Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua Daraja la Mto Nyathorogo lililopo katika Kijiji cha Nyathorogo, Kata ya Nyathorogo, wilayani Rorya, mkoani Mara, ambalo limejengwa kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kati ya wilaya za Rorya na Tarime.
Akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara leo Jumatano, Julai 2, 2026, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Rorya, Mhandisi Elifadhili Moses.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi wa ujenzi wa daraja hilo umegharimu shilingi milioni 729.2 ulianza Agosti 1, 2025 na kukamilika Februari 28, 2026.
Mhandisi Moses alisema daraja hilo limejengwa kwa teknolojia ya mawe iliyowezesha kupunguza gharama za ujenzi kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na usanifu wa awali, na kwamba Serikali imetenga fedha katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa kingo za kulinda daraja dhidi ya athari za maji.
Naye Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege alisema daraja hilo limeondoa adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Rorya na Tarime, ambapo awali walilazimika kuvuka Mto Nyathorogo katika mazingira hatarishi yaliyosababisha ajali na kupoteza maisha.
Aidha, alisema ujenzi wa daraja hilo umeboresha mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.








