Ndugu msomaji, tazama picha iliyo katika ukurasa huu, kisha utafakari. Nimeitumia kama kielelezo halisi cha kutusaidia kuibua mjadala wa maana kuhusu hatima ya umasikini unaowaandama watoto wa masikini katika Taifa letu.

 

Mara zote tumekubalina na dhana ya kwamba elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mara zote alisema kuwa kama unataka kumkomboa kweli mtoto wa masikini, ni kuhakikisha unampa elimu.

Kwa maneno mengine ni kwamba mtoto wa masikini akipata elimu, atapambana na umasikini. Akifanikiwa kuushinda atakuwa ameondoa uwezekano wa familia yake kuwa masikini. Watoto wanaoonekana katika picha hii ni sehemu tu ya malaki ya watoto wa aina hiyo wanaotaabika nchini mwetu.

 

Wakati watoto hawa masikini wakitaabika, kuna kundi dogo sana la watoto wa viongozi na matajiri linalofaidika na rasilimali za Taifa letu. Mtu yeyote makini hahitaji kuwa nabii kujua hatari inayowakabili watoto hao na hata watoto wa matajiri ambao kwa sasa wanasoma katika shule zenye huduma zote muhimu.

 

Ndugu zangu, picha hizi zinawafanya watoto hawa wakue kwa simanzi kubwa. Zinawafanya wawe na kinyongo dhidi ya kundi dogo la familia za viongozi na watoto wa matajiri.

 

Hali hii inawafanya watoto hawa makabwela waingiwe na chuki, hasa pale watakapotambua kuwa tofauti kati yao na watoto wa matajiri haitokani na amri ya Mungu, bali inatokana na ubabe, wizi, dhuluma, ghilba na uonevu wa kundi moja dogo, lakini lenye nguvu na ushawishi wa kujitwalia rasilimali za nchi.

 

Tunaambiwa na ndiyo ukweli ulivyo, ya kwamba Tanzania ni moja kati ya nchi chache sana katika Afrika na dunia nzima zilizojaaliwa misitu mingi. Kama hivyo ndivyo, inakuwaje viongozi na wazazi wa Tanzania wakubali watoto wao kusomea katika mazingira mabaya namna hii?

 

Kabla ya Tanzania kukaribisha wezi kuja kuchimba dhahabu, tanzanite, gesi na madini mengine, watoto wa Tanzania walisoma wakiwa wanaketi kwenye madawati, walipata mlo shuleni, walisafiri kwenda kusoma katika shule za sekondari za serikali kwa gharama ya Serikali.

 

Kuna shule za msingi ambazo zilifikia hatua ya kuwashonea wanafunzi sare na kuwapa mahitaji ya vitabu, kalamu, madaftari na vifaa kadha wa kadha vya kujifunzia. Kabla ya Serikali ya Tanzania kubariki wizi wa samani kupitia viwanda vya kusindika minofu ya samaki, watoto wa Tanzania walitibiwa bure. Walipolazwa hospitalini walihudumiwa chakula, tena kwa mgonjwa kuchagua aina chakula alichokitaka.

 

Leo baada ya kuruhusu uchimbaji madini, uwindaji wa kitalii, usindikaji minofu ya samaki, si tu kwamba hana mahali pazuri pa kusomea, lakini hata elimu yenyewe imekuwa ghali mno. Ndiyo maana najiuliza, kuna jambo gani ambalo Watanzania tumemkosea Mungu?

 

Je, ni haki kweli katika nchi iliyofunikwa na misitu kuwa na watoto wanaosoma wakiwa wameketi kwa shida sakafuni? Je, ni haki kuwa na shule za aina hii ambazo ni kwa ajili ya masikini tu, na kuwa na shule maalumu kwa watoto wa viongozi na matajiri? Tufanye nini sasa? Nadhani wananchi tunapaswa kuikataa hali hii. Hatuwezi kuikataa kwa kulalama tu.

 

Hatuwezi kuondokana na dhuluma hii kwa kuwalalamikia viongozi walioamua kushirikiana na matajiri kuifaidi nchi hii! Mfumo tulionao sasa hauwezi kusaidia kutuondoa katika hali hii, wala Katiba mpya itakayotungwa haiwezi kuwalazimisha viongozi na matajiri kusomesha watoto wao katika sekondari za kata.

 

Lililo wazi hapa ni wananchi kuamka na kuhoji ili kujua ni wapi utajiri wa taifa letu unaishia hadi kutufanya tuwe na watoto wanaoketi sakafuni kwa kukosa madawati? Wananchi wajitokeze kuhoji ni kwanini Hifadhi za Taifa zaidi ya 10 hazijatufanya tuwe na maisha mazuri?

 

Tujitokeze tuhoji kwa nguvu zote ni kwanini kabla ya kuruhusu viwanda vya kusindika minofu ya samaki maisha yalikuwa mazuri kuliko wakati huu wa kuwapo viwanda? Wananchi wajitokeze kwa ujasiri kuwahoji viongozi na matajiri ni kwanini watoto wao hawasomi katika sekondari za kata na shule za msingi za Matembe?

 

Lazima wananchi sasa waulize, hivi hizi bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zinazoingiza mabilioni ya shilingi, fedha hizo zinaishia wapi? Wananchi tusimame kuhoji iweje Muhimbili isiwe na mashine ya X-ray, lakini mashine hiyo ikaweza kuwapo katika kizahanati cha mtaani?

 

Katika mtandao wa kijamii, Mtanzania mmoja amesema haya, “Katika hili la Hospitali ya Muhimbili kwa kuwa naijua vyema naomba niseme haya yafuatayo: 1: MRI (Magnetic Resonance Imaging)- mashine hii Muhimbili ipo, gharama za kipimo ni Sh 120,000. Ukienda Aga Khan, Regency na Hindu Mandal unapigwa Sh 540,000 kwa kipimo.

 

2. CT Scanning: Muhimbili ni Sh 80,000. Ukienda Aga Khan, Regency na Hindu Mandal unapigwa Sh 360,000.3. Kidney Dialysis: Hiyo ndiyo usiseme. Vipimo hivi “day in day out” ukienda Muhimbili unaambiwa vimekufa, nenda Aga Khan, Hindu Mandal na Regency, same doctors (madaktari hao hao wa Muhimbili wana-handle vifaa hivi private hospitals (hospitali binafsi) na kutoa majibu kwa gharama kubwa.

 

Mnyonge inabidi augulie tu, hawezi kumudu. Kila kukicha mafundi  kutoka Phillips Company, Uholanzi wanakuja Tanzania kurekebisha mashine hizi Muhimbili na zinakuwa OK, wakitoka tu zinakufa, patients (wagonjwa) wanaendelea kwenda hospitali binafsi. Madaktari wanalalamikia vifaa duni. Tutafika kweli?”

 

Ndugu zangu, maneno haya kama nilivyosema awali si yangu, bali ni ya Mtanzania mmoja aliyeyatoa kupitia mtandao wa kijamii. Muhimu hapa ni kwamba tatizo hili halijulikani kwenye vyombo vya Serikali? Halijulikani katika mamlaka zinazohusika ili liweze kumalizwa?

 

Kwa kuwa wanaohusika wako kimya, na kwa kuwa kimya chao kinatokana na uwezo na fursa zao nyepesi za kutibiwa India na ughaibuni, ndiyo maana nawahimiza sasa wananchi wenyewe kusimama kidete kudai haki zao. Haiwezekani kipimo cha Sh 80,000 katika hospitali ya umma kikaharibiwa na kwa hiyo wakatakiwa walipe zaidi ya Sh 300,000 katika hospitali binafsi.

 

Ukimya, ukondoo na kutohoji kwetu haki zetu kutatufikisha mahali kila kitu, hata hewa katika nchi hii, itakuwa bidhaa ambayo ili tuipate, itatulazimu tupate ridhaa kutoka kwa viongozi na matajiri wasiokuwa na huruma.

 

Na hili linaonekana wazi sasa kupitia picha hii unayoiona katika ukurasa huu. Kwa uamuzi wa kuwanyima watoto wa masikini elimu nzuri, maana yake ni kwamba makabwela wataendelea kutawaliwa milele. Tuanze kulikataa hili la elimu mbovu.

 

By Jamhuri