Koffi Olomide ataja siri ya kufanya muziki muda mrefu

Mkali wa muziki wa rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Koffi Olomide Mopao Mokonzi, ametaja siri ya kuendelea kuwapo kwenye muziki kwa muda mrefu licha ya kuwa na umri mkubwa.

Olomide amesema hayo alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa Gazeti la JAMHURI katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena.

“Siri ya kuendelea kufanya vizuri katika muziki wangu, cha kwanza ni kumheshimu Mungu na kupenda kile ninachokifanya muda wote, kwani mtu yeyote ukimtegemea Mungu na kuheshimu unachokifanya, kila siku utataka kufanya kilicho bora kuliko jana, hivyo hiyo ndiyo sababu yangu mimi kuendelea kuwa kileleni,” anasema Olomide.

Mbali na hilo, Olomide pia anasema katika muziki wa sasa watu wengi hawapendi kujifunza, ndiyo maana wanabaki nyuma, lakini yeye hujifunza kila leo, ndiyo maana kuna tofauti kati yake na wanamuziki wengine wa Kongo.

Mkali huyo wa vibao vya ‘Papa Ngwasuma’, ‘Efrakataa’, ‘Mbirime’, ‘Selfie’, ‘Tcha Tcho’, ‘Monde Arabe’, ‘Loi’ na vingine vingi, amekuwa akisifiwa katika kutawala jukwaa, mpangilio wa ala za muziki na uimbaji mzuri.

Ujio wa mwanamuziki huyu nchini Tanzania katika Jiji la Dar es Salaam ambako amefanya shoo kubwa na yenye hadhi ya juu katika Ukumbi wa Mlimani City, umeacha funzo kubwa kwa bendi na wanamuziki wa muziki wa dansi nchini.

Mtangazaji wa vipindi vya muziki wa dansi nchini, Dakota Delavida, alipata kumuuliza Olomide kuhusu nini kinafanya muziki wa dansi nchini Kongo kuwa juu wakati katika nchi za Afrika Mashariki unashuka na bendi nyingi zinakufa, na wanamuziki kurudi kuimba miziki ya Lingala kama zamani.

Olomide alisema wanamuziki wengi Afrika wameacha kujiamini na kuimba kile kinachowahusu, hali inayofanya kushindwa kukonga nyoyo za mashabiki wao.

“Mimi huwa ninatazama mashabiki na wapenzi wanataka nini, ndipo ninawapatia hicho,” anasema.

Antoine Koffi Olomidé alizaliwa Agosti 13, 1956 Kisangani, DRC. Ni ni mwimbaji, mtayarishaji na mtunzi wa ngoma aina ya soukous kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Amelelewa katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa.

Alikwenda Ufaransa kusoma. Akiwa Paris, alianza kupiga gitaa na kuandika nyimbo. Aliporudi Kongo alijiunga na bendi iliyokuwa inamilikiwa na Papa Wemba ya Viva la Musica.

Olomide aliimarisha mtindo wa polepole wa soukous, uliokuwa umekwisha umaarufu. Aliuita mtindo huu Tcha Tcho, na ulipata umaarufu nje ya Kongo.

Muziki wa Olomide unaweza kusababisha utata, maana hutumia matukio na mada inayofikiriwa vibaya na kihafidhina katika jamii. Yeye pia ameshiriki katika mradi wa muziki wa salsa wa Africando.

Olomide ameshinda tuzo nne za Kora nchini Afrika Kusini, pia alishinda tuzo ya Msanii Bora Afrika ya Kati. Ameoa na ana watoto watano.