Je, Kikwete atafanikiwa mgogoro wa Libya?

jakaya kikwete
jakaya kikwete
Februari mosi, mwaka huu tulitangaziwa kuwa Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, ameteuliwa na Umoja wa Afrika (AU) kuwa mwakilishi wake katika kusuluhisha mgogoro wa Libya.

Uteuzi huo ulifanywa mjini Addis Ababa katika kikao cha wakuu wa nchi za Afrika, naye Kikwete akawashukuru wakuu wa nchi za AU kwa “imani kubwa waliyoonyesha kwake” na pia akawashukuru wadau wa siasa nchini Libya kwa kuridhia uteuzi wake. AU imemweleza Kikwete kuwa inayo matarajio makubwa juu yake na iko nyuma yake.

Katika jukumu hili, Kikwete atakuwa anaongoza jopo la marais watano walioteuliwa na AU. Kazi yao kubwa itakuwa ni kusuluhisha makundi yanayounda serikali mbili tofauti nchini Libya – moja iliyo mashariki ambayo inatambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na ya pili iliyo katika mji mkuu wa Tripoli ambayo inatawala kwa kutumia majeshi.

Ni vizuri tukajiuliza kama imani hii ya AU inatosha, kwani bila shaka Kikwete atakumbwa na matatizo yanayotokana na mapigano yanayoendelea tangu Libya ivamiwe na majeshi ya NATO, ikasababisha kuuawa kikatili kwa mtawala wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, miaka mitano iliyopita.

Kikwete si tu atakumbana na matatizo ya ndani, bali pia na mataifa ya NATO ambayo yana nia tofauti na ile ya AU. Wakati AU inataka usuluhishi kwa njia ya amani, NATO kama kawaida yake inajiandaa kutumia nguvu zake za kijeshi. Ili kulielewa hili ni vizuri tukaangalia chimbuko la mgogoro huu.

Mnamo mwaka 2011 Gadafi  alipinduliwa na akauliwa baada ya uvamizi wa majeshi ya NATO.  Walifanya hivyo kinyume cha azimio la UN ambalo halikutoa idhini ya kuishambulia Libya.

Sasa imetimia karibu miaka mitano na Marekani na wenzake wa NATO wanapanga uvamizi mwingine katika nchi hii inayoongoza kwa utajiri wa mafuta barani Afrika. Haya yamesemwa na Marekani wenyewe. 

Januari 27 msemaji wa makao makuu ya kijeshi nchini Marekani (Pentagon), Peter Cook alikaririwa akisema kuwa majeshi yake yanajitayarisha kwa mashambulizi ya Libya. Kazi inayofanywa sasa ni kuchunguza ni kikundi kipi wataweza kushirikiana nacho.

Pia kuna Jenerali Joseph F. Dunford Jr. ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Marekani. Januari 23, mwaka huu alisema nchi hiyo na washirika wake wa NATO wanafanya maandalizi ya uvamizi mwingine nchini Libya ili kudhibiti ukuaji wa majeshi ya ISIL (Daesh) nchini humo. Hawa wengi wao ni askari na wafuasi wa Gaddafi ambao wamejichimbia katika mji wake wa Sirte.

 

Akaongeza kuwa uvamizi huu  wa kijeshi utafanyika kwa kushirikiana na “serikali mpya” ya Libya. Hii ni serikali iliyochongwa na mataifa ya NATO kupitia mwakilishi wa UN, Martin Kobler. Alipoulizwa ni lini wanatarajia kuanza mashambulizi, Dunford alijibu “itachukua wiki chache”.

Licha ya Marekani nchi nyingine zilizo msitari wa mbele katika uvamizi huu ni Uingereza, Ufaransa na Italia. Ndiyo maana Februari 2, mwaka huu wawakilishi kutoka nchi 23 walikutana mjini Rome kuzungumzia uvamizi huu wa pili nchini Libya. Hizi ni nchi zilizoshirikiana na NATO katika uvamizi wa 2011. Walijadili mkakati wa kuwazuia mujahidina wasidhibiti mafuta.

Kwa maneno mengine, wakati AU inamteua Kikwete kwenda kusuluhisha mgogoro miongoni mwa makundi ya Libya, mataifa ya kibeberu ya NATO yanafikiria kutumia majeshi yao ili kudhibiti mafuta. 

Lakini jaribio hili halitakuwa rahisi hata kidogo. Mwaka 2011 walitumia kisingizio cha kuwaokoa raia kutoka udikteta wa Gadafi. Safari hii wanasema adui ni mujaahidina wa ISIS (Daesh). Hii si rahisi kukubalika kwani raia wengi wa Libya wanapinga kuingiliwa na majeshi ya kigeni.

Desemba, mwaka jana makomando 20 kutoka Marekani waliovalia kiraia walijipenyeza nchini Libya wakiwa na silaha. Mara moja wapiganaji wa Libya waliwakamata, wakawanyang’anya silaha na kuwafurusha kutoka nchini.

Idhaa ya NBC nchini Marekani ilipowauliza maofisa wa Pentagon kuhusu tukio hili, walikubali kuwa ni kweli, tena wakaongeza kuwa makomando wao wamekuwa wakiingia Libya “mara kwa mara”.

Mataifa ya NATO yakiongozwa na Marekani yaliivamia Iraki na sasa yako Syria. Matokeo yake katika nchi hizi kimezuka kikundi cha Daesh.  Hata hivyo, kikundi hiki kinaonekana kupungua nguvu katika nchi hizi.

Daesh huko Syria inaonekana inarudi nyuma hasa baada ya majeshi ya Russia kuingia nchini na kutumia ndege zake za kivita ili kufagilia majeshi ya rais Assad. Kwa hivyo kuna uwezekano wa kutafuta mahali pa kuhamia, na mahali penyewe yumkini ni Libya.

Ni kwa sababu Libya kwanza imegawanyika na haina serikali moja ya kitaifa. Pili, nchini Libya tayari kuna mujahidina 5,000 katika maeneo ya mwambao nao wanaunga mkono ISIS. Idadi hii inazidi kukua pamoja na kudhibiti uzalishaji na uuzaji mafuta. Kwa hiyo wenzao wa Iraki na Syria wanaweza wakakimbilia Libya na kuanzisha kambi ya mafunzo huko.

Katika hali kama hii Libya inaweza kuwa makao makuu mapya ya ISIS. Kutoka hapa mujahidina wanaweza wakasambazwa kuelekea nchi za Kiarabu, Afrika ya Kaskazini, ya Kati, Magharibi na hata Mashariki. Wanaweza kuendeleza harakati zao katika nchi kama Nigeria, Niger, Chad, Mali, Mauritania na Sudan. Pia Libya imepakana na Tunisia na Algeria ambako tayari kuna mujahidina wenzao.

Wanaweza wakaelekea hadi nchi za Ulaya. Ikumbukwe kuwa kisiwa cha Italia kiitwacho Lampedusa ni maili 200 tu kutoka Libya. Hili ni tishio kubwa kwa nchi za Magharibi.

Hivyo, kinachotia hofu na wasiwasi zaidi kwa mataifa ya NATO ni kuwa hawa mujahidina wa Daesh wanaweza kutumia Libya ili kuvuka Bahari ya Mediterania na kuingia Ulaya ambako tayari kuna vijana watakaosaidiana na wenzao kutoka Libya. Ikumbukwe kuwa Daesh ni kikosi cha kimataifa na wala si Waarabu peke yao. Inasemekana wametoka nchi 60 duniani.

Nchini Libya majeshi yanadhibiti sehemu kubwa mashariki mwa nchi, wakati makundi kadha ya mujahidina yako magharibi ambako wameunda Baraza la Vijana wa Kiislamu (Majlis Shura Shabab Al Islam – MSSI). 

Ni mwezi uliopita tu Daesh walifanikiwa kudhibiti machimbo mawili ya mafuta maeneo ya mashariki ambayo yanazalisha asilimia 80 ya mafuta yote ya Libya. Inakisiwa kuwa Daesh ina wapiganaji takriban 3,000 na wanadhibiti kilometa 300 za mwambao. Wengi wao ni kutoka nje ya Libya na wamekuwa wakipigana nchini Iraki na Syria. Novemba walipouchukua mji wa Darna walianza kubomoa maduka ya manukato na mapambo ya kina mama, pamoja na saluni.

Wengi wao ni wafuasi wa Gaddafi ambao waliingia ‘mitini’ baada ya rais wao kuuawa Oktoba 2011. Ni sawa na wafuasi wa Saddam Hussein (Iraki) ambao walijiunga na Daesh baada ya rais wao kukamatwa mwaka 2003 na baadaye akanyongwa.

Leo wakati NATO inajitayarisha kuivamia Libya kwa mara ya pili, AU nayo inamteua Kikwete kusuluhisha kwa njia ya amani. Inatukumbusha mwaka 2011 wakati AU pia ilijaribu kuzuia mashambulizi ya NATO, lakini ikashindwa.

Februari 23, 2011 wakati vurugu zipoanza nchini Libya, Baraza la Amani na Usalama la AU (PSC) lililaani utumiaji nguvu kukandamiza maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wa Gaddafi. Hata hivyo, Baraza hilo halikukubaliana na msimamo wa NATO wa kuivamia kijeshi Libya.

Machi 10, 2011 PSC ikaandaa mpango wa kuzuia vurugu kwa njia ya maridhiano. Pande zote zilitakiwa ziache kutumia silaha, badala yake zianzishe mazungumzo ya amani. Kamati ya AU ikateuliwa ili kufuatilia jambo hili kwa kuonana na mahasimu.

Kamati hiyo ikaandaa safari ya Libya, lakini nchi za NATO zikawasilisha azimio katika Baraza la Usalama la UN. Azimio namba 1973 likapitishwa. NATO ikaandaa majeshi yake kwenda Libya kuweka kile walichokiita marufuku ya ndege kurushwa ndani ya nchi hiyo (no-fly zone). Nchi tatu za Kiafrika zilikuwamo katika Baraza hilo; nazo ni Afrika Kusini, Nigeria na Gabon. Licha ya azimio la AU nchi hizo zilikubaliana na azimio hilo bila kujali kuwa AU ilikuwa na mpango mwingine wa maridhiano. 

Hata hivyo, Kamati ya AU ikakutana mjini Nouakchott tarehe 19 Machi na wakapanga safari ya kwenda Libya siku inayofuata. Ikawa inasubiri kupata kibali cha ndege yao kuruhusiwa kuingia Libya kwa mujibu wa azimio la UN.

Ndipo Aprili 10 na 11 Kamati ikazuru Libya. Katika Mji Mkuu  wa Tripoli wakakutana na Gadaffi ambaye akakubali mkakati wa AU. Kisha wakaenda Benghazi ambako waasi nao wakakubali kuacha mapigano ili kupisha uundwaji wa serikali ya mpito itakayosimamia uchaguzi ulio wazi na huru. Pia wafanyakazi na wageni kutoka nchi za Kiafrika walitakiwa wahakikishiwe usalama wao.

Baada ya hapo Kamati ikazuru Ufaransa, Uingereza, Ubelgiji, Italia  na Marekani ili kueleza mkakati wa AU na kuomba ushirikiano wa mataifa hayo ya NATO.

Wakati mchakato huu wa AU unaendelea, ghafla Agosti 21 waasi wa Benghazi wakaingia Tripoli. Kambi za kijeshi zikavamiwa na silaha zikaanza kutapakaa nchini kote. Yaliyofuata ni historia. 

Miaka mitano baada ya uvamizi wa mwaka 2011 takriban wananchi milioni mbili wa Libya wamelazimika kukimbilia nchi jirani za Tunisia na Misri. Hii ni theluthi ya wakazi wote. Waliobaki wanaishi maisha ya tabu, wakiwa wamepoteza makazi yao kutokana na vita baina ya makundi yenye silaha, baina ya Mashariki na Magharibi.

Uvamizi wa mwaka 2011 uliofanywa na NATO uliungwa mkono na asasi ya kimataifa kuhusu haki za binadamu (Human Rights Watch – HRW). Sasa, asasi hiyo hiyo inaripoti kuwa makundi yenye silaha nchini Libya yamekuwa yakiteketeza nyumba za raia. Wanawapora raia, wanawakamata, wanawatesa. Halhasili wanachokifanya ni uharamia wa kivita.

HRW inasema maelfu ya raia, wakiwamo wageni, wamefungwa gerezani bila ya kuhukumiwa, huku wakiteswa kila siku.Hivi sasa kuna kile wanachokiita “serikali ya umoja wa kitaifa” ambayo inatambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN). Lakini ndani ya nchi hakuna anayeisikiliza. Katika ukingo wa baharini ambako kuna mafuta, makundi ya mujahidina yameshika hatamu.

Nchi kwa hivyo imegawanyika katika sehemu mbili, kutokana na makundi ya waasi ambao walisaidiwa na majeshi ya uvamizi ya Marekani na Ubelgiji yalipoingia mwaka 2011. Kundi moja ni la mujahidina ambao walipewa misaada ya hali na mali. Marekani na Uingereza waliwapa mafunzo, silaha na fedha ili kumpindua Gaddafi.

Sasa Uingereza inafikiria kutuma wanajeshi 1,000 ili kuendesha mafunzo kwa jeshi jipya la Libya. Pia Italia inakusudia kutuma wanajeshi 6,000. Haiyumkiniki kuwa mujahidina (au Daesh) watakubali kufuata amri ya mabeberu hao. Hapo ndipo mpasuko utaongezeka na huo utakuwa uvamizi wa pili kwa Libya.

Katika hali kama hii ndipo Rais (mstaafu) Kikwete na jopo lake anatarajiwa kuwasuluhisha wananchi wa Libya.  Labda atafanikiwa. Lakini je, atafanikiwa kuwashawishi na wavamizi wa NATO?