SIKU chache baada ya uongozi wa Simba kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mfaransa, Pierre Lechantre, imebainika kuwa kocha huyo amepata dili nono nchini Libya katika Klabu ya Al Nasr inayoshiriki ligi kuu ya nchi hiyo.

 

Hivi karubuni Lechantre ambaye ameiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, aliondoka klabuni hapo baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia katika msimu ujao wa ligi kuu.

 

Hata hivyo habari za kuaminika ambazo zimepatikana zimedai kuwa Lechantre amepata dili la kuifundisha Al Nasr ya Libya na atakuwa akilipwa kwa mwezi kitita cha dola 60,000 (zaidi ya Sh 136m) kwa mwezi.

 

Kiasi hicho cha fedha kinadaiwa kuwa ni mara tatu zaidi ya kile alichokuwa akikipata alipokuwa Simba ambapo inadaiwa kuwa alikuwa akilipwa dola 20,000 (zaidi ya Sh 45 milioni) kwa mwezi.

“Dili hilo la Lechantre ni tofauti na zile tatu alizokuwa nazo kabla ya kuondoka Simba ambapo alikuwa na ofa ya kuifundisha timu ya taifa ya Cameroon na Kuwait lakini pia alikuwa na ofa nyingine nchini Algeria katika klabu ya ligi kuu ya nchi hiyo.

 

“Nimeongea naye jana (juzi) na akaniambia kuhusiana na dili hilo la Libya lakini akadai kuwa bado hajafanya uamuzi wa kujiunga na timu hiyo kwani kuna mipango yake mingine ya kifamilia anaiweka sawa, itakapokuwa sawa ndipo atakapofanya maamuzi ya wapi anaenda,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipotafutwa Lechantre ambaye kwa sasa yupo nyumbani kwake nchini Ufaransa, hakupatikana.

 

By Jamhuri