Kuzimwa simu kuathiri biashara ya pesa mtandaoni

Ukiondoa mawasiliano ya kawaida, eneo jingine kubwa litakaloathirika sana kutokana na zoezi la kuzima laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole litakapokamilika ni biashara ya pesa mtandaoni, ambayo thamani yake ilikuwa imefika zaidi ya Sh trilioni nane kwa mwezi mwishoni mwa mwaka jana.

Pamoja na kurahisisha maisha ya kutuma na kupokea pesa na kufanya malipo mbalimbali, huduma hiyo pia ni chanzo kikubwa cha mapato kwa serikali, kampuni za simu, taasisi mbalimbali pamoja na watu binafsi, hasa wale ambao wamejiajiri kama mawakala wa kampuni za simu.

Uzimaji wa laini za simu ulioanza saa nne usiku wa Januari 20 pia unatarajiwa kuathiri sana huduma za kifedha katika benki kupitia mfumo wa mobile/sms banking ambao umewawezesha watu wengi kuacha kupanga foleni kwenye matawi ya benki kwa ajili ya kutoa na kuweka pesa kwenye akaunti zao.

Hadi Novemba mwaka jana, thamani ya huduma za fedha benki kupitia simu za mikononi ilikuwa zaidi ya Sh bilioni 900, kiasi ambacho lazima kitapungua kutokana na zoezi la kuzima simu ambazo hazijasajiliwa litakapokamilika.

Siku moja kabla ya uzimaji kuanza, ni laini milioni 28.4 tu kati ya milioni 48 zilizokuwa sokoni ambazo tayari zilikuwa Zimesajiliwa, idadi ambayo ni sawa na asilimia 59.2 ya laini zote. 

Kwa mantiki hiyo, laini zitakazoathiriwa na hatua hii ni milioni 19.6 au asilimia 40.8, ambazo madhara yake kiuchumi na kibiashara yatakuwa makubwa sana ikishindikana kuzisajili.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zoezi la uzimaji wa laini hizo linatekelezwa kwa awamu na linatalajiwa kuwa limekamilika ndani ya wiki mbili tangu lilipoanza. Akizungumzia utekelezaji wake mwanzoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alisema awamu ya kwanza ya uzimaji wa simu hizo ulihusisha laini 656,091 na awamu ya pili itakuwa na laini 318,950.

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ndiyo inayosimamia biashara ya pesa mtandaoni, zinaonyesha kuwa miamala iliyokuwa imefanywa nchini kati ya Januari na Novemba mwaka jana ilikuwa na thamani ya takriban Sh trilioni 86.2, ambazo ni wastani wa Sh trilioni 7.8 kila mwezi.

Januari 2019, miamala ya pesa mtandaoni iliyofanyika ilikuwa na thamani ya karibu Sh trilioni 7.2 na mwezi Februari biashara hiyo ilishuka hadi Sh trilioni 7 kabla ya kupanda hadi Sh trilioni 7.3 mwezi uliofuata. Thamani ya miamala hiyo ilikuwa Sh trilioni 7.4, Sh trilioni 7.7 na Sh trilioni 7.8 Aprili, Mei na Juni mtawalia.

Kiwango kikubwa cha miamala kwa mwaka jana kilifanyika mwezi Julai na kilihusisha Sh trilioni 8.7 kabla ya kushuka hadi Sh trilioni 8.4 mwezi Agosti. Kwenye miezi mitatu iliyofuata, viwango vya biashara ya pesa mtandaoni ilikuwa Sh trilioni 8.1 (Septemba), Sh trilioni 8.4 (Oktoba) na Sh trilioni 8.2 (Novemba).

Mwaka 2018, huduma ya pesa mtandaoni ilikuwa na thamani ya Sh trilioni 81.4 ambazo ni sawa na wastani wa Sh trilioni 6.8 kwa mwezi. Biashara hii ilipoanza hapa nchini mwaka 2008, thamani yake ilikuwa Sh milioni 25.2 tu, lakini ilipofika mwaka 2012 tayari ilikuwa imeshamiri sana na kufika Sh trilioni 17.4.