Miaka mingi iliyopita wapenzi wa soka walizoea kuona kila aina ya tuzo katika mchezo wa soka ikichukuliwa na wachezaji kutoka ukanda wa nchi za Afrika Magharibi, hali ambayo imeanza kubadilika katika siku za hivi karibuni.

Hali hiyo imejidhihirisha katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora anayecheza ndani barani la Afrika inayoshikiliwa na Mtanzania, Mbwana Samatta, ambaye sasa anacheza katika klabu ya  Genk ya Ubelgiji.

Katika mtifuano huo, wachezaji wanne wa klabu ya Mamelodi Sundowns wameingia fainali, hao ni Khama Billiat, raia wa Zimbabwe, Keegan Dolly, Hlompho Kekana wote raia wa Afrika Kusini na Denis Onyango wa Uganda ambao watachuana na mchezaji mmoja wa TP Mazembe, Rainford Kalaba, wa Zambia.

Katika hatua ya mwisho kura zitapigwa na makocha wakuu wa timu za taifa za nchi 54 wanachama wa CAF, zikiwamo wanachama washiriki kama visiwa vya Reunion na Zanzibar pamoja na Wajumbe 10 maalumu.

Usiku wa tuzo za CAF 2016 utafanyika Januari 5, 2017 mjini Abuja, Nigeria chini ya udhamini wa kampuni ya simu ya Globacom.

Samatta hajaingia kutetea tuzo ya Mwanasoka Bora anayecheza Afrika baada ya kuhamia katika klabu ya  KRC Genk ya Ubelgiji mapema mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC.

Hatua hiyo ya wachezaji wa ukanda huu kuitawala tuzo hiyo wadadisi wa soka wanasema imechangiwa na kufanya vyema kwa baadhi ya klabu vya ukanda  huu kama TP Mazembe na Klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika ya Kusini.

Wakati hayo yakiendelea Mwanasoka Bora wa Bara la  Afrika Piere Emerick Aubameyang raia wa Gabon anayecheza katika klabu ya Borrusia Dortmund ya  Ujerumani anatarajiwa kutetea tuzo yake dhidi ya wachezaji 5 wanaocheza katika timu mbalimbali barani Ulaya.

Wachezaji hao ni  Riyad Mahrez na Islam Slimani wote wa Leicester City ya England, wengine wanaowania tuzo hiyo ni Sadio Mane wa Senegal wa klabu ya  Liverpool na Mohamed Salah wa Misri kutoka klabu ya Roma baada ya kupigiwa kura na Wajumbe wa Kamati ya Habari ya CAF, Kamati ya Ufundi na Maendeleo na nusu ya Wajumbe 20 maalumu.

Hiyo ni baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutoa orodha ya wachezaji watano wa mwisho wa kuwania tuzo hiyo.

 

Taarifa hii imeandaliwa kwa msaada wa mitandao ya kimataifa ya Voa, News24, BBC

By Jamhuri