Mkuu wa Wilaya (DC) ya Magu mkoani Mwanza, Dk. Philemon Sengati, ameamuru kukamatwa kwa mkazi wa Kijiji cha Shilingwa, Julius Makolobela, anayetuhumiwa kuwatishia maisha wananchi katika eneo hilo.

Uamuzi wa DC Sengati umekuja siku moja baada ya Gazeti la JAMHURI kuandika kwa urefu matukio ya wananchi kuuawa, kujeruhiwa na wengine kukimbia kijiji hicho na kwenda kuishi kwa diwani wakihofia kuuawa.

Katika mkutano wa hadhara ulioitishwa kijijini hapo mwishoni mwa wiki iliyopita, watu tisa wakiwamo ajuza na vikongwe walijitokeza mbele ya DC kueleza namna walivyonyang’anywa mashamba na wanavyotishiwa kuuawa.

Wananchi hao wote walimtuhumu Makolobela kuwa ndiye anayewafanya waishi kwa hofu. Wanadai kuporwa ardhi yenye ukubwa wa jumla ya ekari 100.

Makolobela alikamatwa mkutanoni kwa amri ya DC ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Magu. Hata hivyo mtuhumiwa huyo aliachiwa saa 24 baadaye.

DC aliwataka waliotishiwa maisha wajitokeze na wasimame nyuma ya mtu waliyemtuhumu, ndipo Agnes Lushinge, Monica Jacob, Debora  Lushinge, Agnes Genge, John Simakubela, Simon Shagembe, Lukanya Kidai, Kawawa Lubala na Tabiza Genge (72), walipofanya hivyo.

Wiki iliyopita JAMHURI liliripoti kuwa baadhi ya wananchi wa vijiji vya Shilingwa na Kongolo walikuwa wamekimbia makazi yao wakihofia kuuawa kwa sababu za kishirikina na migogoro ya ardhi.

Makolobela alipopewa fursa ya kuzungumza kwenye hadhira alikanusha tuhuma hizo.

Miaka kadhaa iliyopita wazee hao walimfungulia kesi Makolobela katika Mahakama ya Mwanzo Kongolo wakipinga kuporwa mashamba yao.

Kesi hiyo baadaye ilihamishiwa Mahakama ya Mwanzo Kisesa, Wilaya ya Magu na wazee hao walishindwa.

Oktoba 2, mwaka huu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Magu, E.P. Kente, aliandika barua akimtaja Makolobela kuwa mmiliki halali wa shamba hilo. Barua hiyo ilielekezwa Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Shilingwa.

Katika barua yake, Hakimu Kente, anasema: “Mgogoro juu ya umiliki wa shamba tajwa ulishaamuliwa na Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Ardhi ya Kijiji cha Kongolo mnamo mwaka 2005 na Bwana Julius Makolobela alithibitishwa kuwa mmiliki wa shamba hilo.

“Hakukuwa na rufaa juu ya maamuzi (uamuzi) hayo kutoka kwa Bwana Lukanya Kidai na wenzake na walipoingia kwenye shamba hilo (Criminal Trespass), walikutwa na hatia na waliachiliwa katika hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Kisesa. Adhabu yao iliendelea kuimarishwa na Mahakama ya Wilaya katika Rufaa Namba 4/2012.

“Hivyo, kwa maamuzi hayo suala hili si mgogoro tena kwani maamuzi juu ya nani mmiliki yalishatolewa na wahusika waliridhika nayo. Kitendo cha kuibua suala hili ambalo lilishakwisha ni kuendekeza migogoro isiyofika mwisho bila sababu za msingi.

“Kwa barua hii, naagiza yafuatayo; Mwananchi huyu (Makolobela) aruhusiwe  kuendelea kutumia shamba lake bila bughudha. Pili, Bwana Lukenya Kidai afuate njia zilizopo kisheria kupinga uamuzi uliotolewa miaka mingi iliyopita na vyombo vilivyopo kwa mujibu wa sheria,” amesema hakimu.

Wazee watatu; Lukanya Kidai, Tabiza Genge na John Simakubela, bado wanashikilia msimamo wao kuwa shamba linalotajwa ni lao, hivyo hawakubaliani na uamuzi wa mahakama.

Mmoja wa wazee hao anasema mbinu zilitumika kuwapora mashamba yao kwa sababu ni maskini na hawana elimu.

Wakati huo huo, wiki iliyopita Mahakama ya Mwanzo Nyanguge, Wilaya ya Magu, ilimtia hatiani Makolobela kwa kosa la kutishia kuwaua Tabiza Genge (72) na Lukanya Kidai, kwa sababu ya mgogoro wa mashamba.

Makolobela amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja na kufanya kazi ngumu. Kesi hiyo ilifunguliwa na wazee hao Septemba, mwaka huu baada ya kukimbia kijijini kwao na kwenda kuishi kwa Diwani wa Kongolo, Herbert Faustine, wakihofia usalama wao.

Makolobela huenda akashtakiwa tena baada ya kushutumiwa mbele ya DC na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Magu Oktoba 24, mwaka huu akidaiwa kutishia kuua.

Tabiza aliyepoteza uwezo wa kuona kwa miaka zaidi ya 10, amemtaja Makolobela kuwa amemnyang’anya mashamba yake na kutishia kumchomea ndani ya nyumba.

Anadai kuwa alitishiwa baada ya kuwasilisha malalamiko kama hayo kwa Mbunge wa Magu, Kiswaga.

“Mashamba yangu nimenyang’anywa na Makolobela. Alikuja akaniambia nitakuchomea ndani ya nyumba iwapo utaendelea kulalamikia mashamba,” amesema Tabiza huku akiomba haki itamalaki mbele yake na wazee wengine.

Mzee Lubala anasema amekimbia kijijini baada ya kutishiwa maisha na mtuhumiwa.

Simon Shagembe pia anadai alikwishakimbia kijijini Shilingwa baada ya kile alichodai kutishiwa kuuawa na Makolobela.

Makolobela ametajwa pia kwenye hukumu ya kesi ya jinai Na. 49/2012 katika Mahakama ya Mwanzo Nyanguge, Wilaya ya Magu dhidi ya Karabaga Julius na Simon Shagembe. Hukumu ilisomwa na Hakimu R. Amos Mei 31, 2012.

Katika kesi hiyo alikuwa shahidi wa Karabaga ambapo mahakama ilimwachilia huru Shagembe.

 “Tusaidie mzee (DC). Ardhi yangu kuna makaburi. Mama amezikwa humo, mama mkubwa amezikwa humo,” anasema Shagembe.

Anasema mashamba ni yake, kwani amezika humo ndugu zake wanne: mama yake mzazi, bibi, mjomba na mama yake mkubwa.

Agnes Genge (52) anasema amenyang’anywa shamba lake miaka 20 iliyopita, na kuwa amezuiwa kuzika ndugu zake ndani ya eneo hilo la ekari tatu.

“Kwa sasa mheshimiwa mkuu wa wilaya ulivyokuja hapa, kama alivyokuja mbunge (Mbunge wa Magu, Bonaventura Kiswaga) tukasema malalamiko haya, wengine wakaanza kutishiwa kuuawa.

“Kwa hiyo, najitoa kwako kama ulivyosema tusiwe na wasiwasi, naomba shamba langu baba kama kuna uwezekano nirudishiwe. Nina imani hata kuuawa sitauawa kwa kauli uliyoitoa hapa,” amesema John Simakubela.

DC Sengati amesema Kata ya Kongolo ina matukio yanayotishia usalama wa raia.

“Kumekuwapo matukio ambayo si mazuri kipindi cha nyuma na kwa bahati mbaya bado yanajitokeza. Na vyombo vya habari vimekwisha kuandika matukio kadha wa kadha.

“Lakini, naamini mtaniambia zaidi. Napenda sana nisikie kutoka kwenu. Ila niwahakikishie kitu kimoja, wilaya na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tupo imara kweli kweli kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi mzee au kijana au mtu wa makamo anaishi kwa hofu. Na wanaojihusisha na hayo mambo ninawaomba na ninawaelekeza waache mara moja, la sivyo sheria, kanuni na miongozo mbalimbali vya kuwashughulikia vitaanza kufanya kazi mara moja,” amesema DC Sengati.

Amewataka wananchi wa Kongolo waishi bila bughudha. “Nataka mjenge taswira mpya. Nataka kuanzia leo (Oktoba 24, 2018) nisikie na nipate taarifa za Kongolo iliyo safi, Kongolo iliyojaa amani, Kongolo iliyojaa upendo na mshikamano,” amesema DC Sengati.

By Jamhuri