Sakata la usafirishaji gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam lilipoanza, sikusita kuunga mkono madai ya wana-Mtwara. Kuna kundi la viongozi na wananchi waliothubutu kupotosha ukweli wa madai ya wananchi hao.

Wakasambaza taarifa za upotoshaji wakisema Mtwara hawataki gesi isafirishwe kwenda Dar es Salaam. Huo ukawa upotoshaji uliolenga kuwafanya Mtwara waonekane wanataka kuigawa nchi. Hiyo haikuwa dhamira yao. Wao walichotaka kujua ni, “mnatuachaje?”

 

Mtwara wameonesha njia. Wameuthibitishia umma kwamba Serikali ikibanwa, inaweza kutoa majibu hata kama si ya kiwango stahiki. Zama za ubabe na majibu ya kejeli zimekwisha.

 

Balozi wa Finland hapa nchini, Sinikka Antila, ametusaidia kwa kuwaambia watawala, “Nyaraka za Serikali ziwe wazi kwa kila mtu anayetaka kujua kitu kinachofanyika ndani ya Serikali na hii itasaidia kuendeleza uchumi mbele.”

 

Wengi wamekiri kuwa chanzo cha vurugu za Mtwara ni usiri na ujuaji wa watendaji serikalini. Bahati mbaya ni kwamba watawala katika nchi hii wanadhani kwa kuwa wao ni viongozi, basi ndiyo pekee wenye akili kuliko wananchi makabwela na wasomi wasio viongozi. Kwao, mtu aliye nje ya Serikali huyo hana akili! Mtwara imethibitisha kuwa mtazamo huo ni potofu.

 

Wito wangu ni mmoja – nao ni kuona moto huu wa Mtwara unagusa kila kona ya nchi yetu na kwa kila nyanja ya kiuchumi.

 

Ninapozungumzia moto, ninamaanisha ujasiri wa wananchi kuhoji mambo yenye mustakabali wa maisha yao kiuchumi. Kuhoji mambo na kupewa majibu ya kina ni haki yao kikatiba. Wananchi wanaoishi kando ya migodi kama kule Nyamongo, Geita, Nzega, Buhemba, Kyabakari, Murangi, Mirerani, Buzwagi, Bulyanhulu, Tulawaka na kila kunakopatikana madini, wana haki ya kuhoji namna watakavyofaidika kwa utajiri katika maeneo yao.

 

Haiwezekani maeneo kama Buhemba waletwe majizi kwa kivuli cha uwekezaji, wakombe madini, waondoke bila kuacha japo zahanati, halafu wananchi haki yao iwe kukaa kimya tu bila kuhoji. Hapana.

 

Haiwezekani samaki wavuliwe kwa wingi, minofu isafirishwe kwenda kwa “walaji wa maana” walioko Ulaya, na haki ya wananchi waishio kando ya maziwa, mito na bahari iwe kuambulia mapanki! Mwananchi yeyote anayekubali kukaa kimya bila kuhoji unyanyasaji wa aina hiyo, atakuwa amepoteza tunu ya ubinadamu.

 

Narejea kuwapongeza wana-Mtwara kwa ujasiri wao. Wamemfanya hata Mzee Benjamin Mkapa, aibuke na kukalia kiti cha u-statesman. Haiwezekani nchi yenye marais wastaafu, mawaziri wakuu na watu maarufu wengi tu iwe haina wa kusema lolote kunapotokea mambo makubwa yanayolihusu Taifa letu.

Hasira tulizoshuhudia, ni za gesi tu?

Ndugu zangu, wakati vurugu zikitokea katika mikoa ya Mtwara, Morogoro, Pwani, Kagera na kwingineko nchini, kuna mambo tunayopaswa kujiuliza.

 

Mjini Mtwara tuliambiwa kuwa chanzo ni gesi. Mjini Masasi chanzo kikawa bodaboda – nyumba za viongozi na dola zilichomwa. Dakawa mkoani Morogoro kukawa na vurugu zilizosababishwa na ugomvi kati ya wakulima na wafugaji. Barabara kuu ya Morogoro-Dodoma ikafungwa kwa saa kadhaa. Kagera kumekuwapo matukio ya kuuawa kwa polisi na pia raia.

 

Je, kuna kitu gani nyuma ya vurugu hizi? Je, haya ni matokeo ya wananchi kujiona huru zaidi na hivyo kuamua kufanya lolote wanalotaka kulifanya? Uhuru gani wa waendesha bodaboda kukataa kukaguliwa leseni? Je, haya ni matokeo ya kukata tamaa kwa wananchi, hasa vijana? Je, ni ulegelege wa wasimamizi wa sheria katika Taifa letu? Kuna nini hasa nyuma ya vurugu hizi?

Tunaweza kujiuliza maswali mengi, lakini lililo dhahiri ni kwamba wananchi wamekosa imani na vyombo vya dola. Kwa mfano, ni wapi wananchi hawa wametoa ujasiri wa kuvamia vituo vya polisi wakitaka kuwachukua watuhumiwa ili wao wawahukumu? Kwanini wananchi wachome majengo ya mahakama?  Kinachoonekana hapa ni wananchi kutokuwa na imani kwa polisi na mahakama.

 

Watuhumiwa wanakamatwa. Wanafikishwa polisi na hata vizimbani. Katika matukio ya wazi na yenye ushahidi unaojitosheleza, mara nyingi watuhumiwa wengi wameachiwa huru kwa namna ambayo hata wakulima wasio wanasheria wanaona kuna walakini.


Isitoshe, wananchi wanaposoma na kusikiliza katika redio na kutazama kwenye televisheni, hawakosi kupata taarifa za polisi na wanajeshi kukamatwa wakiwa na nyara za serikali, bangi, dawa za kulevya na matukio ya kihuni ya kugawana fedha zilizoporwa na majambazi –  wanakosa imani na walinzi hao.


Waendesha bodaboda wana hasira kwa sababu wanaonewa. Wanalazimishwa kutoa rushwa. Wamechoka. Wanabambikiwa kesi, ndiyo maana wakipata mwanya wanaamua kuwashughulikia polisi kweli kweli.

 

Kwanini nyumba za viongozi zinachomwa? Nyumba zinachomwa kwa sababu wananchi wa kawaida wanawaona viongozi wengi si wenzao. Wanawaona namna maisha ya wakubwa yalivyo tofauti na ya familia za makabwela. Wanaona wanaotibiwa India ni wao, ilhali Watanzania wengi masikini wakifa kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika. Wanaona viongozi wengi wa umma wamejipatia mali kwa njia za wizi, ubadhirifu, ulaghai na ufisadi.

 

Watoto wa wakubwa wanasafirishwa kwenye ma-STK ilhali wa makabwela wanasukumwa na pengine kufariki dunia kutoka kwenye daladala. Maelfu katika shule za kata wanakwenda na kutoka shuleni kwa kutembea. Tofauti ya maisha kati ya walionacho na wasionacho bila shaka ina mchango mkubwa kwenye vurugu hizi.

 

Tunaweza kutunga uongo wa kila aina ukiwamo kwamba vijana wanafanya vurugu kwa sababu wanahamasishwa na wanasiasa. Tunaweza kusema vurugu hizi ni mpasuko ndani ya CCM. Tunaweza kujitungia nadharia nyingi zinazohusu vurugu hizi; lakini tusisahau kujiaminisha kuwa hali duni ya uchumi na ukosefu wa matumaini miongoni mwa wananchi ni mambo yanayochochea tafrani hii katika kila kona ya Taifa letu.

 

Nchi yenye viongozi wanaokwepa kwa makusudi kujenga usawa; Taifa la watoto wanaosoma wakiwa 150 darasani na wengine wakiwa chini ya 45; Taifa la watoto wenye uhakika wa kula na kusaza, na wengine wakiwa wanatoroka shule ili wapate kuokota na hatimaye kuuza chupa tupu za maji ili wapate mlo, Taifa la aina hiyo haliwezi kuwa tulivu.

 

Hizi kuta zinazojengwa kuzunguka mahekalu yaliyopo Masaki, Oysterbay, Mikocheni, Kunduchi na kwingineko nchini, haziwezi kuuzima moto wa kudai haki utakapokuwa umewashwa na watoto wa makabwela waliopoteza matumaini. Kama kweli kuna amani na utulivu nchini, kuta hizi zinalenga kuwalinda dhidi ya nini? Kuombwa chumvi? Hapana

Tunapojadili na kulaani vurugu zinazotokea nchini, tunapaswa kujiuliza na kusaka vyanzo vya haya mambo. Kwa ufupi ni kwamba wananchi masikini wamekata tamaa. Hawana imani na uongozi na viongozi. Hawaoni mwanga mbele.


Hawana ajira. Kwao, vurugu itakuwa ni sehemu ya kujiliwaza dhidi ya umasikini unaowakabili. Hii ni hatari inayopaswa kushughulikiwa sasa.


By Jamhuri