Kodi vifaa vya gesi zifutwe, tuokoe misitu

Mungu alitupendelea Watanzania. Akatupatia ardhi na misitu mingi, mizuri na yenye tija kubwa kwa binadamu na viumbe hai wengine.

Uzuri wa Tanzania sasa unaharibiwa na Watanzania wenyewe kwa uamuzi haramu wa kuteketeza misitu ya asili.

Takwimu zinaonyesha kuwa hekta 400,000 za misitu huteketezwa nchini kote kila mwaka kutokana na uchomaji mkaa, ukataji kuni na matumizi mengine ya miti.

Tani milioni moja za mkaa huzalishwa nchini kote kwa mwaka, na nusu ya kiasi hicho, yaani tani 500,000 zinatumika katika Jiji la Dar es Salaam pekee. Hizi ni habari za kusikitisha.

Biashara ya mkaa imeshamiri kweli kweli muda huu ambao kila Mtanzania anayejisikia ameamua kuifanya biashara hii. Ujio wa pikipiki nao umechangia sana uhalibifu huu.

Malori mengi yanasafirisha mkaa bila vibali, tena wakati mwingine ukiwa umefungiwa kwenye makontena kinyume cha sheria. Kila siku asubuhi pale Kwa Musuguri, Dar es Salaam mamia ya malori yanashusha maelfu ya magunia ya mkaa. Hakuna maofisa misitu wanaohoji!

Maelfu ya hekta za misitu yanateketezwa wakati viongozi wenye dhamana wakiwa kimya kana kwamba hawaioni hatari hii inayolikabili Taifa. Wabunge, mawaziri, wakurugenzi na watendaji wengi wanasafiri kote nchini wakishuhudia maelfu kwa maelfu ya magunia ya mkaa kando ya barabara, lakini wamekuwa kimya kana kwamba wanachokiona ni kitu cha kawaida.

Matumizi ya mkaa ni desturi iliyokomaa, na sasa imekuwa mila. Kuna sababu nyingi zinazosababisha kushamiri kwa biashara hii. Mosi, mahitaji ya nishati ya kupikia ni makubwa. Pili, upatikanaji wa nishati mbadala umekuwa hauendani na kasi ya ongezeko la watu.

Tatu, hakuna uhamasishaji wa dhati unaofanywa na viongozi na watetezi wa mazingira ili kuwawezesha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni ili watumie nishati mbadala, hasa gesi.

Tunaiomba Serikali ya Awamu ya Tano ilitazame tatizo hili kama janga la kitaifa. Tunashauri wahusika wajitokeze mbele na wahamasishe matumizi ya gesi. Bei ya gesi si kubwa kuliko mkaa, lakini wengi wameshindwa kumudu matumizi ya gesi kwa sababu bei kianzio ni kubwa.

Tunashauri Serikali ifanye utafiti na ikiwezekana ifute kabisa kodi zote kwenye vifaa vya gesi. Hii ni pamoja na gesi yenyewe, majiko na vipuri vya majiko.

Serikali ikaribishe wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa masharti nafuu kabisa wawekeze kwenye vifaa vya gesi kama majiko na mitungi ili viweze kupatikana na kutumiwa na watu wa kada zote.

Haya na mengine yakifanywa, tunaamini kabisa kuwa tutafungua ukurasa mpya katika kuilinda miti yetu; na hapo Serikali itakuwa radhi kutunga sheria kali za kuilinda misitu.

Ulinzi wa rasilimali misitu katika nchi yetu liwe ni jukumu la kila Mtanzania. Faida za misitu ni nyingi mno kuliko hizi za mkaa na kuni. Shime Watanzania tuiokoe misitu yetu. Mkaa ni janga la kitaifa.