suleiman-kovaWiki mbili zilizopita, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, amemaliza mgomo wa madereva.   
Kova alimaliza mgogoro huo baada ya madereva kukataa kwenda tena darasani kila baada ya miaka mitatu, na akaagiza tochi zote za mwendo kasi ziondolewe barabarani na kusema ukaguzi utafanyika kwenye vituo vya mizani pekee.


Baada ya agizo hili la Kova, madereva wakashangilia. Wiki iliyopita niliandika makala kwenye safu hii nikieleza hatari itakayotokana na agizo hili la Kova. Wakati naandika makala hiyo, Jeshi la Polisi nchini likatangaza kuwa Watanzania 866 wamefariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu kutokana na ajali za barabarani.


Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, akasema kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, zimetokea ajali 2,116 katika maeneo mbalimbali nchini. Watu 866 wamepoteza maisha na wengine 2,363 kujeruhiwa. Takwimu hizo zikiongezwa na Machi hadi Aprili, mwaka huu watu wengine 121 wamekwishafariki ajalini. Hii ina maana watu 987 ajali zimechukua roho zao.


  Kamanda Mpinga anaamini mwendo kasi usiozingatia alama za barabarani na kufutika kwa baadhi ya michoro barabarani, vimechangia wingi wa ajali. Ipo pia tabia ya baadhi ya wamiliki wa mabasi kuhamasisha mwendo kasi kwa madereva wao, abiria kushabikia na baadhi ya wadau wa usalama barabarani kutowajibika ipasavyo, ambavyo pia vinazalisha ajali.


Uzembe wa madereva, ubovu wa barabara, uoni hafifu kwa baadhi ya madereva, utelezi, ulevi, uchovu na matumizi ya dawa za kulevya navyo vinachangia ajali.
Kamanda Mpinga ametaja pia tatizo la ubabe wa madereva wanaoendesha magari makubwa ya mizigo kutothamini magari madogo, waenda kwa miguu, bajaj na pikipiki wawapo barabarani.
Kati ya adhabu alizotaja ni pamoja na kuwanyang’anya leseni madereva waliosababisha ajali na ikibidi wenye magari kampuni zao zitafutiwa leseni za biashara hiyo.


Nikiangalia mawazo ya Kamanda Mpinga anawaza zaidi adhabu kali akifikiria zitaondoa tatizo. Kova kwa upande wake anawaza uhuru kwa madereva akidhani utaondoa tatizo.
Sitanii, inawezekana ndugu zetu hawa wana siku nyingi bila kusafiri kwa mabasi au kuendesha magari barabarani. Madereva wa mabasi ni pasua kichwa. Hawa wanapaswa kuadabishwa. Serikali hata kwa gharama zake inapaswa kuwarudisha darasani kuwafundisha umuhimu wa kuthamini maisha ya binadamu wenzao. Kila kukicha  tunasikia ajali mbili au tatu. Watu wanapoteza maisha.


Wakati Serikali iko ‘busy’ kuweka matuta barabarani, kwa mabasi matuta si lolote si chochote. Mabasi yanafukia matuta usipime. Katikati ya mji au kwenye makazi ya watu yanapita na kasi ya hadi kilomita 100 kwa sasa. Matrafiki lazima wafanye kazi ya ziada. Kuwa na kamera za mwendo kasi ni sawa na bure.
Madereva wanayo lugha yao ya ishara. Wanazungumza kwa vidole kama viziwi na wanaelewana. Trafki akiwa karibu ataona basi linatembea kama bibi harusi. Anashangaa hata akijificha porini kila walipo trafiki likiishapita gari moja tu, basi kumkamata anayefuata ni kazi.


Sitanii, tunahitaji kamera za kisasa barabarani badala ya matrafiki. Gharama ya kufunga kamera katika barabara kuu zitakazosoma mwenda wa gari kila baada ya kilomita 15 au 20 haiwezi kuwa sawa na maisha yanayopotea. Nchi zilizoendelea zimeweza kuondoa jinamizi la ajali kwa kutumia kamera (CCTV).
Kamera zinafungwa kila mahala barabarani, madereva hata wakipeana ishara wanazopeana sasa haitawasaidia maana mwendo wao utakuwa unaonekana makao makuu ya kikosi cha usalama barabarani na kwa namba gari linalozidisha mwenendo linapigwa faini mara moja au kumnyang’anya leseni dereva.
  Nilisema furaha ya muda Kova aliyowapa madereva, itakuwa balaa kwa nchi hii. Nadhani sasa wakati umefika. Kova afute tamko lake, matrafiki warudi barabarani kudhibiti mwendo wakati tunasubiri wazo la teknolojia ya CCTV kwa barabara zote nchini.


Sitanii, wakati tunasubiri wazo la CCTV tunapaswa sasa kuwakemea wamiliki wa mabasi. Kanuni zibadilishwe haraka wachukuliwe hatua za moja kwa moja. Haiwezekani wakaajiri wahuni wanaopoteza maisha ya wananchi bila kujali. Pia, polisi sasa wafanye kazi ya kupima kilevi. Zipo taarifa kuwa viroba vinamaliza madereva wetu. Wengi wanaendesha magari wakiwa wamelewa bwiii. Madereva pia wakaripiwe na kupewa mafunzo upya juu ya matumizi ya barabara. Bila kuchukua hatua kama hizi, tutakwisha.


Japo nafasi inazidi kuwa ndogo, lakini lipo moja niliseme.  Kinachotokea barabarani kwa madereva kutoheshimu sheria ni ishara pana. Ni ishara kuwa wananchi wameanza kuacha kutii sheria. Ni ishara kuwa tuliowapa kazi ya kusimamia sheria hawatendi ipasavyo. Ni ishara kwamba Tanzania sasa imegeuka nyumbani kwa kambale –  mdogo, mkubwa wote wana sharubu.
Hii ni ishara mbaya. Viongozi wetu sasa wanapaswa kurejesha heshima ya Jeshi la Polisi. Kwamba mwananchi amuone polisi hali rushwa ya kulazimisha barabarani. Matrafiki kwa kuchukua hadi rushwa za mikate, inaondoa hofu kwa madereva. Wanawaona matrafiki kama polisi jamii. Hii ni hatari. Hili tuikatae.
  Nahitimisha kwa kurejea kauli yangu kuwa Kova sitisha agizo lako, ajali zinamaliza Watanzania.

 

2195 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!