Kama ilivyo ada ya muungwana, salamu ni jambo muhimu sana kwa msomaji wa safu hii ya kizuzu. Utakubaliana nami kwamba sijawahi kuacha kuwajulia hali.

Hii inatokana na mafunzo niliyopata nikiwa kinda kwa wazazi wangu na mwishowe mafunzo ya uzalendo kwa mujibu wa sheria ya serikali yangu wakati nilipomaliza shule.

Watu wengi hawawezi kuelewa nitazungumzia nini katika waraka wangu wa leo kwa sababu hawajapata fursa ambazo wakongwe tulizipata kwa kwenda katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, wakati ule jeshi hili lilikuwa linajenga taifa kwa maana ya uchumi, chakula, utu, uzalendo na uwajibikaji.

Wakati wetu kuwa jeshini ilikuwa ni zaidi ya masomo ambayo tulipata darasani, yapo ambayo tulikumbana nayo kwa vitendo na mengine tulijifunza hapo kwa kukosa kuyapata madarasani.

Naamini na nitaendelea kuamini kuwa kuacha mambo ya JKT au kuyafupisha mafunzo yale ndiyo moja ya matokeo ya kutokuwa wazalendo na kupenda kupata maisha bora bila kutoa jasho.

Nimepitwa na mengi na hata sijui nimuombe nani anisaidie kwa sababu nyingi, lakini mojawapo nauona muingiliano wa kutojua ni nani mwenye dhamana ya kusimamia suala hili kwa sasa, huenda ni wizara fulani au mhimili fulani au mamlaka fulani, kiukweli sijui, lakini naomba ujumbe uwafikie wenye dhamana.

Sisi tulifundishwa umuhimu wa uzalendo na makamanda wetu ambao walitujenga katika mfumo wa kuona kila kitu kinakuhusu kama raia, tulijengwa kuipenda nchi yetu kwa moyo na vitendo, tulibatizwa kwa nyimbo za ukombozi na kulipenda taifa letu, wakati huo ukisikia wimbo wa taifa unatamani kuangalia juu na kuona malaika wakishuka.

Jeshi lile lilikuwa la kitaifa, mnakutana langoni bila kujuana na kuanzia hapo mnakuwa kitu kimoja, umoja wa kitaifa unaanzia hapo, humjui katokea wapi, kabila gani, kasoma wapi, kaletwa na nani.

Lakini mtaimba wimbo mmoja na kuwa kitu kimoja, mtakula pamoja, mtalala pamoja na kuamka pamoja, mtalia pamoja na kucheka pamoja, mtachoka wote na mtaimba wote, huo ndio ulijenga taifa hili hadi mwishoni mwa miaka ya themanini.

Watu wasiojua watauliza tulifundishwa nini? Tulifundishwa kufanya kazi, hatukufundishwa kuwa nyoronyoro, kaulimbiu ya sasa kwetu siye wa JKT ni kama mate na ulimi. Tulilima mashamba ya ‘Dunia’ na kuvuna, tulipalilia shamba la ‘Mungu’ na kuvuna, taifa halikuwahi kuingiwa njaa, tulikuwa na chakula cha kutosha na serikali iliuza na kupata fedha.

Huwa sielewi ni wapi tulikosea kisera kuifuta hii, na huwa sielewi kwanini waliopitia mafunzo haya hawaoni hili ombwe la kukosekana kwa mafunzo yale, labda ni kutokana na uzuzu wangu sijui gharama za kuliendesha jeshi ambalo lilikuwa likijenga nchi wakati huo.

Ukiuliza tulifanya nini? Majibu utapata kwa aliyepitia jeshi lile, lakini tulifunzwa nidhamu ambayo vijana wengi wa leo hawana, utaambiwa juu ya umuhimu wa kutii sheria na uwajibikaji, utaelezwa juu ya kufanya kazi na uimarishaji wa afya.

 Mwishowe utafahamishwa juu ya kujenga umoja wa kitaifa na uzalendo halisi na si huu wa kuimbaimba midomoni kwa kukariri bila vitendo, hiyo ndiyo JKT niliyopitia mimi.

Kwanini ilifutwa? Jibu sina na sijawahi kuambiwa, lakini ninachojua ipo ya kujitolea kwa vijana wasio na kazi na kwa mujibu wa sheria lakini kwa siku chache, haijawa sheria kama wakati wetu kwamba bila JKT hauna haki ya kuajiriwa na hauna haki ya kuendelea na masomo.

Kwa uzuzu wangu, naona faida zake zilikuwa ni nyingi kuliko hasara na kwa ubwege wangu ningeshauri zoezi lile lirudishwe ili lijenge taifa mbalo kwa sasa linahitaji vijana wachapakazi, wazalendo, wawajibikaji na wanaozingatia sheria, zoezi lile lilituletea viongozi wa taifa na hata pale ambapo kiongozi aliteuliwa na hakupitia jeshi lile alilazimika kwenda kusafisha nyota ya Utanzania.

Najua nitawakera lakini ukweli lazima niuseme, hatuna wazalendo wa kutosha na tuna watu ambao hatuna hakika kama ni Watanzania, kwa kuwa hawakupita katika chekecheke na chujio la taifa. Naomba mniwie radhi, sikufundishwa JKT kuwa mwoga.

Wasalamu,

Mzee Zuzu, 

Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share