Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kuandika makala hii na kuchapishwa katika gazeti hili mahiri ili kuelimisha na kuwajuza Watanzania nini kinajiri katika sekta ya madini.

Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali asilia ikiwemo ardhi, madini, misitu, wanyamapori, maji chumvi/maji baridi, samaki na viumbe hai wengine waishio majini, bioanuai na rasilimali watu. Nilihudhuria mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Umoja wa Mataifa Kamisheni ya Uchumi ya Afrika (UNECA), Addis Ababa, Ethiopia.

Ulihudhuriwa na watunga sera na wafanya uamuzi katika nchi za Afrika na ulizungumzia namna ya kuimarisha uchumi wa nchi za Afrika kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

Hata hivyo, ulipofika mjadala kuhusu rasilimali madini ilijitokeza sintofahamu. Nikashangaa wajumbe wengi waliposema “madini kwa Afrika ni ‘laana’, si ‘baraka’”. Waliosema walihusisha mikataba mibovu inayowapendelea wawekezaji; rushwa na kukosa uadilifu/utaifa na kuwapo usimamizi usioridhisha kwa sekta ya madini.

Mwito ulitolewa kwa viongozi wa Afrika kufanya mageuzi kwa kuweka vipaumbele thabiti, pia kuwa na mtazamo sahihi kuhusu rasilimali madini kwa faida na maendeleo ya Bara la Afrika.

Kutokana na matokeo ya mkutano huo ikaonekana ni vema Bara la Afrika likawa na mtazamo na mwelekeo mzuri kuhusu rasilimali madini. Hivyo, mwaka 2009 viongozi wa nchi kupitia Umoja wa Afrika (AU), wakapitisha “Maono ya Afrika kwa Rasilimali Madini.” (Africa Mining Vision – AMV). Nia ya kuwapo maono ya pamoja kwenye madini ni kuiwezesha Afrika kunufaika na rasilimali hiyo. Mei, 2019, Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) waliitisha mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi ya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wataalamu wa sekta ya madini.

Majadiliano yalilenga kuimarisha nchi katika kumiliki rasilimali madini na kujiletea maendeleo kupitia maono ya sekta ya madini ya Afrika ya mwaka 2009. Walishiriki watu zaidi ya 60 kutoka Tanzania, Botswana, Ghana, Kenya, Lesotho, Afrika Kusini na Uganda. Nilihudhuria mkutano huo kutokana na uzoefu wangu katika masuala ya uhifadhi mazingira na maliasili zetu.

Mkutano ulifunguliwa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko na uliongozwa na Profesa Ammon Mbelle wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kabla ya kufunguliwa rasmi, Mtendaji Mkuu wa Uongozi Institute, Profesa Joseph Semboja, akimshukuru Waziri Biteko na kusema uwepo wake ni kuwa amedhamiria kuinua sekta ya madini nchini. Akasema sera za madini na mikakati ya utekelezaji vinalenga kuwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali madini.

Naye, Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Natalie Boucly, katika maneno ya utangulizi alisema kwa miaka mingi Tanzania haijanufaishwa vya kutosha na rasilimali madini na mchango wake kwa uchumi umekuwa mdogo.

Hata hivyo alisema sera na mikakati ya sasa vitaiwezesha Tanzania kunufaika. Aliiomba serikali iangalie uwezekano wa kutumia gesi asilia kwa mahitaji ya kupikia ili kuokoa misitu ya asili ambayo ni tegemeo kubwa katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabia-nchi.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjilla, akimkaribisha Waziri Biteko kufungua mkutano alisema kuwa ni wakati sahihi kwa kampuni za kuchimba madini kujua fika taifa linataka nini na litanufaika vipi na rasilimali hiyo: kipi chema na kipi hakitufai ndani ya muda mfupi, wa kati na kwa muda mrefu.

Waziri Biteko alisema serikali iko makini kuona kuwa sekta ya madini inaweka mhimili imara kuiwezesha Tanzania kuwa na maendeleo endelevu kupitia usimamizi imara wa rasilimali madini na kuwapo uhusiano mzuri kwa sekta za umma na binafsi.

Akasema kuwa mafanikio yanategemea zaidi sera na mikakati madhubuti kuhakikisha sekta ya madini inasimamiwa na kuwawezesha wadau kuziheshimu na kufuata sheria, kanuni na taratibu. Vilevile alisisitiza kuwa lazima kuwepo mipango mikakati ya kuongeza ubora na thamani kwa madini kwa faida ya Watanzania wote.

Moja ya mawasilisho ya kitaalamu yalitolewa na Dk. Paul Jourdan kutoka Mintek-Afrika Kusini kwa kueleza kuwa maono ya Afrika kuhusu sekta ya madini ni suala muhimu. Alisisitiza kwamba kuwapo kwa madini ni jambo moja, lakini la pili ni kwa jinsi gani taifa linatumia madini hayo kujiletea maendeleo. Lazima kuwapo uhusiano wa kimaendeleo kati ya sekta ya madini na sekta nyingine. Alisisitiza kuwa madini yakiisha hakuna kusema kuna kurudia mara ya pili (no second chance). Iwapo mpango na vipaumbele vitakuwa si sahihi, taifa litabaki na mashimo na athari kubwa kwa mazingira.

Alihusisha uchimbaji wa madini na uanzishaji na uendelezaji wa viwanda kama kutengeneza mbolea, saruji, kusindika mazao ya kilimo au kutengeneza miundombinu kama barabara, umwagiliaji, uzalishaji umeme kupitia maji au gesi asilia, kujenga uwezo kwa nguvu kazi kupitia sekta za elimu na afya.

Kwa maneno mengine alimaanisha kuwa tunapofikiria kuchimba madini leo, tufikirie hali ya baadaye (kesho) itakuwaje baada ya taifa kuishiwa rasilimali madini.

Mawasilisho mengine yalihusisha pia kujifunza kutoka kwa wenzetu (case studies), hususan uzoefu kutoka Ghana, Nigeria na kwenye ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Kimsingi ilionekana kuwa hatua zinazochukuliwa na Tanzania ikiwamo utashi mkubwa kisiasa kuinua sekta ya madini kuwa tegemeo kwa maendeleo kiuchumi ni sahihi.

Tukioanisha maono ya madini Afrika na Sera ya Taifa ya Uchumi wa Viwanda pia kuiwezesha Tanzania kufikia kipato cha kati ifikapo mwaka 2025; ni dhahiri kuwa mchango wa madini haukwepeki. Ilisisitizwa tuongeze nguvu katika usimamizi kwa kuhakikisha sera na sheria vinatumika ipasavyo na kujenga uwezo wa kuinufaisha Tanzania kupitia rasilimali madini hatimaye kuwekeza kwenye miundombinu, kujenga uwezo wa nguvu kazi, kuhakikisha wawekezaji wanawajibika ipasavyo kuinua hali za maisha kwa jamii inayoishi karibu na migodi au viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye madini. Hayo yanapaswa kuingizwa kwenye mikataba.

Tukitumia madini yetu vizuri tutajenga mhimili imara kwa maendeleo endelevu kupitia uwekezaji katika sekta nyingine na hili ndilo suala ambalo serikali inakazana kulifanikisha kwa kutekeleza sera muhimu ya uchumi wa viwanda. Kutokana na hali hiyo, Watanzania kwa muda mfupi ujao tutaona rasilimali madini ni “Baraka” kwa nchi na si “laana”.

 

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri, Misitu Afrika. Anapatikana kwa namba 0783 007 400.

By Jamhuri