Siamini yupo binadamu anayekubali kwa hiari kuvumilia ubaguzi wa aina yoyote; kwa hiyo tunaposikia matamshi au kushuhudia vitendo tunavyohisi kuwa vya kibaguzi vinatuamshia mara moja hisia ya kujihami na hata kurejesha mashambulizi.

Nilikuwa abiria kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali, Rwanda nikienda kwenye mji wa Kigali nikasikia abiria mwenzangu akisifia usafi na mpangilio mzuri wa jiji hilo. Akaongeza: “Rwanda wamefanikiwa kufanya mambo ambayo maeneo mengine ya Afrika yameshindwa kabisa kufanikisha.”

Niliweka jitihada kubwa kujizuia kugeuka kumtizama abiria aliyetamka maneno hayo kwa lugha ya Kiingereza. Niliyasikia kama yana chembechembe ya kibaguzi ndani yake.

Maana moja ya kibaguzi ya “kushindwa kwa Afrika kufanya jambo” fulani ni namna nyingine ya kusema kuwa Waafrika hawana uwezo wa kufanya jambo lolote kwa ufanisi.

Baadaye niligundua kuwa aliyesema maneno yale ni raia wa Ghana. Mwafrika mweusi kama mimi, lakini mwenye lafudhi ambaye haikumtambulisha kuwa ni Mwafrika. Nilimdhania kuwa mzungu.

Mambo mawili yalinitokea mara moja. Kwanza, kuamini kuwa sikuwa nimesikia matamshi ya mbaguzi.

Na ufahamu huu ukanifunulia ukweli kuwa ningepata mengi sana ya kushutumu kwenye safu hii iwapo maneno yale yale yangetamkwa na, mathalani, mzungu.

Haikupita muda sana kuona kuwa yule raia wa Ghana alikuwa amezua mkanganyiko mkubwa zaidi kwangu kuliko nilivyodhania awali.

Kwamba Kigali ni mji msafi uliyopangwa vizuri na unaweza kuwa hauna mfano wake barani Afrika ni suala linalobeba ukweli kwa kiasi kikubwa. Kwamba Bara la Afrika lina miji mingi ambayo inakiuka kila kipengele cha mipango miji pia ni ukweli mtupu.

Kwa hiyo jambo la pili kunikabili ni kutafakari ni sababu gani ya msingi ukweli huo ukitamkwa na mzungu unakuwa ni tatizo kwangu, na unapotamkwa na mtu ninayemtambua kama Mwafrika sioni kuwa ni tatizo.

Sababu moja ni imani kuwa ndugu yako anapokusema hawezi kuwa na nia mbaya. Ni imani yenye kasoro.

Ni kujidanganya kuamini kuwa mzawa wa Afrika hawezi kuwa na hisia za kibaguzi kali zaidi dhidi ya wazawa wenzake hata kushinda wale ambao kwa kawaida tunawashuku kuwa wabaguzi.

Wapo Waafrika wengi wanaoamini kuwa wao wanafanana zaidi kitabia, kitamaduni, au kwa desturi na watu wa mabara mengine kuliko Waafrika wenzao, na baadhi yao wakijihisi kuwa wao ni bora zaidi.

Si ajabu kuwa yule raia wa Ghana alikuwa ni aina hiyo ya Waafrika; Mwafrika anayeonea aibu Uafrika wake, Mwafrika ambaye angepewa fursa ya kuamua angeamua kuzaliwa na rangi ya ngozi tofauti na aliyonayo.

Kinadharia, kama ndugu yangu wa Ghana anaweza kuwa kinara wa kukoleza fikra za kibaguzi zilizopo dhidi ya Afrika na watu wake, basi jambo lolote linawezekana.

Kwa hiyo hata wale tunaowadhania wabaguzi wanaweza kutamka jambo ambalo la kweli, lakini tutaliona ni la kibaguzi kwa sababu sisi wote – wabaguzi na tunaobaguliwa – tumezoeshwa kupima maisha ya binadamu kwenye mizani ya kibaguzi.

Hatuwezi kupata suluhisho la matatizo yote yanayotukabili, lakini tunaweza kupiga hatua moja halafu nyingine kuelekea huko kwenye maisha bora.

Kwa kuanza, nadhani ni muhimu kuyakubali kwanza matatizo yanayotukabili. Nimegusia mawili kwenye makala hii: ubaguzi na tatizo la mpangilio mbovu wa makazi ya mjini kwenye sehemu kubwa ya Bara la Afrika.

Wazanaki wana msemo kwamba anayeficha ugonjwa huumbuliwa na kifo. Unaanza kutafuta suluhisho la tatizo kwa kukubali kwanza kwamba tatizo lenyewe lipo, lakini tatizo haliishi kwa kubadili mada na kusema kuwa kuna ubaguzi mkubwa dhidi ya Waafrika.

Lakini la muhimu zaidi baada ya kubaini tatizo ni kufikia uamuzi kuwa tatizo hilo linahitaji suluhisho la kudumu.

Wote tukipita tumeziba pua mbele ya lundo la takataka tutafanikiwa kuepuka harufu mbaya kwa muda mfupi tu, lakini kuhatarisha afya yetu ya muda mrefu na kuacha tatizo pale pale.

Sifahamu idadi, lakini naamini ni mameya wengi wa majiji ya Afrika waliozuru Kigali na kuona tofauti iliyopo na kwao. Haiwasaidii kusifia tu. Muhimu ni kujifunza na kutumia hiyo elimu kuboresha majiji yetu.

Kufanana kwa usafi na mipangilio mizuri ya majiji yote ya Bara la Afrika na Kigali hakutamaliza tatizo la ubaguzi ambalo lina mizizi imara katika historia na tamaduni.

Lakini kutaboresha maisha ya Waafrika wengi wa mijini, kulinda afya zao, na kupunguza mada zenye chembechembe ya kibaguzi dhidi ya Afrika.

By Jamhuri