Januari 4, 2020 Jenerali David Bugozi Waryoba Musuguri, alikuwa na hafla ya kutimiza umri wa miaka 100. Mamia ya watu walihudhuria sherehe hizo zilizofanyika nyumbani kwake Butiama mkoani Mara. Ufuatao ni wasifu mfupi wa Jenerali Musuguri uliosomwa siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake.

Jenerali mstaafu David Bugozi Waryoba Musuguri alizaliwa Januari 4, ‌1920 katika Kijiji cha Kumuruti, Masabha. Sasa sehemu hiyo inajulikana kama Nyasirori, akiwa mtoto wa tatu katika familia ya mzee Musuguri wa Nzangho. 

Alipozaliwa aliitwa jina la Waryoba, ikiwa ni ishara kwamba alizaliwa asubuhi wakati jua linachomoza. Baba yake mkubwa, Mgendi wa Nzangho alimwita jina la Bugingo. 

Akiwa na umri wa miaka mitano,  mzee Musuguri Nzangho alihamia Kijiji cha Butiama‌, ‌wakati huo paliitwa ‌Mu-kyaro. 

Jenerali mstaafu David Bugozi Waryoba Musuguri alikuwa mtoto wa tatu kuzaliwa katika tumbo la mama yake, Wakuru wa Kibumbiko. Bibi mzaa mama yake pia alikuwa anaitwa Wakuru wa Kigeso. Jina la Wakuru ni jina kubwa sana katika ukoo huu wa Jenerali Musuguri. 

Mzee Musuguri wa Nzangho alioa wanawake ‌sita. Alikuwa mfugaji wa ng’ombe na mbuzi na alikuwa stadi kulinda mifugo yake, kwani yeye na wachungaji wenziwe waliwahi kwenda kuwinda simba na waliua simba 18‌

Enzi hizo wanyama wa pori walikuwa wapo mapori ya karibu maeneo ya  ‌Bisarye, Ikizu na Buhemba. 

Akiwa kijana mdogo, hakubahatika kwenda shule. Muda mwingi alichunga ng’ombe na mbuzi wa baba yake, kwa kuwa alikuwa mtoto wa kiume pekee hapo kwao, wengine walikuwa wasichana. 

Jina la Bugozi

Jenerali Musuguri kwa maisha yake ya kazi amejulikana pia kwa jina la Bugozi. Jina hili alijiita mwenyewe kutokana na uwezo wake wa kupigana mieleka, inayojulikana kwa Kizanaki kama, ‘erigori.’ Wakati huo ‘erigori‌’ lilifanyika eneo ambalo lilipata umaarufu kwa kuitwa jina lake hilo. 

 ‌

Kuingia Jeshi la Mkoloni – King’s African Rifles (KAR) 

Jenerali Musuguri aliingia jeshini ‌katika mazingira tata. Mwenyewe anasimulia kwamba kati ya mwaka 1942 au 19‌43, katika sehemu ya kilima cha Mutuzu‌, ‌Butiama kuna mama aliuawa kutokana na sababu za kishirikina. Polisi walifika ‌hapo kijijini na kuwakamata vijana ili wasaidie kubeba mwili wa marehemu ‌kuupeleka Musoma kwa ajili ya uchunguzi. 

Wakati wakisubiri kwenda Musoma‌, ‌waliwekwa rumande kwenye boma la Chifu Edward Wanzagi Nyerere. Lakini usiku kabla ya safari hiyo‌, ‌kijana Waryoba Musuguri akiwa na umri wa miaka 22, na vijana wengine walitoroka na kwenda Musoma‌. Huko akajiandikisha kujiunga katika Jeshi la KAR. 

Alipotoroka aliambatana na wenzake – ‌Mugendi Nyamatwema na Mkono wa Nzenzere. Wakatembea mpaka Musoma kujiunga jeshini. 

Wakati huo Chifu Edward Wanzagi Nyerere alikuwa ametawazwa mwaka 1942 baada ya baba yake, Chifu Nyerere Burito, kufariki dunia. 

Baadaye alijiunga na vijana wenziwe Mwanza, wengine wakajiunga Morogoro, mpaka walipo‌fika ‘depo’ ya mafunzo Dar es Salaam. 

Akiwa jeshini ndiko alikopata elimu ya kusoma na kuandika, na akaweza kujiendeleza hata kufanya kozi ‌mbalimbali za kijeshi katika nchi za Canada na China. 

Akiwa KAR alipigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambayo ilimwezesha kupigana katika uwanja wa vita katika nchi nyingi, zikiwamo India, Burma, Ushelisheli, Canada, mpaka Japan ambako alijeruhiwa kwa risasi kwenye paja. Alivuja damu na kupoteza ‌fahamu‌. Alibebwa na askari mwingine Mtanzania aliyeitwa Marega – huyu anatoka Ngoreme. Kwa kitendo hicho cha kumwokoa, aliendelea ‌kuwa rafiki yake wa karibu hadi alipofariki dunia. 

Akiwa KAR‌, miongoni mwa wanafaunzi wake ni aliyekuja kuwa kiongozi wa Uganda, ‌Idd Amin Dada, aliyejiunga na jeshi la KAR, Kahawa Barracks mjini Nairobi. 

Jenerali ‌Musuguri pia alipigana vita ya MAUMAU nchini Kenya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia akiwa jeshi la KAR. 

Mwaka 1957 aliongoza kikosi cha wanajeshi wa KAR kutoka Afrika Mashariki kwenda London, Uingereza kwenye gwaride la Malkia wa Uingereza. Alipeleka ‌historia ya KAR katika Afrika Mashariki, na yeye ndiye aliyemkabidhi historia hiyo Malkia Elizabeth II Juni 11, 1957 katika Kasiri la Mfalme la Buckingham wakati huo akiwa na cheo cha Warrant Officer Platoon Commander (W.O.P.C). Alikuwa Mwafrika wa kwanza kuonana na kupeana mkono na Malkia Elizabeth II wa Uingereza.

Uhuru 

Baada ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961, aliendelea kuwapo jeshini. Baada ya Uhuru KAR ilibadilishwa jina na kuitwa Tanganyika Rifles. 

Baada ya maasi ya mwaka 1964, Jeshi la Tanzania liliundwa upya likawa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ‌) ‌au Tanzania People’s Defence Forces (TPDF)‌, ‌likiwa na viongozi Watanzania wazalendo. Alikwenda kwenye vita ya Kagera ya kumtimua nduli Idd Amin ‌kati ya mwaka 1978 hadi 1979, ambako alitambulika kwa kuongoza vita kishupavu na akaitwa ‘‌Jenerali Mutukula, ‌Kamanda mwenye Uso wa Chuma’.

Jenerali mstaafu ‌Musuguri alipitia vyeo vyote vya kijeshi kuanzia ‘Private’ mpaka ‘‌Full General’ akiwa Mtanzania wa kwanza kupata cheo hicho cha ‘‌Full General’.

Aliendelea kufanya kazi ya jeshi kwa weledi na ujasiri hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ‌(CDF). Kwa mtiririko wa ma-‌CDF wa JWTZ, Jenerali Musuguri alikuwa ‌wa tatu.

Alistaafu kazi ya jeshi mwaka 1988 na tangu hapo amekuwa akiishi nyumbani kwake Butiama (‌Makao Makuu ya 

Wilaya ya Butiama) akijishughulisha na kilimo na ufugaji. 

Baada ya kustaafu‌, ‌Jenerali mstaafu David Bugozi Waryoba Musuguri, akiwa kijijini alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Butiama, mwaka 1990 hadi mwaka 1991. 

Katika siku hii ya leo (Januari 4, 2020) ‌Jenerali Musuguri anapotimiza miaka 100, anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha kuwa na afya njema na uhai wa kutimiza karne moja.

Anaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Amiri Jeshi Mkuu, Dk. John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile anatoa shukrani kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo‌, makamanda na ‌wapiganaji wote. 

Anatoa ‌pia shukrani kwa Watanzania wote kwa heshima na huduma nzuri ambayo taifa limekuwa likimpa, hususan katika matibabu ambayo amekuwa akipata hapa nchini na nje ya nchi.  ‌

Katika nyakati tofauti, Jenerali Musuguri amepata matibabu katika hospitali mbalimbali. Anapenda kuwashukuru madaktari na wauguzi wote wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama, Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Hospitali ya Jeshi Lugalo,‌‌Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na hospitali zilizoko nje ya nchi kama ‌China, Urusi, London – Uingereza, Ujerumani, ‌Pretoria – Afrika Kusini na New Delhi, India.

By Jamhuri