Kubadili hati ya nyumba, kiwanja kwa haraka andaa nyaraka hizi

Watu wengi wanaonunua ardhi wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa katika kubadili majina, yaani kutoka mmiliki wa awali kwenda kwa mmilki mpya aliyenunua.
  Upo usumbufu unaosababishwa kwa makusudi na maofisa wanaohusika, lakini pia upo usumbufu ambao husababishwa na watu wenyewe wanaotaka kubadili majina.
 Awali ya yote, lazima nikiri kuwa baadhi ya maofisa wa mamlaka za ardhi husababisha uchelewaji kwa makusudi kabisa na lengo likiwa kujenga mazingira ya kupozwa kidogo.
  Hili lipo na kila mtu ambaye amekuwa akishughulikia masuala ya hati na kubadili majina miliki kama mimi, atakiri kukutana na haya.
 Hao tuwaache. Mimi leo nazungumzia maandalizi ambayo ukiyafanya mapema utafanikiwa kwa urahisi na haraka kubadili jina la kiwanja au nyumba kutoka kwa mtu aliyekuuzia kuingia jina lako.
 
Umuhimu wa kubadili jina haraka baada ya ununuzi

Sheria iko wazi kuwa ambaye jina lake linaonekana kwenye hati ndiye mmiliki. Kwa kauli hii mnunuzi anatakiwa kufanya jitihada za haraka na za makusudi kubadili jina mara tu baada ya kununua kiwanja au nyumba.
 Sikatai kuwa kunakuwa na mkataba wa mauziano, lakini lazima ieleweke kuwa mbele ya macho ya sheria jina lililo kwenye hati lina uzito kuliko mkataba wa mauziano.
  Usiridhike kukaa na mkataba wa mauziano ikiwa hujabadili jina. Hii ni kwa ajili ya ulinzi wako na wa ardhi yako. Utakapotokea mgogoro wa umiliki ikiwa hujabadili jina waweza kuwa katika hatari kubwa ya kupoteza hasa kama mgogoro huo umeanzishwa na aliyekuuzia.
  Huu ndiyo ukweli na lazima tuonyane ili tuwe salama na mali zetu. Lakini pia hata ukitokea mgogoro mwingine wowote wa umiliki kuna mambo ndani ya sheria yataufanya kuwa mgumu kutokana na sababu tu kuwa ulikuwa hujabadili jina.
 Hapo sijaongelea faida nyingine za kubadili jina kama kukopa na kadhalika. Nishauri tu kwa ufupi kuwa unapojiandaa kununua nyumba au kiwanja, jiandae pia na kubadili jina moja kwa moja. Hakikisha haya mawili yanakwenda  pamoja.
 
Ili kubadili hati kwa urahisi kwa haraka hebu andaa nyaraka hizi

Nyaraka za uhamisho zinajumuisha fomu Na. 29 ijulikanayo kama Fomu ya Kusudio la Uhamisho (Notification of Disposition) ambayo hueleza nia na lengo la muuzaji kutaka kubadili jina au kuondoa jina lake katika hati.
  Hii utaandaa nakala tatu. Pili ni fomu Na. 30 ambayo hujulikana kama Fomu ya Ithibati ya Uhamisho (Application for Approval of Disposition). Katika  fomu  hii muuzaji pia atakuwa anatoa idhini kwa mamlaka za ardhi kuidhinisha hiari yake ya kuachia umiliki kutoka kwake kwenda kwa mtu mwingine ambaye ndiye mnunuzi.
 Mwisho ni fomu Na. 5 ijulikanayo kama fomu Rasmi ya Kuhamisha Umiliki (Transfer of Right of Occupancy) ambayo ndiyo rasmi sasa huhamisha umiliki kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi. Hii ndiyo inayompa mnunuzi umiliki rasmi. Pia mkataba wa mauziano ni nyaraka ambayo itaambatanishwa hapa.
  Kwa kiwanja au eneo ambalo halijaendelezwa (halijajengwa) huandaliwa kitu kiitwacho 'Commitment Bond' kikiwa kama ziada ya nilivyotaja hapo. Fomu zote hizo pamoja 'Commitment Bond hupatikana katika ofisi za wanasheria na huandaliwa na wanasheria.

Taarifa ya Uthamini

Taarifa ya uthamini ni taarifa rasmi ambayo hutoa tathmini ya thamani ya eneo/jengo. Lazima umtafute mthamini (valuer) ili athamini thamani ya eneo/jengo lako na hiyo taarifa iwasilishwe mamlaka za ardhi ili iweze kupitishwa na mthamini mkuu wa serikali Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi.
  Ukienda mamlaka za ardhi uliza utawakuta wathamini ili wakufanyie kazi ya uthamini ninayoongelea hapa.
 
Uraia

Sheria iko wazi kuwa wanaotakiwa kumiliki ardhi ni raia wa nchi hii tu. Hivyo unapotakiwa kupata hati ya umiliki lazima pia uthibitishe Utanzania wako. Hapa utatakiwa kuandaa nakala (copy) ya cheti cha kuzaliwa ambayo imethibitishwa (certified) na wakili au nakala ya pasipoti ambayo imethibitishwa na wakili au kama huna hivyo vyote basi yakupasa kuandaa kiapo (affidavit).

Ada

Ni muhimu pia unapofanya taratibu za kupata hati au kubadili jina kujiandaa na malipo ya ada za ardhi. Ada ziko aina tatu: kwanza 'stamp duty fee', 'consent/approval fee' na 'registration fee'. Sitaweka viwango vya ada hizi kutokana na kubadilikabadilika kwake.
  Mwisho napenda kusema kuwa ikiwa utajiandaa vyema na haya, utapata hati kwa urahisi au kama unabadili jina utabadili kwa urahisi pia. Jiandae, epuka usumbufu.
 
Mwandishi wa makala hii ni mwanasheria, pia tembelea sheriayakub.blogspot.com, usome ushauri sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa na kadhalika.