kwa miaka miwili sasa bei ya sukari imekuwa ikiporomoka kwa kasi huku gharama za uzalishaji zikipanda kutokana na soko kufurika sukari ya nje ya nchi, hatua ambayo alidai itawavunja moyo wawekezaji.

Anasema mrundikano wa sukari kwenye maghala ulifikia tani 37,000 hadi Januari, mwaka jana huku mzunguko wa fedha ukidaiwa kuwa mgumu kwa wazalishaji wa bidhaa hiyo na kuonya kuwa mwenendo huo utaisambaratisha sekta ya sukari.

“Mheshimiwa mwenyekiti, upo uwezekano kwa sekta ya sukari kuyumba kwani wakulima wa nje kwa sasa wamekata tamaa kulima zao la miwa na kuwatia hasara zaidi ikiwamo kufilisika lakini uwekezaji zaidi katika sekta hii utapotea mfano kiwanda chetu cha TPC,” anasema.

Anasema kuwa kiasi kikubwa cha sukari kutoka nje ya nchi inaingizwa bila uhalali kwa maana ya kutolipiwa ushuru na hivyo kuwalazimisha wazalishaji wa ndani kushusha bei ili kushindana na sukari kutoka nje ili kutanzua matatizo ya mtiririko wa fedha pekee.

Kiwanda hicho cha sukari ambacho kimekuwa kikielezewa na Serikali kama moja ya viwanda vilivyobinafsishwa kwa mafanikio makubwa na kufanya vizuri kwenye uwekezaji, hadi kufikia Juni mwaka juzi, kilikuwa kimewekeza kiasi cha Sh. bilioni 124 tangu kilipobinafsishwa.

Kwa mujibu wa mtendaji huyo, uwekezaji huo ulijikita katika ukarabati wa kiwanda, mashamba na miundombinu na kuongeza kuwa uwekezaji huo umetokana na mapato ya ndani, mikopo kwa wanahisa kutoka katika mabenki ya ndani ya nchi.

Kufutwa kwa mpango huo wa uwekezaji kwa miaka mitano ni pigo pia kwa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ambayo imekuwa ikivuna mamilioni ya shilingi kutoka kiwandani hapo kama mapato na ushuru wa halmashauri.

Takwimu zilizotolewa na TPC, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mwaka 2010 ilivuna milioni 65, mwaka 2011 ikapata milioni 80 na mwaka 2012 ikalipata milioni 86.

Kwa mujibu wa mchanganuo huo, mwaka 2013 halmashauri hiyo ilipata kiasi kikubwa cha Sh milioni 448 wakati mwaka jana mavuna yalishuka hadi kiasi cha Sh milioni 431 hii ni baada ya kuanza kuyumba kwa soko la ndani kutokana na wimbi la sukari ya ya magendo.

Kwa upande wa Serikali Kuu, TPC inadai kuwa inapoteza kodi ya kati ya Sh. bilioni 50 hadi 70 kwa mwaka kutokana na ukwepaji huo wa kodi huku hasara zaidi katika pato la taifa ikitarajiwa kuongezeka.

Kiwanda hicho kinaonya kuwa maelfu ya Watanzania wanaotegemea kipato chao kutoka sekta ya sukari ajira zao zitapotea, kuongezeka kwa wimbi la umaskini na kubakia Taifa tegemezi la sukari kutoka nje ya nchi itakayouzwa kwa bei ya juu zaidi.

Kiwanda hicho kilibinafsishwa na Serikali mwaka 2000 kwa Kampuni ya Sukari Investment Company Ltd (SIL) ya nchini Mauritius ambayo ilinunua asilimia 75 ya hisa na Serikali kubakiwa na hisa 25.

Aidha, Sukari Investment inamilikiwa na kampuni mbili ambao ni Alteo Limited kutoka Mauritius kwa asilimia 60 na Kampuni ya GQF (Tereos) kutoka kisiwa cha Reunion inayomiliki asilimia 40.