Wadau na wapenzi wa mchezo wa kuogelea nchini, wameombwa kutoa michango yao ya hali na mali kuhakikisha mchezo huo unapiga hatau kwa manufaa ya Taifa pamoja na changamoto zilizopo ikiwamo uhaba wa vitendea kazi.

Akizungumza na JAMHURI wakati wa kufunga mafunzo ya ukocha wa kuogelea yaliyofanyika katika bwawa la kuogelea la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katikati ya wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Ufundi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Suleiman Jabir (pichani), anasema makocha hao wanapaswa kwenda kueneza mchezo huo huko waendako hasa kuanzia ngazi ya chini.

Anasema pamoja na changamoto mbalimbali watakazokabiliana nazo huko waendako, lakini Taifa linawategemea wao katika kuhakikisha mchezo huo unaanza kuota mizizi kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.

Anasema mchezo wa kuogelea ni miongoni mwa michezo pendwa hapa nchini na duniani kote, na umewawezesha baadhi ya wachezaji kuwa matajiri ndani ya nchi zao na kutoa ajira kwa watu wengine hasa katika nchi zilizo na miundombinu mizuri ya mchezo huo.

“Tunaelewa nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto nyingi hasa ya mabwawa ya kufanyia mazoezi yanayokidhi viwango vya kimataifa, lakini tuendelee kuvitumia hivi vichache tulivyonavyo hadi hapo tutakapojitosheleza,” anasema Jabir.

Anasema katika siku za hivi karibuni, Kamati ya Olimpiki, kwa kushirikiana na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), imekuwa ikijitahidi kuhakikisha idadi ya makocha wa kuogelea wanaongezeka kwa manufaa ya mchezo wenyewe, hali ambayo imeanza kuonesha matumaini kwa vijana wengi kuanza kushiriki.

“Pamoja na ongezeko hili la walimu wa mchezo huu katika miaka ya hivi karibuni, niwaombe wadau wa mchezo huu waliopo ndani na nje ya nchi kutuunga mkono katika juhudi zetu za kukuza mchezo huu kuanzia ngazi ya chini,”anasema mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo wa ufundi alisisitiza kuwa wahitimu wanatakiwa kuwa wavumilivu na kujitoa zaidi katika mchezo huo, ili kuufikisha mbali kwa maana ya kuwaandaa wanafunzi kuwa washindani katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Naye mratibu wa mafunzo hayo, Noel Kiunsi, aliwaasa wahitimu hao kuwa ujuzi walioupata uwe ni chachu ya maendeleo ya mchezo huo hapa nchini kwa manufaa mapana ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Tunajua twendako tutakutana na changamoto za ukosefu wa vitendea kazi, lakini niwaombe hali hiyo isiwavunje moyo… tuendelee kupambana hadi tone la mwisho kuhakikisha mchezo unakua,” anasema Kiunsi.

Akitoa neno kwa niaba ya washiriki, Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhan Namkoveka, aliwashukuru waandaaji wa kozi hiyo kwa kusema itawasaidia katika maandalizi yao ya kushiriki Olimpiki ya Tokyo 2020.

“Hii sasa ni changamoto kwenu wahitimu kuhakikisha Tanzania inapata washindani wa kweli katika mashindano ya ndani ya kimataifa, hili litawezekana tu pale wote kwa pamoja tutakapounganisha nguvu kwa lengo la kuunyanyua mchezo huu,” anasema Namkoveka.

Anasema mchezo wa kuogolea umekuwa maarufu sana na umekuwa ukichezwa duniani kote hadi kujizolea mashabiki wengi kila kukicha, na kuchangia kwa kiwango kikubwa kukabiliana na tatizo la ajira duniani.

“Mchezo huu unakuwa na watazamaji wengi kwenye mashindano makubwa kabisa ya Olimpiki na mengine kama Commonwealth, All Africa Games.

‘’Hapa nchini unafundishwa na kuchezwa, lakini umekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa na mabwawa yenye viwango vya kimataifa kwani yaliyopo ni ya zamani yenye mita 25 na 33 yasiyotambulika kwenye mashindano ya kimataifa, na kusababisha washindani wetu kutofanya vizuri,” anasema Namkoveka.

Anasema chama mara nyingi hulazimika kupeleka timu ya Taifa kufanya mazoezi nje ya nchi kama Kenya au Zambia zenye mabwawa yanayokidhi vigezo ambako TSA inalipa Sh 5,000 za Kitanzania kwa kila mchezaji anayeshiriki mazoezi – ni gharama kubwa.

Jumla ya makocha 28 walihudhuria mafunzo hayo yaliyotolewa na mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Kuogelea (FINA), Joshua Neuloh, wa Ujerumani.

Wanafunzi walipewa mafunzo mbalimbali ya nadharia na vitendo kwa kupitia udhamini wa Olimpics Solidarity kwa ushirikiano na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) pamoja na TSA.

1502 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!