Na Mwandishi Wetu Zanzibar
Mwenyekiti wa Kamati ya Mapngo wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman, amewataka wadau wanaojihusisha na masuala ya ukatili na udhalilishaji kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano ili kutokomeza vitendo hivyo katika jamii.
Mhe. Haroun alitoa wito huo jana wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya ngazi ya Mawaziri uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport, Zanzibar.
Alisema kuwa lengo la kuundwa kwa kamati hiyo ni kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto, kwa lengo la kupunguza na hatimaye kuvimaliza kabisa.
Aidha, aliitaka kamati hiyo kutekeleza majukumu yake kwa bidii, kuweka mikakati madhubuti na kuhakikisha sheria pamoja na sera zilizopo zinatekelezwa ipasavyo ili kulinda haki za wanawake na watoto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Anna Athanas Paul, alisema Wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuimarisha mifumo ya ulinzi wa jamii.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itaendelea kutoa elimu kuhusu haki za wanawake, watoto na wananchi kwa ujumla ili kujenga jamii yenye kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Naye Afisa Programu za Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Ali Haji Hamadi, alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia utekelezaji wa programu zinazolenga kulinda haki, afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana.
Katika uzinduzi huo, Mkuu wa Divisheni ya Watoto, Mohammed, aliwasilisha muhtasari wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa miaka mitano (2025–2030), akieleza mpangilio wa utekelezaji wake, ushirikiano wa sekta mbalimbali na wadau wa maendeleo, pamoja na mfumo wa uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya mpango huo.
Kwa upande wa Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, ndugu Omar Haji, aliwasilisha muundo na majukumu ya Kamati hiyo. Alieleza kuwa Kamati itaongozwa na Waziri anayeshughulikia masuala ya sheria, ndie mwenyekiti huku Waziri anayesimamia masuala ya jinsia akiwa Mwenyekiti Mwenza, kamati hiyo inawajumuisha Wizara,na taasisi za Kiserikali na binafsi na washirika wa maendeleo.
Alisema miongoni mwa majukumu makuu ya Kamati hiyo ni kutoa mwongozo wa kisera, kuhakikisha afua zinaendana na mikakati ya kitaifa, kushawishi ugawaji wa bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mpango kazi, kusimamia usimamizi wa kesi za ukatili na kuhakikisha mashitaka yanawasilishwa na kuendeshwa kwa wakati.
Uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza Ukatili na Udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto ulihudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali, wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), pamoja na washirika wa maendeleo wakiwemo UNICEF, UNFPA na UN Women.









