Wiki iliyopita makala hii iliishia pale iliposema kesho ya mtoto  inajengwa na leo, methali ya Kiswahili inatukumbusha maneno haya: “Samaki mkunje angali mbichi.”

Itakuwa ni biashara isiyolipa kumkunja samaki akiwa mkavu. Atavunjika, utapata hasara ambayo pengine hukutegemea kuipata. Nakubaliana na Frederick Douglass kusema: “Ni rahisi sana kujenga watoto imara kuliko kukarabati watu wazima waliovunjika.”

Mzazi unatakiwa uwe mlezi saa ishirini na nne, unatakiwa uwe mlezi siku saba za wiki, unatakiwa uwe mlezi siku 30 za mwezi, siku 365 za mwaka. Malezi hayana likizo, ni utumishi.

Malezi bora ndiyo yanayowaandaa watoto kifikra na kitabia, tafakari kesho ya mwanao umeiandaaje? Elewa kwamba wewe ni mzazi na mlezi, timiza wajibu wako.

Malezi ni kulea, mzazi au mlezi unapomlea mtoto wako usisahau kujilea. Maisha unayoishi wewe mzazi yana maana kubwa sana kwa wanao kuliko maneno unayowaambia.

Padri Anton wa Padua, aliyeishi karne ya 14 kila alipokuwa akianza mahubiri alikuwa anawaambia waumini wake maneno haya: “Matendo yanaongea zaidi kuliko maneno.” Maneno yanafutika, si matendo.

David Oyedepo amepata kuandika haya: “Wazazi wanapaswa kuwaongoza watoto wao, huku wao wakiwa mfano bora kwa matendo yao, kwa kuwa watoto huiga kile kinachofanywa na wazazi wao.”  Watoto huwaiga wakubwa. Je, maisha unayoishi yana mfano gani kwa watoto wako?

Mwanafalsafa Tolmons alipata kuandika hivi: “Katika maisha unayoishi unaweza kuonyesha sura ya Mungu au sura ya shetani.”  Kazini kwako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura ya Mungu.  Kwenye familia yako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura ya Mungu.

Kwa majirani zako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura ya Mungu.  Inategemea maisha yako unayoishi yanawakilishwa na matendo ya aina gani.

Vivyo hivyo katika maisha unayoishi unaweza kuwa chachu ya mabadiliko ama mhanga wa mabadiliko. Tupembue tuone,  ufisadi ni sura ya shetani, rushwa ni sura ya shetani, uchu wa madaraka ni sura ya shetani.

Uchawi ni sura ya shetani, uchoyo ni sura ya shetani, umbea ni sura ya shetani, udini ni sura ya shetani, biashara haramu  kama  ya dawa za kulevya ni sura ya shetani.

Wizi wa pembe za ndovu na meno ya tembo ni sura ya shetani, ukahaba ni sura ya shetani. Kwa upande mwingine pia tuone Mungu anawakilishwa na sura ya namna gani.

Sura ya Mungu ni sura ya uadilifu na uaminifu, upendo. Sura ya Mungu ni sura ya amani na mshikamano.  Sura ya Mungu ni sura ya unyenyekevu na huruma.

Leo unaposoma makala hii, chagua unapenda maisha yako yawakilishwe na sura ipi? Sura ya Mungu au shetani? Ulimwengu unalia kwamba maadili yameporomoka.

Kwa uhalisia wake ni kweli maadili yameporomoka. Lakini kwa nini maadili yameporomoka? Nani alaumiwe, mtoto au mzazi? Viongozi wa dini au wazazi?

Kwa hakika mimi na wewe hatuwezi kukwepa kujibu swali hili. Chanzo cha maadili kuporomoka katika jamii yetu ni nini?

Ni ukweli usiohitaji hoja kwamba wanaoharibu ulimwengu kwa matendo yao maovu hawajatokea vichakani wala kuzaliwa na wanyama, bali wametokea kwenye familia zetu.

Lakini kwa nini wamegeuka kuwa magaidi? Kwa nini wamegeuka kuwa mashoga? Kwa nini wamegeuka kuwa mafisadi? Kwa nini wamegeuka na kuuza miili yao?

Nani amewaandalia mazingira haya? Ni mimi au wewe?

591 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!