Kwa hili sote tu wadau (4)

Ilipoishia wiki iliyopita: Upinzani mzuri ni ule unaokosoa huku ukiwa na mpango kamili ya sera mbadala ya maendeleo ya Taifa. Kwa maana hiyo bungeni panakuwa na mawaziri wa Serikali kivuli (shadow government with its shadow Cabinet). Endapo Serikali iliyoko madarakani itaondolewa kwa kile kinachojulikana kuwa wabunge hawana imani nayo (by vote of ‘No Confidence’) mara moja upinzani wanachomoza na kutekeleza sera zao. Mpango namna huo ndiyo unaojulikana kama Serikali mngojea – (Government in waiting). Mambo hayaanzi upya kwa kufumua kila kilichojengwa na ile Serikali iliyoondolewa (voted out government). Wao wanajenga pale wenzao walipoboronga ilimradi kufanikisha maendeleo ya nchi yao. Endelea… 

 

magufuli88Sisi Watanzania kweli tunao mtazamo namna hii? Sifa sana ni kukosoa kila jambo na kumuona kila kiongozi hajui kitu na haelewi maana ya utawala bora isipokuwa upinzani wakipata wasaa namna ile wataonesha uwezo wao! Hapo ni kama yule mbunge wa mchezo wa mpira katika mazungumzo yale ya baada ya habari.

Kule Marekani, uchaguzi unafanyika mwezi Novemba ya mwaka huo wa uchaguzi. Kukabidhiana madaraka kumepangwa kikatiba huwa ni tarehe 20 Januari mwaka unaofuata. Rais mteule hukaa nje kuanzia Novemba mpaka Januari 19 mwaka unaokuja. Hapo Rais mpya anaangaliwa bila ya comments zozote mpaka tarehe 20 Aprili. Kuanzia hapo sasa mawazo yanaanza kumiminika juu ya utendaji wa Rais mpya.

Sisi huku Rais Magufuli ameapishwa Alhamisi Novemba 5, 2015 kwa hiyo mpaka  tarehe 5 Februari 2016 (siku 100 hizi) ndipo wakosoaji au wapongezaji watueleze maoni, mawazo au mitazamo yao. Siyo kabla ya hapo tunaposema mbona hata mishahara ye wabunge hatujalipwa! Huo ninauita ni hali ya kukamia kupinga kila kitu kijacho maadamu wewe au chama chako hakitawali, basi ni hovyo tu! Huo si utaratibu wa kujenga nchi ye umoja bali ni maisha wanasheria wanayoyaita ‘hostile’ ama kwa Kiswahili hali ye ‘uhasama’ tu.

Ninawasihi waheshimiwa viongozi wetu wote, waheshimiwa wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa Serikali tujijengee hali ya upendo. Tuwe na utulivu na tudumishe amani yetu. 

Niliwahi kuandika kuwa Mzee Lowassa anapenda utulivu na amani basi mashirika ya dini ulimwenguni zaidi ya 1,200 yameamua kumtuza medali ya Amani. Kumbe tunasikia pole katika mafundisho ya mlimani kule Galilei Bwana Yesu alitoa Heri 8. Moja wapo ya Heri zile inasema Heri Wapatanishi, maana hao wataitwa Wana wa Mungu (Mat. 5:9) na kwa hili mimi kiimani yangu hii nasema ukiwa mpatanishi, kamwe huwezi kuwa mvurugaji wa hali, na ndiyo maana utastahili kuitwa mwana wa Mungu ni ahadi isiyopingika.

Mwalimu Nyerere Mei 12, 1964 aliwaambia waheshimiwa wabunge maneno mazito haya nayanukuu, “Hakuna hata mtu mmoja kati yetu anayeweza kumaliza matatizo yote tuliyo nayo, na jinsi kila mmoja wetu anavyofanya yake ndivyo maendeleo yatatokeo. lpo kazi kwa kila mmoja wetu, wabunge wana kazi kubwa yenye madaraka na kwa miaka ijayo wajumbe waheshimiwa wana kazi ya kusaidia mpango wa maendeeo ufanikiwe na vile vile kutafuta na kusahihisha vitatizo vyovyote vitakavyoleta kutokuelewana kama vikitokea.” (Nyerere: Mpango wa I wa Maendeleo — Bunge 1964 -1965 ukumbi wa Karimjee).

Wabunge talented kama akina Zitto Kabwe, Tundu Lissu na John Mnyika wanaweza sana kutoa mchango mzuri katika maendeleo ya nchi yetu wakiwa bungeni au nje ya Bunge kwenye jamii. Karama zao zinatumika visivyo kwa kukamia kupinga hata lisilopingika. Hii ndiyo shida ya masomo ya Sanaa (Arts), kumbe kisayansi hesabu au physics au chemistry ni kucheza na fomyula au tarakimu kukokotoa tu hakuna bla bla ya maneno hapa. Hapo hapatatokea ubishi wa kuchanganya maneno ya kisheria (symantix).

Wabunge wa kuchaguliwa wote wanawajibika kwa wapiga kura waliowawezesha kuingia bungeni. Sasa inakuwa haieleweki mbunge anasusia kikao kwa uamuzi wa silika na matakwa yake tu, wala hakushauriana na waliomchagua. Hakuwauliza ridhaa yao eti itokeapo hali namna kadhaa kadhaa “nisusie kikao au niendelee kuwawakilisha?” Awasikie waajiri wake watampa mwongozo gani. Hapo ndipo mimi naona ubinafsi wa kibinadamu, haufikirii wengine hata kidogo.

Mimi naona tabia hili ya upinzani kususa ni wa silika ya kibinadamu na wa kujinufaisha. Naifananisha na mwenye mnyama (ng’ombe au mbuzi au kuku mgonjwa) anampeleka kwa tabibu wa mifugo (veterinary surgeon akatibiwe. 

Swali langu, je, huyo mnyama anajua kuwa anaumwa? Pili unapomgharamia tiba kweli mnyama anaona faida yake au ni wewe mwenye mfugo ndiyo unayenufaika na kupona kwake? Huo ndiyo uroho na unafsi wa mwanadomu. Yuko tayari kabisa kumgharamia mfugo wake ili apone, anone amuuze kwa faida yake. Kamwe mfugo huo haujui hayo. Ndivyo wabunge kadhaa wafanyavyo, kulilia kura waende bungeni kunufaisha silika zao na itikadi ya vyama vyao. Hilo ndilo kosa kimaendeleo ya nchi yetu. Kutoka nje ya Bunge kunamsaidiaje yule mpiga kura wa kule kijijini? Faida ipi hiyo kimaendeleo au imempunguziaje kero zake pale kijijini? Je, amepata mali anayohitaji? Amepata dawa anazohitaji? Badala yake wewe uliyesusa na kutoka bungeni umeonekana mwenye runinga. Huko ndiyo kuwakilisha shida za wapiga kura?

Ushauri wa bure. Watanzania sasa tumepevuka kisiasa, tusiendelee kuiga demokrasia za kuonekana mwenye vyombo vya habari kuwa tumetoka nje ya Bunge, tumesusia vikao na kadhalika. Wafadhili wanapenda hilo lakini je, jimboni walikokupigia kura umewanufaishaje? Lipi la msingi lililokupeleka – la uwakilishi au kumpendeza mfadhili yule wa ng’ambo? Si utumwa huo? Kupokea amri kutoka nje si ukoloni mamboleo?

Tumhukumu Rais Magufuli kwa yale atendayo baada ya zile siku 100. Suala Ia mishahara ya wabunge kuchelewa kulipwa ni la watendaji wa Bunge siyo sera ya Rais wa chama tawala. Basi hoja yangu ya msingi hapa ni kwamba hii tabia ya baadhi ya wawakilishi wetu katika vyombo vya maendeleo kuendeleza mwelekeo hasi (bear negative attitudes) ibadilike sasa. Mtazamo hasi kwa kila litendwalo na Serikali ni kudumaza maendeleo ya nchi. Kama kuna ongezeko la makusanyo ya kodi ya fedha na fedha zile zikaelekezwa kwenye huduma muhimu kama afya na elimu, hapo mbunge kukosoa eti hajalipwa mshahara wake wa ubunge ni dalili wazi ya ubinafsi. Apate yeye kwanza ndipo akiri kama kweli pato huko Hazina limeongezeka.

Tulisikia Bunge lililopita mbunge Zitto Kabwe na wengine kadhaa walisitisha kupokea posho zao za vikao na wakaelekeza (directed?) zipelekwe majimboni kunufaisha wengi. Kama hilo ni kweli, hapo unaona mitazamo tofauti ya moyo wa uzalendo. Baadhi ya Wabunge wanasusa vikao lakini wanapokea posho ya siku. Wazalendo wanahudhunia vikao na kuelekeza posho ipelekwe majimboni kwa faida ya waliowapa kura. Sijui wasomaji hapo nani anaonesha uongozi bora Ukisusa kikao, usipokee posho hapo itakuwa umeokoa fedha za umma (savings to government) ‘Tanzania itajengwa na wenye moyo’, je, ni akina nani hao? Ni wewe na mimi.

Jambo kubwa, muhimu na la msingi kwangu mimi ni Watanzania viongozi na sisi tunaoongozwa tujione sote kuwa tu wadau wa amani. Dhamira ya kwanza ni kudumisha amni katika nchi yetu. Ukiwa mzalendo kweli ninaamini utaelekeza fikra zako, nguvu zako na matendo yako yote kwenye kutafuta amani ya kweli hapa nchini. ‘Shalom’ – amani iwe kwenu.