Wakati Rais John Magufuli akisisitiza mara kadhaa kwamba serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaokabiliwa na njaa, mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mazao yameharibika kutokana na mbolea za kukuzia kutofika kwa wakati kwa wakulima.

Rais Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilhali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.

Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni katika ziara yake mkoani Pwani wakati akizungumza na wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja, ikiwa ni ziara yake katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.

Hata hivyo wakulima waliozungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya wamesema mbolea ya kukuzia aina ya UREA na DAP haikupelekwa kwa wakati na matokeo yake mazao yao yalinyauka na kudumaa.

Wamesema mwaka huu wanatarajia kupata mazao ya chakula kwa kiwango kidogo tofauti na miaka iliyopita baada ya kucheleweshewa mbolea.

Rukwa

Mkazi wa Manispaa ya Sumbawanga na mkulima wa mahindi, Kotrida Tenganamba, amelieleza JAMHURI kuwa ucheleweshaji wa mbolea ya kukuzia umesababisha hasara kubwa kwa wakulima mwaka huu.

Amesema kwa mwaka huu wanategemea kuvuna magunia matano tu kwa ekari moja badala ya magunia 25 waliyokuwa wakivuna miaka iliyopita kutokana na mazao yao kuharibika yakiwa shambani kwa kukosa mbolea.

Tenganamba ambaye pia ni mjumbe wa Chama cha Ushirika wa Wauza Mazao katika Soko la Mandela, mkoani Rukwa, amesema hasara waliyoipata wakulima kutokana na kuchelewa kwa mbolea ya kukuzia itachangia kupanda kwa bei ya mahindi.

“Kwa sasa gunia moja la mahindi tunauza kwa Sh 30,000 na haya ni mahindi ya mwaka jana ambayo hatukuyauza, hii ni hasara kubwa sana kwetu wakulima na wafanyabiashara, soko ni gumu sana kwa sasa,” amesema Tenganamba.

Naye Mwenyekiti wa ushirika huo na mkulima wa mazao ya chakula mkoani humo, Lusubilo Kalinga, amesema mbolea imechelewa sana na kupishana na kilimo cha mahindi na kwamba hata kama itawekwa bado haiwezi kusaidia.

Kalinga amesema kutokana na mazao kuharibika sana kwa sasa kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula nchini.

“Soko letu la mahindi tulikuwa tunagemea wanunuzi kutoka nchi za Kenya, DRC na mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam lakini mwaka huu hatutaweza kupata chakula kama miaka iliyopita,” amesema Kalinga.

Hata hivyo kutokana na malalamiko ya wakulima mkoani humo kwamba mbolea ilichelewa kufika kwa wakati, JAMHURI lilipita katika maduka ya mawakala wa mbolea na kukuta mbolea hiyo ikiwa imerundikana huku wanunuzi wakiwa wachache.

Katika maduka hayo yamebandikwa matangazo ya bei elekezi ya mbolea kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga na kuwaonya wote watakaokiuka maelekezo hayo.

“Bei elekezi za rejareja za mbolea kuanzia Machi 1, 2018; mbolea ya kupandia (DAP) ni Sh 60,322 na mbolea ya kukuzia (UREA) ni Sh 56,977.

“Bei hizi zimepangwa kwa mujibu wa Kanuni ya 56 (3) ya kanuni za mbolea za 2011 zilizorekebishwa kwa tangazo la Serikali (G.N), Namba 50 la mwaka 2017 na bei hizi zitadumu hadi zitakapobadilishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 56 (4).

“Mfanyabiashara wa rejareja wa mbolea atakayeuza zaidi ya bei hizo atakuwa amevunja sheria na atahukumiwa kifungo jela cha miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 10,000,000 au vyote kwa pamoja,” imeeleza sehemu ya tangazo hilo lililobandikwa kwenye milango ya maduka ya mbolea Manispaa ya Sumbawanga.

RC Rukwa afunguka

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, amesema mahitaji ya mbolea ya kupandia (DAP) kwa mkoa huo ni tani 4,945 na hadi Februari mwaka huu walikuwa wamepokea tani 6,071.9 na hapakuwa na upungufu wa mbolea hiyo.

Wangabo amesema mbolea ya kukuzia (UREA) mahitaji ni tani 10,600, lakini iliyopokewa ni tani 7,147 huku kukiwa na upungufu wa tani 3,453.

Katika msimu wa 2016/2017, Mkoa wa Rukwa ulilima hekta 556,975.9 za mazao ya chakula na kuvuna tani 1,109,055.6 na kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602.

Kwa msimu huu wa kilimo wa 2017/2018  mkoa huo umelenga kulima jumla ya eneo la hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula, lakini lengo hilo linaweza kupungua kutokana na hali mbaya ya mazao kwa sasa iliyochangiwa na kuchelewa kwa mvua na mbolea.

Mkoa wa Songwe

Wakulima katika Mkoa wa Songwe nao wamelalamikia kucheleweshwa kwa mbolea, hivyo kusababisha mazao kuharibika hususan mahindi.

Edwin Haonga (51) mkazi wa Wilaya ya Momba, mkoani humo amesema pamoja na kuchelewa kufikishwa kwa wakati mbolea ya kupandia na kukuzia, kilichowaumiza wakulima ni serikali kutoweka ruzuku kwenye mbolea.

Haonga amelieleza JAMHURI kuwa kinachozungumzwa kuhusu mbolea ni siasa tu, kwani sababu kubwa ni kucheleweshwa, kwa kuwa serikali haikuhusika kwa namna yoyote katika uagizaji wa mbolea kwa mwaka huu.

“Kama hakuna ruzuku ni wazi kwamba wakulima wengi watashindwa kumudu bei, kwa sababu wafanyabiashara wanachohitaji ni kupata faida kubwa na iwapo watabanwa katika bei elekezi watasafirisha nje ya nchi,” amesema Haonga.

Bei elekezi ya mbolea kwa Mkoa wa Songwe ni kati ya Sh 53,500 na Sh 56,000 kwa mfuko wa kg 50 kwa mbolea aina ya DAP na UREA ni kati ya Sh 41,000 na Sh 43,000 kwa mfuko wa kg 50.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa, ameeleza kuwa mahitaji ya mbolea kwa mkoa huo ni tani 8,000 lakini wamepata tani 6,000 tu huku mbolea hiyo ikiwa imechelewa kuwafikia wakulima na kusababisha mazao kuharibika.

Pamoja na kuchelewa kwa mbolea, amesema wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakiisafirisha katika nchi za jirani za Zambia na Malawi ambako wanaiuza kwa bei kubwa tofauti na zilizoelekezwa na serikali.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mbolea ya ruzuku inayopelekwa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imekuwa ikivushwa kwa magendo katika nchi hizo za jirani ambako mfuko mmoja wa kg 50 unauzwa kati ya Sh 80,000 na Sh 100,000 kwa mbolea ya UREA.

Hivi karibuni Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wilaya ya Ileje mkoani Songwe ilikamata mifuko 300 ya mbolea yenye ruzuku ya serikali ikitoroshwa kwenda nchini Malawi kwa njia za panya.

Baada ya kukamatwa kwa mbolea hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Joseph Mkude, akaamuru wapewe wananchi 178 kutoka kaya maskini zinazonufaika na TASAF na vikundi 12 vya watu wasiojiweza.

TFRA wazungumza

Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA), Lazaro Kitandu, amesema kwa mwaka huu kumekuwa na ongezeko kubwa la uingizaji wa mbolea tofauti na miaka iliyopita.

Kitandu amesema mbolea ya kukuzia aina ya UREA ambayo ndiyo inatumika kwa wingi hapa nchini imeingizwa tani 140,000 na kiasi hicho ni ongezeko kubwa sana.

Amesema miaka yote iliyopita wakulima walikuwa wanategemea mbolea ya ruzuku, lakini kwa mwaka huu hakuna ruzuku iliyotolewa na serikali.

Amesema pamoja na kutokuweko kwa ruzuku, mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti bei na kuleta unafuu kwa wakulima nchini.

“Mbolea ya UREA ni dili sasa, na udhibiti wa bei umefanyika kwa kiwango kikubwa sana, kwa mwaka jana zilitumika tani 90,000 kwa nchi nzima.

“Sumbawanga, Kalambo na Songwe mbolea ilikuwa inatoroshwa nje ya nchi na tatizo liko kwa wakuu wa mikoa ambao wamekuwa wakijitoa katika kazi ya kudhibiti utoroshaji wa mbolea,” amesema Kitandu.

Hata hivyo amesema awali inaonyesha kulikuwa na matumizi mabaya ya ruzuku na isipokuwepo mawakala wanaojitokeza wanakuwa wachache kwa madai kwamba hawawezi kupata faida.

Amesema mamlaka hiyo pekee haiwezi kudhibiti utoroshaji wa mbolea ambapo kwa nchi ya Zambia mbolea aina ya UREA inauzwa zaidi ya Sh 70,000 wakati hapa nchini inauzwa kwa Sh 44,000.

Amesema mbolea ya UREA ilifikishwa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Oktoba mwaka jana huku Mkoa wa Songwe ukipata tani nyingi kuliko historia ya miaka yote iliyopita, lakini ikawa inatoroshwa kwa magendo nje ya nchi.

Amesema awali ilikuwa inaelezwa kuwa mahitaji ya mbolea kwa mkoa huo pekee ni tani 40,000 na hizo ni hoja za kisiasa ambazo hazina ukweli wowote.

Amesema mahitaji halisi ya mkoa huo ni tani 8,000 za mbolea na kwamba kiasi hicho kilifikishwa kwa wakati na si tani 6,000 zinazodaiwa kufikishwa mkoani humo.

Kitandu ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka huu zimeingizwa tani 430,000 za mbolea za aina zote nchini na kwamba serikali haijahusika na usambazaji kwa kuwa haikutoa fedha za ruzuku.

TFRA imesajili mawakala 311 na kutoa vibali 172 vya kuingiza mbolea nchini, lakini inaelezwa kuwa kuna mgomo wa mawakala baada ya serikali kutowalipa fedha zao za usambazaji wa mbolea katika msimu wa 2015/2016.

Hadi Machi, 2017 tani 297,000 ziliingizwa nchini na kati ya hizo tani 140,000 zilikuwa ni mbolea ya kukuzia na tani 74,000 za mbolea ya Minjingu iliyopelekwa nje ya nchi katika nchi za Kenya, Uganda na Afrika Kusini.

 

Matumizi ya mbolea nchini

Pamoja na Tanzania kuwa ni nchi yenye matumizi ya chini sana ya mbolea katika ngazi ya wakulima wadogo (smallholder farmers) barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, imeshindwa kuongeza matumizi ya mbolea.

Katika Azimio la Maputo (The Maputo Declaration 2003), liliazimia masuala mbalimbali katika kilimo na kuongeza matumizi ya mbolea katika eneo la ukanda wa SADC angalau kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta.

Tanzania imefikia kiwango cha kilo 19 tu za virutubisho kwa hekta, ikiwa ni sawa na asilimia 38 ya lengo lililowekwa, na hicho ni kiwango cha chini sana kwa matumizi ya mbolea.

Wizara ya Kilimo na Chakula imeshindwa kuhakikisha kuwa mbolea inafika kwa wakati kwa wakulima na usimamizi wa matumizi sahihi ya mbolea.

Mwanzoni mwa mwaka huu Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, kuhakikisha anafikisha mbolea ndani ya wiki moja katika mikoa ya Ruvuma na Katavi na mbolea hiyo ilifikishwa kwa wakati sawa na agizo la rais.

Na iwapo hatua zozote hazitachukuliwa mapema kuhakikisha kuwa wananchi wanapata pembejeo kwa wakati ikiwemo mbolea za kupandia na kukuzia, majanga ya njaa hayawezi kuepukika nchini.

Imeandikwa kwa hisani ya Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).

By Jamhuri