Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeguswa na matumizi mabaya ya fedha za umma yanayodaiwa kufanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, na kuna taarifa za uhakika kuwa imeanza kumchunguza.

Pamoja na ofisi hiyo, kuna kikosi kazi kilichoundwa na mamlaka za juu kuchunguza suala hilo na hadi tunakwenda mitamboni tayari kimeshabisha hodi katika taasisi mbili kati ya nne zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Taasisi kuu zenye ukwasi zilizo chini ya wizara hiyo ni Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

“TAWA kifedha ina hali mbaya, huwezi kuilinganisha na hizo tatu, lakini kote huko amekuwa akitaka apewe fedha,” kinasema chanzo chetu.

Taarifa kutoka Ofisi ya CAG na ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii zinasema habari za matumizi mabaya yaliyomwandama Dk. Kigwangalla zimeshitua mamlaka ya nchi na ndiyo maana hatua za uchunguzi zimechukuliwa.

“Tumewasiliana na Ofisi ya CAG ili ikiwezekana ianze uchunguzi mara moja kuhusu tuhuma za matumizi ya fedha za umma yanayodaiwa kufanywa na waziri, tutatoa taarifa,” kinasema chanzo chetu kutoka serikalini.

Chanzo chetu kingine kinasema: “Haya mnayoambiwa kuhusu huyu waziri mbona ni madogo. Mambo yake makubwa yapo, ni suala la muda Watanzania watajua ukweli.” JAMHURI linaendelea kufuatilia jambo hilo.

CAG Charles Kichere, ameulizwa kuhusu ukaguzi unaodaiwa kufanywa katika taasisi hizo. “Siwezi kusema lolote, hayo mambo kama yapo au hayapo ni ya kiofisi. Kama lipo la kuuambia umma mtaambiwa, lakini kwa sasa naomba nisiseme lolote. Tunafanya kazi kwa taratibu na miiko,” anasema.

Dk. Kigwangalla amekuwa kwenye ugomvi mkubwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, chanzo kikielezwa kuwa ni amri za waziri huyo za kuchotewa fedha kutoka kwenye taasisi zilizo chini ya wizara anayoiongoza.

Katibu Mkuu anataka matumizi ya fedha yafuate miongozo, ilhali waziri akitumia mamlaka yake ya kiongozi mkuu wa wizara kupewa anachotaka. Fedha nyingi amekuwa akizichota kwa matumizi ya kile anachosema ni kutangaza utalii kupitia kwa wasanii mbalimbali.

Ugomvi huo umemfanya Rais John Magufuli atishie kutengua uteuzi wao endapo wataendelea kugombana na kukwamisha kazi za wizara ambayo ni mhimili mkuu katika kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Pamoja na fedha, Dk. Kigwangalla amekuwa akitumia mamlaka yake kuzigeuza ndege zinazomilikiwa na wizara hiyo kama daladala, kwa kuagiza ziwachukue rafiki zake mbalimbali bila kujali gharama. Mara kadhaa ametuma ndege kuwachukua wasanii, ama mmoja mmoja, au kundi kutoka pande mbalimbali za nchi.

Katika matukio mawili, waziri huyo ameagiza moja ya ndege za Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imfuate msanii kutoka Kigoma ili ashiriki tamasha jijini Arusha.

Katika tukio la pili, aliamuru ndege ya TANAPA imfuate mwanahabari mmoja jijini Dar es Salaam na kumpeleka Arusha, Rubondo, Katavi na baadaye akarejeshwa Arusha. Ndege hiyo ilitakiwa imchukue mwanahabari huyo saa 2 asubuhi katika Uwanja wa Julius Nyerere, lakini alitokea saa 9 alasiri huku ndege ikiendelea kumsubiri kwa muda wote huo.

“Haya mnayoandika ni tone ndani ya pipa la maji, tunashukuru mamlaka za juu zimeanza kufanya uchunguzi. Majibu mtayapata, matumizi ya fedha yaliyofanywa ni makubwa mno,” kinasema chanzo chetu.

Wageni wake, wakiwamo wasanii wakiwa katika majiji kama Arusha hulazwa katika hoteli za kifahari za kuanzia hadhi ya nyota nne.

Profesa Mkenda amekuwa haridhishwi na matumizi ya fedha hizo, na amekuwa akitaka taratibu zifuatwe ili kunusuru fedha za umma, lakini na yeye mwenyewe kama mtendaji mkuu na ofisa masuuli wa wizara abaki salama.  

Dk. Kigwangalla, kama alivyowahi kufanya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa mwisho katika Awamu ya Nne, Lazaro Nyalandu, amekuwa akiagiza apewe fedha nyingi ili kuwalipa wasanii kwa kigezo cha kuwatumia kuhamasisha utalii ndani na nje ya nchi.

Kwa kigezo hicho, amekuwa akiyatumia makundi ya wasanii kuzunguka huku na kule nchini kufanya shughuli hiyo. Wasanii hao huzuru hifadhi za taifa, pia hushiriki matamasha mbalimbali. Hivi karibuni alipeleka kundi la wasanii kukwea Mlima Kilimanjaro, lakini ni mmoja tu aliyefanikiwa kufika kileleni. Wengine, licha ya kushindwa, waliendelea kulipwa fedha kwa muda wote uliopangwa.

“Kuna makundi ya wasanii yanapelekwa kwenye maeneo mbalimbali ya hifadhi, gharama zake ni kubwa. Waziri anadai gharama zibebwe na wizara, sawa; lakini kuwe na utaratibu, yeye hataki. Unakuta anaagiza zitolewe Sh milioni 170, zitolewe Sh milioni 80; mara zitolewe Sh milioni 100 na kadhalika. Hizi fedha ni nyingi na kwa maana hiyo lazima kuwe na utaratibu wa kifedha wa kuziomba na kuzitoa.

“Mbaya zaidi, fedha hizo hutakiwa zilipwe na wakuu wa taasisi kwa maelekezo ya waziri. Huo si utaratibu. Kule kwenye taasisi wakisema hawana mamlaka ya kufanya malipo bila maelekezo ya katibu mkuu, mgogoro huanzia hapo.

“Katibu Mkuu anapoambiwa anang’aka na kutaka fedha zisitolewe bila kufuata mfumo wa malipo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Waziri akishajua katibu mkuu amekwamisha malipo kwa sababu hizo, basi ugomvi unalipuka,” kinasema chanzo chetu.

JAMHURI limeelezwa kuwa baada ya Waziri Kigwangalla kuona anakwamishwa na katibu mkuu, alianza kutumia utaratibu wa kumwagiza msaidizi wake kuwasiliana moja kwa moja na wakuu wa taasisi hizo ili wafanye malipo.

“Hilo nalo lilionekana kuwa ni ukiukwaji wa taratibu, kwa sababu msaidizi wa katibu hana mamlaka ya kuwasilisha maelekezo ya kufanyika malipo. Utoaji fedha za umma una taratibu zake,” kinasema chanzo chetu.

“Ninachoweza kukuhakikishia ni kuwa kuna mpango wa watu kuwania nafasi kubwa zaidi mwaka 2025, kwa hiyo kinachofanyika sasa ni kuwavuta wasanii ili wawe karibu nao kwa ajili ya mwaka 2025. Hili halina ubishi kwa sababu tumo humu tunajua mengi. Kinachofanywa sasa ni kujenga mtandao wa kuungwa mkono na ndiyo maana unaona wanaotumika hapa ni wasanii na watu wa online,” kinasema chanzo chetu na kuongeza:

“Angalia hata wajumbe wa bodi, baadhi yao wanateuliwa kwa sababu ni marafiki wa wakubwa wizarani na wanawekwa kwa malengo maalumu.”

Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana, wasanii saba walifanya ziara katika baadhi ya hifadhi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sehemu ya kujionea vivutio ili kuvitangaza, hivyo kuhamasisha wageni na wenyeji kutalii.

Ziara hiyo ilianzia katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato na kuendelea hadi Hifadhi za Taifa za Ibanda – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe. Kiongozi mkuu wa msafara alikuwa Dk. Kigwangalla mwenyewe. 

Wasanii wa muziki na maigizo (Bongo Movie) walioshiriki ni Steve Nyerere, Dude, Richie, Shilole, Ebitoke, Shetta na mwakilishi kutoka Muziki AT (Zanzibar). Baadaye walizuru Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.

Wizara ya Maliasili na Utalii inatajwa kuwa miongoni mwa wizara zenye vishawishi na fitina nyingi. Mara kadhaa viongozi wenye ‘roho nyepesi’ za kujipatia ukwasi wamekuwa hawadumu. Lakini pia wale wanaokuwa na ‘mioyo migumu’ ya kukataa kushiriki magenge ya ufisadi wamekuwa wakiandamwa kwa kuundiwa fitina ambazo hatimaye huwaondoa madarakani.

Kuanzia mwaka 2006, Wizara ya Maliasili na Utalii imeongozwa na mawaziri saba kwa vipindi vinane. Alianza Anthony Diallo, akafuata Profesa Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga, Ezekiel Maige, Balozi Khamis Kagasheki, Lazaro Nyalandu, Jumanne Maghembe (mara ya pili) na sasa ni Dk. Hamis Kigwangalla.

Kwa kipindi hicho makatibu wakuu waliopitia wizara hii ni Salehe Pamba, Blandina Nyoni, Dk. Ladslaus Komba, Maimuna Tarishi, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, na sasa ni Profesa Mkenda.

Idara ya Wanyamapori inayotajwa kuwa yenye vishawishi vya kila aina, haikuwa nyuma kwenye pangua pangua za wakurugenzi wake.

Kuanzia mwaka 2016, idara hiyo imeongozwa na Emmanuel Severre, Erasmus Tarimo, Obeid Mbangwa, Profesa Alexander Songorwa (mara mbili), Paul Sarakikya (Kaimu), Herman Keraryo na sasa ni Dk. Maurus Msuha.

Nyalandu anayetajwa kuwa miongoni mwa mawaziri walioifaidi vilivyo Wizara ya Maliasili na Utalii, alifikia hatua ya kuwa na vyumba maalumu katika hoteli za kitalii katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha vilivyolipiwa na taasisi za NCAA na TANAPA. Malipo hayo hayakuzingatia kama amelala, au la.

Ofisini kwake kwenye Jengo la Mpingo, alionekana kwa nadra; na hata alipotaka kuzungumza na waandishi wa habari, alitumia hoteli za kitalii ambazo malipo yake huanzia Sh milioni 3 kwa saa kadhaa. Alifanya hivyo ilhali wizarani kwake kukiwa na ukumbi wa kisasa wenye viyoyozi na huduma zote za kuendeshea mikutano.

Mara kadhaa alitumia ndege za taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa ajili ya shughuli binafsi zisizokuwa na uhusiano na ofisi.