Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema kuwa katika kipindi cha takribani miaka 100 tangu Bunge lianze kufanya kazi, kuanzia enzi za ukoloni, kuna mambo mengi yamefanyikao, ikiwemo kuisimamia Serikali kwa ufanisi na kutanguliza maslahi ya wananchi ili kuleta maendeleo.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, Julai 1, 2026, Spika Zungu amesema kuwa Bunge linapoelekea kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1926 chini ya mkoloni wa Tanganyika, maadhimisho ambayo yanatarajiwa kufanyika Januari 2027, limeendelea kujitahidi kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kupitia taratibu mbalimbali za kibunge.
Amesema chimbuko la muhimili huo ni Machi 19 ambapo mwaka 1926 wakati Tanganyika ikiwa chini ya ukoloni wa Uingereza ndipo ilitungwa Sheria ya kuanzisha Baraza la Kutunga Sheria
Zungu amesema Baraza hilo lilizinduliwa katika Ukumbi wa Shule ya Aga Khan ambayo kwa sasa ni Sekondari ya Tambaza ambapo Baraza la kwanza, liliundwa na wajumbe 20 walioteuliwa na sheria zilizotungwa zilipelekwa Uingereza kupata idhini ya mfalme.
Mabadiliko yalishuhudiwa kwa kuingia kwa Watanganyika ndani ya Baraza wakianza Chifu wa Wachaga na Wasukuma. Amesema katika miaka 100, Bunge limekuwa nguzo muhimu ya Demokrasia.
Ametolea mfano ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akisema kuwa hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa baada ya Bunge kuzifanyia kazi ripoti hizo. Ameongeza kuwa wakati wote Bunge limekuwa mstari wa mbele kusimamia ustawi wa wananchi kwa kuhakikisha mambo yenye kuleta maendeleo yanasimamiwa ipasavyo.
Katika kipindi hicho, amesema Bunge limefanikiwa kwa kuwa na uwakilishi wa kutosha wa wanawake ambao kwa mwaka huu ni takriban asilimia 40, kiwango ambacho ni cha juu.
Amesema tangu kipindi hicho, uwakilishi wa vijana umefikia wabunge 72 na sasa kimeanzishwa chama cha wabunge vijana Tanzania, huku wabunge wenye ulemavu wakiongezeka na kufikia 11.
Spika amesisitiza kuwa shughuli za Bunge zinaendeshwa kwa uwazi na weledi na endapo kuna mtu anaona jambo linafanyika tofauti na matarajio yake, milango iko wazi kupokea maoni yake na kuyafanyia kazi.
Kihistoria Bunge la Tanzania linatimiza miaka 100 mwaka huu tangu kuanza kwake kama Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1926 ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Miaka 100 ya Bunge: Historia Yetu, Dira Yetu”.












